Wednesday 16 October 2013

[wanabidii] Udhibiti wahamiaji haramu katika maeneo nje ya mikoa ya operesheni kimbunga

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

IDARA YA UHAMIAJI

Idara ya Uhamiaji ni moja ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyenye jukumu la kuhakikisha kwamba Ulinzi na Usalama wa nchi unaimarishwa. Katika kusimamia jukumu hilo kikamilifu, Idara ya Uhamiaji inatekeleza majukumu makuu ya Msingi yafuatayo:

i.  Kuwezesha na kudhibiti uingiaji na utokaji wa watu nchini
ii.  Kutoa huduma ya pasipoti au hati nyingine za safari kwa Watanzania wanaosafiri nje ya nchi kwa shughuli mbalimbali. 
iii.  Kutoa huduma ya Vibali vya kuishi nchini pamoja na Pasi mbalimbali kwa wageni wanaokuja nchini kwa shughuli mbalimbali.
iv.  Kufanya misako, doria, kubaini na kuwakamata wahamiaji haramu nchini na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria zilizopo. 
v. Kuratibu mchakato wa maombi ya wageni wanaoomba uraia wa Tanzania na kumshauri ipasavyo Mhe. Waziri wa Mambo 
ya Ndani ya Nchi kwa hatua ya uamuzi.

Majukumu hayo ndiyo yanaipatia Idara ya uhamiaji wajibu wa kulinda na kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi, sambamba na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Uwezeshaji na Udhibiti wa wahamiaji nchini
Tanzania ni nchi inayofahamika sana duniani kwa ukarimu wa watu wake, ardhi yenye rutuba, rasilimali mbalimbali na vivutio vingi vya aina yake kwa watalii. Tanzania pia kutokana na historia yake ya amani na utulivu pamoja na imani ya viongozi wake kuwa binadamu wote ni sawa na Afrika ni moja, Tanzania imekuwa ni kimbilio salama la wakimbizi wengi na wapigania uhuru kutoka mataifa mbalimbali Barani Africa.

Tanzania pia inazidi kuwa kivutio kwa wageni wengi kutokana na kuwa na fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, madini, utalii n.k. Hata hivyo, si wageni wote wanaoingia nchini wanafuata taratibu za kiuhamiaji katika kipindi chote cha kuwepo hapa nchini. Hivyo, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inakabiliwa na changamoto ya kuwepo wahamiaji haramu. 

Wahamiaji haramu hao wanatokana na makundi makuu yafuatayo:

Wahamiaji haramu walioingia nchini kabla ya uhuru pamoja na vizazi vyao.
 Wengi walikuja kama manamba katika mashamba ya wakoloni. Ingawa wengi wao wamefariki, lakini vizazi vyao bado vipo. Wahamiaji haramu wa aina hii wengi wanapatikana katika mikoa mingi ya mpakani, Tanga, Pwani na Morogoro. Hawa kwa mujibu wa historia yao ni miongoni mwa wahamiaji "walowezi" hapa nchini. Kazi kubwa inayofanywa na Idara ya Uhamiaji ni kuwatambua, kuwaandikisha na baadae kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu hatua za kuchukua.  

Wahamiaji haramu wanaotokana na kuwepo kwa makambi ya wakimbizi na wapigania uhuru nchini.  

Baada ya nchi nyingi kupata uhuru, wapigania uhuru wengi waliondoka, lakini baadhi vizazi vyao bado vipo hapa nchini na baadhi ya vizazi hivyo vinaishi isivyo halali nchini.

 Aidha, wengine ni wale walioishi nchini kama wakimbizi na baadae kutorejea nchini kwao pamoja na vizazi vyao. Wengi wa wahamiaji haramu hao wapo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora, Rukwa, Mtwara Ruvuma, Morogoro.

Katika kuwashughulikia Wahamiaji haramu wa aina hii, Idara imeweka utaratibu wa kuwatambua kwa kuwaandikisha katika madaftari maalum ili kuwa na kumbu kumbu zao sahihi na baadae kuishauri Serikali kuhusu hatua za kuchukua. Madaftari haya yameisaidia Serikali kuwatambua Wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kagera na Kigoma wakati wa Operesheni "Kimbunga" inayoendelea hadi sasa.

Wahamiaji wanaozidisha muda wa ruhusa ya kuwepo nchini.
Hawa ni Wahamiaji wanaoingia nchini kihalali na kupewa muda maalum wa kuwepo nchini. Baadhi yao muda huo unapokwisha hawaondoki, wanaendelea kuishi kwa kujificha na kuukimbia mkono wa sheria. Wahamiaji haramu wa aina hii wanashughulikiwa kwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa nchini.

Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Hawa ni wale ambao wanaingia nchini bila kufuata taratibu zozote za Uhamiaji. Wengi wao wanatumia njia zisizohalali wakati wa kuingia nchini. Kundi hili linahusisha Wahamiaji haramu wengi waliopo katika maeneo ya mipaka yetu na nchi jirani pamoja na makundi ya Wahamiaji haramu wanaoingia nchini kutoka nchi za Pembe ya Afrika (Somalia na Ethiopia). 

Wahamiaji haramu wa aina hii wanashughulikiwa kwa kuwasaka, kuwakamata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani na kuwaondoa nchini.

Udhibiti wa Wahamiaji haramu katika maeneo yaliyopo nje ya Mikoa ya "Operesheni Kimbunga"
Wakati wa utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la kuwataka majambazi, majangili na wamiliki wa silaha kinyume cha sheria kujisalimsha na Wahamiaji haramu walipo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita kurudi nchini kwao kwa hiari, Idara ya Uhamiaji iliendelea na shughuli za udhibiti wa wageni katika kipindi hicho kwenye Mikoa iliyopo nje ya eneo la operesheni. Katika shughuli hizo za udhibiti wa wageni, Jumla ya wahamiaji haramu 6,653 kutoka mataifa mbalimbali wamekamatwa na kuchukuliwa hatua mbali kwa mujibu wa sheria. Mataifa ya Wahamiaji hao haramu na idadi yao kwenye mabano ni kama ifuatavyo:- Malawi (3,778), Burundi (696), Congo DRC (1,739), Kenya (147), Uganda (20), Pakistan (12), Somalia (31), Nigeria (23) na Msumbiji (20). Wengine ni India (16), China (09), Rwanda (40), Ethiopia (97), Komoro (10), Uturuki (03), Afrika Kusini (02), Bukina Faso (01), Liberia (02), Italia (01), Singapore (01), Libya (01), Bulgaria (01), Ghana (02) na Syria (01).

Wengi wa Wahamiaji haramu hao wameondolewa nchini, wengine wamefikishwa mahakamani wakati wengine uchunguzi dhidi yao bado unaendelea. Aidha, wapo walio halalisha ukaazi wao nchini wakati wengine wameorodheshwa kwa ajili ya hatua zaidi. 

Watanzania Wahamiaji haramu katika nchi nyingine.
Wakati Tanzania ikiendelea na udhibiti wa Wahamiaji haramu nchini, takwimu zilizopo zonaonesha kwamba wapo watanzania ambao nao wanakiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi mbalimbali wanazokwenda, ikiwemo kuingia na kuishi katika nchi hizo wakiwa Wahamiaji haramu. 

Katika kipindi cha mwaka 2012, Jumla ya watanzania 1,263 walirejeshwa nchini kutoka mataifa mbalimbali. Aidha, katika kipindi cha Januari-August, 2013 jumla ya watanzania 715 wamerejeshwa nchini kwa makosa ya kukiuka taratibu za Uhamiaji katika nchi walizokwenda, hususan Afrika Kusini.

Kwa kuwa sasa tunaishi katika ulimwengu ambao watu wanasafiri kutoka nchi moja hadi nyingine kuliko kipindi chochote kile katika historia ya binadamu, tunapenda watanzania nao wasafiri nje ya nchi kwa ajili ya kunufaika na fursa mbalimbali na tumekuwa tukiwawezesha kufanya hivyo. Pamoja na nia hiyo njema ya Serikali, tunatoa wito kwa watanzania wenzetu kuheshimu Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo katika nchi wanazo kwenda, kama ambavyo tunapenda wageni nao waheshimu Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo hapa nchini. Kufanya hivyo sio tu kwamba kutatujengea uaminifu na uadhilifu katika jamii ya watu tunaoishi nao ugenini, bali pia kutajenga jina zuri na heshma kwa nchi yetu miongoni mwa mataifa mengine. 

Sote tufahamu kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuvumilia Wahamiaji haramu, bila kujali wanatoka taifa gani. Kila nchi inajitahidi kukabiliana na changamoto hii ya Wahamiaji haramu. Tofauti ni mbinu zinazotumika kulingana na mazingira na uwezo wa nchi husika. Ndio maana kwa mazingira ya jiografia ya nchi yetu, mapambano dhidi ya Wahamiaji haramu ni endelevu bila kujali kama kuna operesheni maalum au ni katika hali ya utendaji kazi wa kawaida. 

Hitimisho:
Suala la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni la kila mwananchi. Vyombo vya Ulinzi na Usalama peke yake haviwezi kutekeleza jukumu hili bila ushirikiano wa karibu na wananchi. Wahamiaji haramu hawana kisiwa chao wenyewe, bali wanaishi ndani ya jamii.  Tunawashukuru wote waliotupatia ushirikiano katika kutekeleza majukumu yetu na tunaomba tuendelee kushirikiana kuanzia mwananchi mmoja mmoja, viongozi wa ngazi mbalimbali, wanahabari pamoja na vikundi mbalimbali vya kijamii.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment