Monday 14 October 2013

[wanabidii] MMETUPORA KILA KILICHO CHETU, TUACHIENI NYERERE WETU

MMETUPORA KILA KILICHO CHETU, TUACHIENI NYERERE WETU
Na Mwl. Sabatho Nyamsenda

Wanyonge walia, waporaji washerehekea

Siku ya leo nchi yetu inaadhimisha miaka 14 tangu kuondokewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.Hivyo, leo ni siku ya furaha na huzuni; ni siku ya harusi na matanga. Kwa waporaji, wanyonyaji, wabaguzi wa rangi, wadini na wakabila, leo ni siku ya kunywa mvinyo na kusherehekea. Ule mwiba uliowachoma siku zote na kuwakosesha raha hatimaye uliondoka siku kama ya leo, nao wakapata nafasi ya kutamba.

Kwa wanyonge – wakulima wadogo, wafugaji wadogo, warina asali, waokota makopo, wafagia barabara, wabeba zege, machinga, mama ntiliye, wafanyakazi wa ngazi za chini,  na wote wanaoishi katika dhiki na kukosa huduma bora za afya, maji, elimu na malazi – leo ni siku ya huzuni. Lile jabali lililoongoza mapambano yao hatimaye lilistaafu rasmi kazi ya kupambana 
siku kama ya leo. Nyerere, msemaji wa wanyonge, akaacha kusema. Kambarage, mshairi wa makabwela, akaacha rasmi utunzi wa mashairi. Julius, mfasiri wa vitabu, akaweka kalamu chini huku akiwa amekamilisha kutafsiri kwa Kiswahili kitabu cha mwanafalsafa wa Kiyunani, Plato, kiitwacho ''The Republic''. Mwalimu wa wanyonge akakoma kufundisha. Akatulia tuli. Akalala usingizi wa kudumu.

Tufurahie maisha yake kuliko kuomboleza kifo chake

Je, ni sahihi kwa wanyonge kulia? Ni haki kwa wanyonge kuomboleza? Kulia na kuomboleza ni haki ya kila ampotezae mpendwa wake. Lakini kwa kuwa Nyerere alikuwa binadamu wa kawaida na sio malaika aliyeshushwa toka angani hatukutegemea kwamba ataishi milele. Binadamu huzaliwa, hukua, huzeeka, huugua, hufariki. Ndicho kilichotokea kwa Mwalimu. Pengine siku ya leo yapaswa kuwa siku ya kufurahia maisha ya Mwalimu kuliko  kuhuzunikia kifo chake. Kwa maana hiyo, siku kama ya leo twapaswa kuzitafakari kwa kina fikra zake na jinsi tutakavyozitumia kuendeleza mapambano ya wanyonge.

Nyerere hajafa, sisi ndio Nyerere
Aina hii ya kumwenzi kiongozi wa mapambano kwa kuendeleza yale aliyoyapigania niliiona kwa Wavenezuela walipoondokewa na shujaa wao wa mapinduzi ya kidemokrasia, rais wa wanyonge, Hugo Chavez, alipofariki mwezi machi mwaka huu. Nilipowaona katika televisheni mamilioni ya wanyonge wa Venezuela wakitiririkwa na machozi, nilidhani huo ndio mwisho wa mapinduzi ya kijamaa ya kibolivari (The Bolivarian Socialist Revolution) waliyoyaasisi wanyonge wa nchi hiyo wakiongozwa Chavez.

Kilichonitisha zaidi ni jinsi viongozi wa mataifa ya mabeberu, na hasa Barack Obama wa Marekani, walivyotoa kauli za kusherehekea kifo cha gwiji hilo la mapambano. Na mabeberu walikuwa na haki kushangilia kifo hicho kwani ni Chavez aliyehakikisha kuwa utajiri wa mafuta ya nchi hiyo unaenda kuwafaidisha wanyonge kwa kuwapatia hudumu bora za kijamii zisizo na malipo. Mawakala wa ubeberu nchini Venezuela wakisaidiwa na majasusi wa Marekani walijaribu kumpindua Chavez lakini mamilioni ya wanyonge waliandamana hadi aliporejeshwa madarakani.

Lakini kauli za wanyonge wa Venezuela zilinipa matumaini: pamoja na kutiririkwa machozi, walipohojiwa na waandishi wa nchi za Magharibi juu ya kifo cha kiongozi wao, walijibu: ''Chavez hajafa. Sisi ndio Chavez''. Kwa kauli hiyo wanyonge walikula yamini kuendeleza mapinduzi ya kijamaa na kuhakikisha kuwa utajiri wa nchi yao unaendelea kuwafaidisha wanyonge badala ya kikundi kidogo cha mawakala wa mabeberu na mabwana wao.

Tena wanyonge wa Venezuela wameonyesha mshikamano wa kitabaka na wanyonge wa nchi nyingine kama Cuba, Ecuador, Nicaragua na Bolivia ambazo zote zinaongozwa na serikali za kijamaa. Mathalani, Cuba yenye madaktari wengi waliobobea huwapeleka Venezuela ili kutoa huduma za afya kwa wanyonge mijini na vijijini, wakati Venezuela ikiipatia Cuba mafuta kwa bei rahisi na kuisaidia kiuchumi ili iondokane na hali ngumu inayosababishwa na vikwazo vya Marekani.

Kambarage mpinga unyanyasaji

Historia ya Kambarage inaonyesha kuwa tangu akiwa mdogo alichukia kila aina ya uonevu, ubaguzi, unyanyasaji na ukandamizaji. Akiwa mtoto mdogo, Kambarage alikuwa akimsindikiza mama yake shambani ; mama akiwa analima, Kambarage alikuwa akimbembeleza mdogo wake. Huruma ilikiwa ikimwingia Kambarage kumwona mama yake akifanya kazi za suluba siku nzima bila kupumzika. Hivyo akabuni mbinu ya kumpumzisha mama yake. Akawa anamfinya mdogo wake, na kitoto kile kichanga kikawa kikitoa kilio kikali, kilio kilichomfanya mama adhani kuwa kichanga yule ana njaa. Hivyo, mama akaacha kulima na kuja kumnyonyesha mwanawe. Kamnyonyesha mtoto, lakini pia kapumzika. Kambarage alitabasamu na kujiona mshindi, hata kama ushindi wenyewe ulikuwa wa muda mfupi tu.

Miaka mingi sana baadaye kitoto hiki, ki-Kambarage, sasa akiwa kijana wa umri wa miaka 22 na mwanafunzi wa Makerere aliandika insha ya kiswahili iliyoitwa ''Uhuru wa Wanawake''. Ndani ya insha hiyo kijana Julius aliichambua na kuilaani mifumo ya jamii zetu za Kiafrika iliyokuwa ikiwakandamiza na kuwanyanyasa wanawake kana kwamba wao si binadamu kamili. Na ni mfumo wa kikoloni ulichochea moto na kuhalalisha mfumo dume.
Insha hiyo, ambayo ambayo ilishinda tuzo ya Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki kwa wakati huo, na sasa imechapwa katika kitabu, inaishia na kisa cha kifaranga cha tai kilichochanganywa na kuku, kikalishwa chakula cha kuku, hata chenyewe kudhani ni kuku. Lakini tai huyo alipopelekwa kilimani na mtaalamu wa wanyama, na kuambiwa: tai, wewe sio kuku, kwako ni angani, hivyo ruka uende angani. Tai akaruka na kupotelea mawinguni. Kwa kutumia mfano huo, Nyerere akawataka wanawake kutokubali madhila ya mfumo kandamizi unaowaaminisha kuwa wao ni kuku, warukia chini, ilhali wao ni tai, warukia juu. Hivyo walipaswa kuruka na kupaa.

Hata hivyo mtazamo wa Mwalimu haukuwa finyu kwa kudhani kuwa ni wanawake pekee ndio waliokandamizwa na kunyimwa fursa. Mfumo wa kibepari, ambao kwa wakati huo ulichukua sura ya ukoloni, uliwakandamiza wanyonge wote, wake kwa waume, katika Afrika na mabara mengine. Hivyo, wanyonge wote walipaswa kupambana na kuushinda ukoloni. Ndio maana Nyerere alikuwa mbele kuongoza mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa rangi na ukandamizaji, katika Afrika na dunia nzima kwa ujumla.

Julius asiyenunulika

Shuleni Tabora, Julius alipewa ukiranja. Hii ilitokea baada ya yeye kuamua kuacha shule kutokana na kunyamazishwa na mwalimu mkuu wakati wa mdahalo. Kambarage alikuwa ametoa hoja za kupinga uonevu na unyonyaji wa serikali ya kikoloni hali iliyomwudhi mwalimu mkuu wa kizungu na kumwamuru akae chini. Kwa nini anyamazishwe? Mwanafunzi huyo aliamua kufunga virago vyake na kurudi kwao lakini utawala wa shule kwa kushirikiana na serikali ya kikoloni walimkatiza na kumrudisha shuleni kisha wakampatia uongozi.

Kama walimu wa kikoloni walidhani kwa kumpa ukiranja walikuwa wamemnunua Julius basi walikuwa wakiota ndoto mchana kweupe. Ukiranja wa shule ulimpa Kambarage haki ya kupata nusu lita ya maziwa kila siku, ilhali wasio viranja walipata robo lita. Ni Kambarage, si mwingine, aliyeongoza mgomo wa wanafunzi kupinga ubaguzi huo na kudai wanafunzi wote wapate mgao sawa wa maziwa. Mgao huwa wa kibaguzi ukakoma. Tayari Nyerere alishaanza kupigania usawa. 

Miongo kadhaa baadae serikali ya kikoloni ilimpatia ujumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (ubunge kwa wakati huo). Walidhani wamemnunua na kumnyamazisha. Lakini alipoona hoja zake hazipewi nafasi Nyerere alijiuzulu ubunge huo na kuyarejea maisha yake ya dhiki aliyokuwa akiishi baada ya kuacha kazi ya ualimu. Alikataa kuwasaliti wanyonge.

Kipo kisa katika kitabu cha Mohamed Said kiitwacho Uamuzi wa Busara wa Tabora kinachoonyesha maisha aliyoishi Nyerere baada ya kuacha kazi ya ualimu iliyokuwa na mshahara mnono kwa wakati huo ili kuongoza mapambano ya uhuru. Familia yake ikakosa hata mlo wa kueleweka. Siku moja, akiwa hana hata senti moja mfukoni, Mwalimu aliamua kutembea kwa mguu toka nyumbani kwake Magomeni hadi Kariakoo, akitegemea huenda atabahatisha kupata chakula. Njiani akakutana na mzee Msume Kiate, mwana TANU ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza samaki. Baada ya kusikiliza shida ya Mwalimu, mzee Kiate akampatia shilingi mia mbili akanunue mahitaji yake. Na baada ya hapo mzee Kiate na wana TANU wenzake walijitolea kuihudumia familia ya Mwalimu kwa chakula na wakaendelea kufanya hivyo hata baada ya uhuru kupatikana. Tunapomkumbuka Nyerere tunapaswa pia kuwakumbuka mashujaa wengine, kama Mshume Kiate, ambao vitabu vingi vya historia havitaji majina yao.

Mwalimu Nyerere, kiongozi wa makabwela

Kitabaka, Mwalimu hakuwa katika kundi la makabwela. Kwa kuzaliwa katika familia ya kichifu tayari alikuwa na fursa ambazo watoto wengine hawakuwa nazo. Moja ya fursa hizo ilikuwa elimu. Lakini elimu ikamfungua na kuiona dunia. Kadiri ilivyomfungua ndivyo ilivyomtenganisha na watu wake. Toka Butiama akaenda Musoma, toka Musoma akapita Mwanza, Shinyanga hadi Tabora. Akavuka mipaka ya kijiji na mikoa. Akavuka mipaka ya nchi, akaenda Uganda. Akavuka mipaka ya bara, akaenda Uingereza. Elimu yake haikumvusha mipaka ya ramani tu bali mipaka ya kitabaka. Kadiri alivyoongeza vidato na shahada ndivyo alivyolihama tabaka la "walalahoi".

Lakini japokuwa kitabaka alikuwa katika "walalahai" kabla ya uhuru, na kuhamia katika "walalaheri" baada ya uhuru, Mwalimu mwenyewe aliamua kwa makusudi kabisa kuliasi tabaka lake. Hivyo usomi wake haukuwa na bei (exchange value) bali ulikuwa na thamani (use value). Katika fikra za Mwalimu, msomi anayejitapa kuwa yeye hawezi kutumika kwa wanyonge mpaka alipwe kiasi fulani cha fedha huyo si binadamu kamili bali ni mtumwa. Binadamu pekee mwenye bei na anayeuzika sokoni ni mtumwa.

Ndio maana hata baada ya kutoka Uingereza, akiwa Mtanganyika wa kwanza kupata shahada ya umahiri (master's degree), Mwalimu hakuhangaika kutafuta fursa za kujitajirisha na kuishi maisha ya anasa. Kwa kuwa maslahi hayo ya kitabaka alishayaaga haikuwa vigumu kwake kuachia nyadhifa zenye malipo manono ili akawapiganie wanyonge.

Hata baada ya kukaa Ikulu kwa zaidi ya miaka 20, alifanikiwa kujenga kajumba kadogo na ka kawaida kabisa kijijini Butiama, na nyumba yake ya Msasani aliijenga kwa mkopo ambao hata hivyo  alishindwa kuumalizia, na kuiomba serikali imalizie mkopo na kuchukua nyumba hiyo. Serikali ya Mwinyi ikafanya hivyo lakini ikampatia Mwalimu nyumba hiyo. Mwaka 1966 Mwalimu alikata mshahara wake kwa asilimia 20. Wakati huo alikuwa akipokea shilingi 5,000/=, hivyo akabakia na shilingi 4,000/= na hakuwahi kujiongezea mshahara mpaka anaondoka madarakani. Hivyo, wapo watumishi wengi kabisa wa serikali, wakiwemo maprofesa, waliopokea mshahara mkubwa kumzidi.

Azimio liliwajali wanyonge
Lakini kutopenda mali inaweza kuwa hulka ya mtu yeyote kabisa. Mkristo au mwislamu mzuri, anayeamini katika pepo ya baadae, hawezi kujikita katika anasa za kidunia. Ila Nyerere alifanya hivyo si kwa sababu ya ukristo wake, ila kwa sababu ya itikadi iliyomwongoza, itikadi ya kijamaa. Ndiyo maana, baada ya kuwaona viongozi wenzake wanatumia nyadhifa zao kujitajirisha, aliasisi Azimio la Arusha, ambalo pamoja na mambo mengine liliwazuia viongozi kumiliki nyumba za kupangisha, kupokea mishahara miwili au zaidi na kumiliki hisa au kuwa wakurugenzi katika kampuni za kibepari.

Kupitia Azimio la Arusha, njia kuu za uzalishaji-mali na rasilimali za taifa, kama viwanda, mabenki, misitu, madini, ardhi, njia na vyombo vya usafiri wa anga, reli na maji, viliwekwa mikononi mwa umma. Umma wa wanyonge ulichagua serikali kwa njia ya kidemokrasia, serikali ambayo ilipewa jukumu la kusimamia rasilimali hizo kwa niaba ya wanyonge. Faida inayozalishwa ilitakiwa kwenda kuwahudumia wanyonge, na sio kikundi cha watawala. Azimio lilisisitiza juu ya kuwajali wakulima vijijini, na kuonya juu ya misaada kutoka ughaibuni.

Azimio likahujumiwa na kupinduliwa
Kama inavyofahamika, wanyonge, wake kwa waume, vijana kwa wazee, waliandamana nchi nzima kuunga mkono Azimio la Arusha. Lilikuwa ramani yao kuelekea nchi ya usawa na matumaini. Lakini hata hivyo, utekelezaji wa Azimio uliwekwa mikononi mwa watu walewale walioanza kujitajirisha. Japo katika miaka ya 1970 sera za kijamaa zilifanya vema na serikali ikaanza kuonyesha mafanikio katika kutoa hudumu bora kwa jamii bila malipo, hali ilibadilika katika kipindi cha miaka ya 1980.

Nchi za kibeberu, Marekani na Uingereza, zilishikwa na waumini wa sera za uliberali mambo-leo na hivyo kuzilazimisha nchi maskini kufuata sera hizo kwa kubinafsisha kila kilichotaifishwa, kufuta ruzuku katika kilimo na vyakula, na kuacha mara moja kutoa huduma zisizo na malipo. Ndani ya nchi, tena Mwalimu akiwa bado madarakani, sera hizi zilipata mashabiki wengi. Wachache walijionyesha waziwazi. Wengi walijificha na kuendelea kuhujumu chini chini. 

Nchi ikiwa imetoka vitani, bidhaa za msingi zikawa hazipatikani. Zilikuwa zimehodhiwa na kikundi cha watu wachache, baadhi wakiwa katika dola na baadhi nje ya dola. Hivyo, baada ya vita vya Uganda, Mwalimu alikuwa na vita viwili vya kupigana: vita dhidi ya wahujumu uchumi/ujamaa ndani ya nchi, na vita dhidi ya mabeberu nje ya nchi. Makundi hayo yalikuwa yakishirikiana kwa ukaribu sana, na hata yakafanikiwa kuupindua Ujamaa baada ya Mwalimu kung'atuka.

Sera za kiporaji

Uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ya utekelezaji wa sera za uliberali mambo-leo umetuonyesha kuwa mfumo huu ni katili zaidi pengine kuliko hata biashara ya utumwa na ukoloni. Rasilimali za wanyonge zinaporwa, na wanyonge wanapojaribu kupinga hutumiwa majeshi na serikali zao au za mabeberu. Tumeyaona hayo nchini mwetu. Pia tumeyaona barani kwetu na duniani kote mifano ikiwa ni uvamizi wa Libya na Iraq uliopelekea kuchinjwa kwa viongozi wa nchi hizo, na mamilioni ya wanyonge kuuawa.

Akihutubia mjini Mbeya katika sherehe za Mei Mosi mwaka 1995, Mwalimu aliziita sera za ubinafsishaji na uwekezaji kuwa ni za kinyang'anyi. Akasema kuwa zitazalisha mabilionea, lakini watakuwa wachache. Lakini pia zitazalisha maskini, na hao watakuwa wengi sana. Hayo ndiyo yatokeayo nchini mwetu na duniani kote.

Jengeni sanamu zake, sisi tutazienzi fikra zake
Mwaka mmoja kabla ya kufariki Mwalimu alikuwa ametabiri kuwa ipo siku Tanzania itarejea katika misingi ya Azimio la Arusha. Katika Kongamano la kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha, Profesa Issa Shivji naye pia alisisitiza juu ya uwepo wa dalili zinazoonyesha kuwa Watanzania walio wengi wameanza kupigania kurudi katika misingi ya Azimio la Arusha lakini akaonya kuwa dalili hizo zinaweza kuzimwa na kakundi ka watu wachache kanakofaidika na mfumo uliopo.

Nafikiri kuwa miongoni mwa mbinu za kuzima dalili hizo ni kuhodhi jina la Mwalimu huku wakijidai wanamuenzi. Eti wanamuenzi kwa kuongeza idadi ya sanamu zake, na taasisi na viwanja vyenye jina lake ilhali Mwalimu mwenyewe alishakataa hayo tangu akiwa hai. Wakijidai kugusia fikra zake basi wanamhubiri kama mpenda amani na umoja. Lakini ni Mwalimu mwenyewe aliyesema kuwa mahali pasipo na haki (justice) wala usawa (equity) hapawezi kuwa na amani. Pia hauwezi kuwa na umoja kati ya wanyonyaji/waporaji wachache na mafukara wengi.

Ili nisionekane nabandika maneno katika mdomo wa Mwalimu, nitanukuu sehemu ya hotuba yake aliyoitoa mwezi mei mwaka 1989 wakati akifungua semina ya wazalishaji wakubwa iliyoandaliwa na Chama cha Mapinduzi:

"Si kwamba Azimio la Arusha limeondoa umaskini hata kidogo, wala halikutoa ahadi hiyo. Azimio la Arusha limetoa ahadi ya matumaini. Ya haki, ahadi ya matumaini kwa wengi, ndio watu wengi wa Tanzania wanaendelea na kuwa na matumaini hayo. Madhali yapo matumaini hayo, mtaendelea kuwa na amani… Kama wengi hawana matumaini, tunajenga 'volcano'. Siku moja italipuka na lazima ilipuke. Isipokuwa watu hao wajinga. Wengi wa nchi hiyo wajinga, wanakubali kutawaliwa hivi hivi. Kuonewa hivi hivi na wingi wanao, wajinga hao. Kwa hiyo, Watanzania hawa watakuwa wajinga, wapumbavu, kama wataendelea kukubali kuonewa na watu wachache katika nchi yao. Kwa nini?''


Waporaji wa rasilimali za nchi, wavunaji wa jasho la wanyonge, vibaraka wa mabeberu (wasemao 'tunapendwa huko nje') hawana haki ya kutumia jina la Mwalimu. Wametupora kila kilicho chetu (tangu viwanda, ardhi, madini hadi nyumba), wamewanyang'anya wanyonge haki ya kupata huduma bora za afya, elimu, malazi na chakula. Hawa hawana haki ya kutaja jina la Mwalimu. Njia ambayo wanyonge wanaweza kumuenzi Mwalimu ni kwa kuzichambua kwa kina fira zake, na hasa Azimio la Arusha, na kuzitumia kama silaha ya mapambano!

Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma. Anapatikana kwa barua-pepe: sany7th@yahoo.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment