Friday 4 October 2013

[wanabidii] Al Shaabab Na Chimbuko La Ugaidi ( VII)


 

Kwanini Tanzania inahitaji kuwa makini?

Leo tunajadili nafasi ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ugaidi duniani. Na ni kwa kuangalia historia  inavyoihusisha Tanzania na harakati za kupambana na maadui wa chini kwa chini.
       

Bila shaka, kwa kuingalia historia, sura ya dunia imekuwa ikibadilika katika vipindi tofauti. Itakumbukwa baada ya Vita Kuu ya Pili, dunia ilipitia kipindi cha vita baridi . Kulikuwepo pia na kundi la nchi zisizofungamana na upande wowote. Tanzania ilikuwa mwanachama wa kundi hili.  Hata hivyo, nyingi ya nchi hizi kimsingi zilikuwa na upande zilizoegemea
kati ya makundi mawili niliyoyataja.

Katika miaka ya 60 kulikuwa na mapambano ya kiitikadi baina ya kambi mbili kuu kiitikadi ulimwenguni; kulikuwa na NATO ikiongozwa na Marekani na Warsaw Pact ikiongozwa na Urusi. Yalikuwa ni mapambano kati ya mifumo ya Ukomunisti na Ubepari katika dunia.

Katika hili, Marekani, na  kwa sababu za kimaslahi imekuwa na historia ya kuingilia mambo ya ndani ya  nchi za Kiafrika ili kuchunguza na pengine kusimamisha kasi ya kuenea kwa itikadi za Kikomunisti. Mapinduzi  mengi barani Afrika katika miaka ile ya 60 yamekuwa yakipangwa na  kufadhiliwa na Shirika la kijasusi la Marekani, CIA.

Shirika hilo lilikuwa likiwatumia mawakala wake barani Afrika na  sehemu nyingine za dunia kutekeleza mipango ya mapinduzi. Viongozi wengi wa kimapinduzi barani Afrika ama waliuawa au kulazimika kuzikimbia nchi zao na kuwapisha viongozi vibaraka waliopandikizwa na CIA. Nchi ya Kongo ambayo  baadae ikaja kujulikana kama Zaire ni mfano wa mabadiliko ya uongozi yaliyodhaminiwa na CIA. Patrick Lumumba, kiongozi mwanamapinduzi wa Kongo aliuawa kinyama na kuzikwa kusikojulikana.

Tunasoma pia, kuwa Marekani na hususan kupitia Shirika lake la
ujasusi la CIA ilijiingiza kwa mara ya kwanza katika siasa za Zanzibar mara
baada ya mapinduzi ya 1964  kwa lengo la  kupunguza kasi ya kuenea kwa
Ukomunisti.  Marekani iliingiwa na hofu ya Zanzibar kama kisiwa  kutumiwa na
Wakomunisti. Katika Zanzibar, bado kuna kumbukumbu ya historia hii kwa
kuyaangalia  majina kama Uwanja wa Mao Tse Tung, hospital ya V.I Lenin,
shule za Fidel Castro, Patrick Lumumba na mengineyo. Yote haya yalikuwa na
mwelekeo wa  kambi ya Warsaw; ukomunisti.

Mvutano wa kiitikadi kati ya Warsaw na NATO  uliendelea kuwepo
hadi pale ukuta wa Berlin uliopoangushwa Agosti 23, 1989. Huo ndio ulikuwa
mwisho wa vita baridi ya dunia. Marekani ikabaki bila mpinzani wa kiitikadi.
Kuanzia hapo upepo wa kisiasa uligeuka ghafla, wimbi la demokrasia ya vyama
vingi likaanzia Ulaya Mashariki na kuikumba Afrika.

Katika kipindi cha miaka ile ya 60 hadi miaka ya 70 Tanzania kama
nchi ilikuwa ni "Taifa Kubwa" barani Afrika. Tanzania ilikuwa ni moja ya
nchi zilizoaminika na kuheshimiwa sana kwa uwezo wake katika ulinzi wa jumla
(Total Defence). Mwalimu Nyerere alichukuliwa kama msemaji wa Bara la Afrika
na aliongoza harakati za mapambano ya ukombozi ikiwemo ya kukabiliana na
mamluki na majasusi.

Tanzania ilihesabika kama moja ya nchi zenye uwezo mkubwa wa
kijeshi ikiwa ni pamoja na umahiri wa kukabiliana na maadui wa chini kwa
chini. Ni wakati ule ambapo Afrika ilikumbwa na wimbi la mamluki, askari wa
kulipwa waliokuwa wakitumiwa na mataifa makubwa katika kupindua serikali
halali za nchi za Kiafrika. Kwa lugha nyingine, tunaweza kusema kuwa mamluki
ndio magaidi wa jana.

Tanzania iliweza kutuma vikosi vyake hata katika nchi nyingine za
Kiafrika kuzima majaribio ya mapinduzi yaliyofanywa na Mamluki. Nchi ya
Seyshelles ni mfano mmoja wapo. Kutokana na uwezo huo wa kijeshi wa 
Tanzania ikiwemo uwezo wa kukabiliana na mamluki haikuwa jambo la bahati
mbaya kwa Tanzania kukabidhiwa dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa Kamati Ya
Ukombozi. Kamati  Muhimu ya uliokuwa  Umoja wa nchi hutu barani Afrika, OAU.
Hata Makao Makuu ya Kamati hiyo yalikuwa Dar Es Salaam yakiongozwa na
Brigedia Hashim Mbitta. Ni kutokana na uwezo huo wa Tanzania kukabiliana na
mamluki na hata majasusi vyama vingi vya ukombozi barani Afrika viliifanya
Dar Es Salaam kuwa Makao Makuu yake.

Kama ilivyokuwa katika miaka ile ya 60, ndivyo ilivyo sasa. Hakuna
tena masuala ya ndani ya Tanzania , Zimbabwe, Uganda au Ushelisheli. Dunia
imebadilika. Yanayotokea Dar Es Salaam, Kampala na Nairobi  yanaihusu Idara
ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, Shirika lake la ujasusi CIA na hata FBI.
Yanahusu pia masuala ya usalama wa nchi zetu.

 

 Mathalan, tukio la Agosti 7 la kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani katika ardhi ya Tanzania lilipunguza  idadi ya watalii na wawekezaji kwa kuhofia usalama wao. Huenda isingekuwa
rahisi kwa tukio lile kutokea Dar Es Salaam kama Tanzania ingekuwa na uimara
ule ule wa kukabiliana na maadui wa chini kwa chini kama ilivyokuwa katika
miaka ya 60 na 70. Katika miaka ile isingekuwa rahisi kwa wahusika kufanya
tukio lile na kufaulu kutoka nje ya mipaka yetu kirahisi.

Tukirudi kwenye mtiririko wa matukio, tunaona kuwa kati ya mwaka
1990 hadi 1998 tulishuhudia kuwepo kwa ombwe la kiitikadi (idelogical
vacuum). Agosti 7, 1998, sura ya dunia ilianza kubadilika. Ni mara ile
balozi za Marekani Nairobi na Dar Es Salaam zilipolipuliwa. Septemba 11,
2001 sura ya dunia ilibadilika ghafla, pale kikundi cha kigaidi cha Alqaida
kilipofanya maangamizi makubwa katika miji ya Washington na New York.

Kwa Marekani adui Ukomonisti alishafutika machoni, aliyejitokeza sasa ni adui mpya mwenye  nguvu za kutisha, ugaidi wa kimataifa ukiongozwa na Alqaida ya Osama Bin Laden. Marekani na washirika  wake wameweka bayana, kuwa wamo katika vita dhidi ya ugaidi katika kila kona ya dunia.
           

Leo inafahamika, kuwa mmoja wa waliotuhumiwa na tukio la
kulipua ubalozi wa Marekani Dar Es Salaam ni kijana Ghailan aliyekamatwa Pakistan
  na alitokea Zanzibar, hususan Mji Mkongwe.

Bila shaka, Tanzania kama nchi ina nafasi ya kutumia uzoefu wake katika kupambana na ugaidi kama utaingia ndani ya mipaka yake, na hata kuchangia vita dhidi ya ugaidi
duniani. Itaendelea...

 

Maggid.

0754 678 252

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment