Monday 21 October 2013

[wanabidii] BIDHAA BANDIA NI JANGA LA KITAIFA!

Tatizo la bidhaa za bandia nchini Tanzania ni sawa na uji kwa mgonjwa. Kwa mujibu wa takwimu za serikali 40% ya bidhaa zote zinazouzwa katika nchi hii ni za bandia. Nadhani kwamba tatizo hili ni kubwa zaidi ya tunavyoaminishwa na takwimu hizi. Yawezekana bidhaa bandia katika masoko yetu ni zaidi ya 40% kwani mimi sijawahi kuziona wala kuzinunua. Mimi ni mhanga mkubwa wa bidhaa bandia pengine kuliko mtu yeyote katika nchi hii.

Ni muda mrefu sasa mamlaka zinazohusika zimeshindwa kupunguza ama kutokomeza kabisa tatizo la bidhaa bandia katika masoko ya Tanzania. Wanunuzi wanazidi kupata hasara kwa kununua bidhaa feki huku wafanyabiashara wakineemeka na haijulikani ni lini hasa tatizo hili litapatiwa ufumbuzi au dawa ya kudumu.

Ni ajabu kwamba mamlaka zinazohusika kudhibiti bidhaa bandia zimeshindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi na weledi wa kutosha kwa kuachia bidhaa zisizokuwa na ubora kuingizwa nchini.  Nchi hii imegeuzwa 'Jalala la Bibi' kwamba kila anayejisikia kuagiza bidhaa bandia hufanya hivyo bila woga wowote. Masoko yamejaa bidhaa hafifu na hivyo kuzidi kuporomosha uchumi wetu na kuwatia hasara wanunuzi wa bidhaa hizo. Na tatizo ni kwamba sio rahisi kutofautisha bidhaa bandia na bidhaa halisi kwani bado wananchi hawajapewa somo la kutosha jinsi ya kuweza kutambua bidhaa feki.

Kibaya zaidi ni kwamba hata dawa bandia nazo huingizwa na kuuzwa hapa nchini kwa wingi na dawa hizi zimerundikana kwenye maduka ya dawa huku wauzaji wa dawa hizo wakiwa hawachukuliwi hatua zozote za kisheria. Dawa bandia ni mbaya kuliko bidhaa yoyote feki kwani dawa hizi husababisha usugu wa magonjwa na hivyo kuwafanya wagonjwa wasipone hata pale wanapotumia dawa halisi.

Wakati umefika sasa serikali iwaonee huruma wananchi wake wanaoumizwa na bidhaa bandia. Zitungwe sheria kali za kudhibiti uagizwaji, uingizwaji na uuzwaji wa bidhaa bandia nchini mwetu. Watu wanaokamatwa wakiuza dawa bandia za mimea, mifugo au binadamu wanyongwe kwani watu hawa ni wabaya kuliko wauaji.

0 comments:

Post a Comment