Friday 18 October 2013

[wanabidii] Ndege ya fastjet yarudi Dar kwa kushindwa kutua Mwanza baada ya taa kuzimika

KUZIMIKA kwa taa katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza juzi kulisababisha ndege ya fastjet kushindwa kutua na kulazimika kurejea jijini Dar es Salaam.

Inaelezwa kwamba ndege hiyo iliyopaswa kutua saa 2 usiku kwenye uwanja huo ikitokea jijini Dar es Salaam, ilishindwa
 kutua na kulazimika kuzunguka hewani mara tano, hali inayodaiwa kuleta taharuki miongoni mwa abiria.

Habari zinadai kuwa kukosekana kwa umeme katika uwanja huo kulisababisha kutokuwapo kwa mawasiliano, hivyo kuzua tafrani kubwa kwa baadhi ya abiria.

Baadhi ya abiria waliosafiri na ndege hiyo waliieleza Tanzania Daima kwamba wengi walikumbwa na hofu ya kuzama katika Ziwa Victoria.

"Tuliogopa sana baada ya kuona ndege imeanza kuzunguka zunguka angani, na tukahofia kuwa huenda tukatumbukia ziwani, maana uwanjani haukuwa na umeme.

"Nilianza kusali huku mapigo ya moyo yakinienda mbio sana. Maana rubani angeweza kushuka ziwani kwa kuona taa za wavuvi," alisema abiria mmoja ambaye hakutaja jina lake.

Hata hivyo, baadhi ya abiria na wadau wengine wa usafiri, akiwamo Mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje na Meneja wa Shirika la Bima la Jubilee Mkoa wa Mwanza, Jared Owando, walieleza kusikitishwa na taarifa za kukatika kwa umeme kwenye uwanja wa ndege.

Walisema kwamba, kitendo hicho kinapaswa kudhibitiwa, ikiwa ni pamoja na uongozi wa uwanja huo kuwajibika kikamilifu, ili tatizo hilo lisijirudie tena, kwani hali hiyo ni hatari katika usalama wa abiria na ndege kwa ujumla: "Siku hiyo mimi nilifika Mwanza mapema usiku na ndege ya Precision kutoka Dar. Lakini baadaye nikaarifiwa kwamba kuna ndege imelazimika kurejea Dar es Salaam kwa sababu uwanja una giza. Sasa najiuliza, hakuna jenereta uwanjani hapo?" alisema Jared.

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Easter Madale, alipoulizwa jana kwa njia ya simu kuhusiana na tatizo hilo, alikiri kutokea hitilafu ya umeme hivyo ndege hiyo kupata usumbufu ikiwa angani, na kusema hilo ni tatizo la kawaida: "Ni kweli siku hiyo kulikuwa na hitilafu ya umeme, hivyo mawasiliano yakakosekana! Umeme ulikatika na jenereta la TCAA halifiki huku kwetu…na sisi hapa jenereta yetu ni ndogo haina nguvu sana," alisema meneja huyo.

Miaka kadhaa iliyopita iliwahi kutokea ajali mbaya, baada ya ndege ya mizigo kutoka Ulaya iliyokuja kubeba samaki kutumbukia ndani ya Ziwa Victoria, kutokana na kukosekana kwa umeme na mawasiliano uwanjani hapo.

--- via Tanzania Daima

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment