Wednesday 9 October 2013

Re: [wanabidii] “Kwa Heri Dr. Hashim Msafiri Twakyondo...Umefundisha Wengi”

Poleni sana familia, ndugu, jamaa, marafiki na familia ya chuo kikuu cha DSM.
Apumzike kwa amani.


2013/10/9 Mathew Mndeme <mathewmndeme@gmail.com>

Ijumaa  ya tarehe 4/10/2013 wiki iliyopita tulikua kwenye kikao cha kazi ambacho kilihusisha wahadhiri wote wa kitivo chetu na kilifanyika hadi jioni kabisa. Alikuwepo mmoja wa wahadhiri waandamizi ambaye wengi wetu tulikua hatujaonana naye kwa muda mrefu wala kumuona kwenye vikao. Mwaka jana alikua amechukua likizo ndefu kwa ajili ya kazi za kitaaluma na baadaye nadhani alikua ana mambo mengine nje ya eneo la kazi na nje ya nchi pia, hivyo kutoonekana mara kwa mara. Nakumbuka pale kwenye kikao alikua amekaa sambamba na nilipokua nimekaa na tulipoona muda umekwenda sana na kikao kikiendelea nilimuuliza kikao kinakwenda hadi saa ngapi naye akanijibu hajui ila muda umesogea sana. Kwa kuwa hali ya chumba cha mkutano ilikua ina joto nilipata kiu sana na niliamua kwenda kuchukua maji ambapo naye alinimba nimpe chupa moja. Nakumbuka kuna kamati ndogo iliundwa kufuatilia jambo fulani na yeye alikua mmoja wa waliombwa kutoa mchango wake kwenye hiyo kamati kutokana na uzoefu na maarifa yake jambo ambalo alilikubali. Baada ya kikao kwisha kamati ile ndogo ilikaa kwa dakika chache kujadili lile jukumu. Tulipoagana pale eneo la kikao ilikua inakaribia saa kumi na mbili hivi za jioni.

Kesho yake (Jumamosi ya tarehe 05/10/2013) asubuhi na mapema tukapigiwa simu na kuambiwa kuwa Dr. Hashim Twakyondo amefariki dunia. Kusema ukweli nilishtuka na nilibisha kwanza kuwa huenda habari sio za kweli huku nikiendelea kuuliza maswali yasiyo na mpangilio. Tulipouliza, tukaambiwa kuwa hiyo asubuhi ya Jumamosi alimka kwa lengo la kwenda shamba hivyo akaondoka yeye na mke wake na mtoto wao wa mwisho wa kiume ambaye ndiye alikua anaendesha gari. Alionekana mzima wa afya na asiye na tatizo lolote. Lengo ilikua ni wapite kwanza gereji kuweka gari sawa halafu waende shamba. Wakiwa ndio wametoka tu nyumbani eneo la Makuburi akaanza kuwaambia kuwa anajisikia vibaya na baada ya muda wakaona kama anaishiwa nguvu. Wakaamua wampitishie hospitali ya Amana maana ni njia waliyokua wanaipita. Ila kabla hawajafika hospitalini ikawa ndio keshatangulia kule kifo kinapopelekaga roho za watu. Ilinisumbua sana na kuwaza huenda Dr. Twakyondo alikuja kwenye kikao kile kutuaga, na siyo yeye wala sisi tuliogundua hilo. Labda kwa baadhi yetu ingekua rahisi kupokea habari za msiba ule iwapo tusingekutana naye jioni ile kwa vile hatukua tumemuona kwa muda mrefu.

Dr. Twakyondo amekitumikia chuo Kikuaa cha Dar es Salaam kwa takribani mika 30 akipanda nfazi kutoka mkufunzi hadi mhadhiri mwandamizi. Pamoja na kazi yake ya kitaaluma, amekua kiongozi kwa muda mrefu akiongoza idara ya Kompyuta Sayansi kwa miaka trakribani saba na baadaye kuwa mkurugenzi wa kitendo cha elemu mtandao cha Chuo Kikuu kwa miaka sita. Mafanikio haya ni ushahidi tosha kua amefanya mengi ya kukumbukwa na kuondoka kwake ni pengo kubwa litakalochukua muda kuliziba.

Tulipokua tunaaga mwili nyumbani kwake juzi Jumatatu, watu walikua ni wengi sana, kitu kilichodhihirisha Dr. Twakyondo alikua mtu wa aina gani kwenye jamii. Wasifu wake uliposomwa yalijulikana mambo mengi aliyokua ameyafanya, kuyafanikisha na mengine ndio alikua kaanza kuyafanya hasa kwenye utaalamu wake katika tasnia ya Sayansi ya Kompyuta. Kwa wale amboa wamepita katika fani hii, na ukweli kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndio kitovu cha fani ya Kompyuta katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, wataungana nami kuwa Dr. Tywakyondo alikua ni Mwalimu wa wengi na alifanya mengi kwa sehemu yake.

Kama ilivyokua kwangu tangu niliposikia msiba huu, kila niliyemsikia pale msibani alikua anasikitishwa na namna alivyoondoka. Wengi walikua na huzuni kuwa ameondoka kwa haraka, kwa kushtukiza, na pasi kujulikana ugonjwa na huenda. Kifo kimemshtukiza kama kilivyowashtua aliowaacha. Mzee Yusuph Makamba akiwa kama sehemu ya wanafamilia/jamaa zake alipewa nafasi ya kuongea. Kama kawaida ya ucheshi wake aliongea mengi lakini mojawapo alisema kuwa marehemu alikua anajiandaa kuwa mbunge wa jimbo fulani mwaka 2015. Akasema yeye ndio alikua anaongoza kamati ya fitna kuhakikisha hilo linafanikiwa pamoja na marehemu kupata cheo kingine ndani ya chama. Akasema kuwa Ijumaa kabla hajafariki walikua wamewasiliana kuwa walikua waonane Jumapili ili ampe taarifa mpya za fitna za kuelekea 2015 na kuweka mikakati vizuri zaidi.

Pamoja na hili la siasa, kwa upande wa kazi nilikua nina taarifa  kuwa marehemu ndio alikua amenza kupitia mchakato wa kupandishwa cheo na kuwa uprofesa ambayo ni ngazi ya juu kabisa katika taaluma.

Ninapoombeleza kifo cha Dr. Twakyondo na jinsi alivyokua na yale niliyoyosikia wakati wa mazishi yake juu ya aliyoyafanya na mipango aliyokua nayo, napata mawazo mengi juu ya maisha baada ya kifo. Sio tu kwa ajili ya nini kitatokea na kuendelea kwenye roho yangu baada ya kufa, bali juu ya wale tunaowaacha na jinsi watakavyoathiriwa na kuondoka kwetu. Ninapata maswali mengi; Je marehemu alikua amejiandaa kiasi gani kuwa atakufa? Alikua ameweka mambo ya nyumba yake vizuri kama matayarisho ya kuondoka kwake? Katika yale yote aliyojishughulisha nayo, nini kitaendelea katika kutokuwepo kwake?

Sina majibu ya maswali haya na wala sijajishughulisha kuyatafuta. Lakini kama mwanadamu ninawaza tu kuwa huenda Mwalimu wangu hakuwahi kuwaza kuwa kuna kufa karibuni. Huenda alikuangalia kufa kama tukio la baada ya uzee uliotukuka akiwa kama profesa na mwanasiasa aliyestaafu iwapo ni kweli  ndiko alikokua anakwenda kama alivyotuambia Mzee Makamba. Wengi wetu huwa tunaposikia kuwa wengine wamekufa, tunasikitika na kuombeleza halafu tunaishia hapo. Tunapojifikiria sana tunaona  kufa kwa upande wetu bado ni jambo la baadaye sana na hivyo hatujishughulishi kufanya matayarisho yoyote ya nini kiendelee baada ya kufa kwetu. Tunawaza huenda kufa kwetu utatokea baada ya matukio mengine kadha wa kadha kwenye maisha yetu.

Kwa wale wanaamini katika Mungu  na kuwa kuna mwisho wa maisha haya ya damu na nyama, wako wanaojitahidi sana kukesha katika maombi na utakatifu kuwa iwapo siku ya tukio ikifika basi wakutwe wako tayari na wana wasifu wa kuwawezesha kuyaendea yale makao mapya na ya milele. Ila sina hakika kama wengi wanapiga hatu ya pili na kuajiandaa pia namna ya kuziacha familia zetu na mambo mengine sawa iwapo tutakufa muda wowote. Wengi wetu tunawaza tu juu ya yale yatakayotokea kwetu na nini twatakiwa tufanye kuamua hayo...lakini huenda hatuwazi kabisa juu ya wale tutakaowaacha na kupunguza madhara ya kutokuwapo kwetu kwenye maisha yao.

Shuhuda ni nyingi za familia ambazo baada ya baba au mama kufariki, ulikua ni mwanzo wa kila kitu kukaa kushoto. Kumekua ni mwanzo wa watoto kuharibika/kuharibikiwa; imekua ni mwanzo wa kifo cha biashara, huduma au kampuni ambayo aliyefariki aliwekeza maisha yake yote kuendeleza; imekua ni mwanzo wa hali ya maisha ya familia kubadilika; Imekua ni mwanzo wa watoto na mke/mume kuachwa kwenye mateso na masumbufu mengi; imekua ni mwanzo wa kesi zisizoisha za kugombea mali; Imekua ni mwanzo wa magomvi yasiyo na kikomo; na mengine mengi. Haya yote yanatokea kwa sababu ya ubinafsi wetu unaotusukuma kujiwazia mema sisi wenyewe na kufanya bidii kubwa kuziandaa roho zetu bila kujua kuwa jukumu letu haliishii hapo.

Huenda mawazo yangu haya hayakua sahihi kunisumbua kipindi hiki, lakini namna kifo cha Mwalimu wangu Dr. Hashim Twakyondo kilivyotokea, kinanilazimisha kutokuwaza haya. Pamoja na ugumu wa kukubali kuondoka kwake, kifo chake kinaniambia kuwa kuna haja ya kujiandaa maana ulimwengu huu sio wetu na hatuna mkataba wa kukaa kwa kipindi fulani au milele. Hivyo basi pamoja na mipango mizuri tuliyonayo tunalazimika kuwaza yatakayoendelea iwapo kuondoka kwetu kutakuja bila taarifa kwetu sisi wenyewe au kwa wale tutakaowaacha. Mtu mmoja aliwahi kusema kuwa, "twalazimika kufanya kazi kama vile tutaishi milele na kuishi kwa tahadhari kama vile tunakufa kesho".

Kwa heri Mwalimu wangu Dr. Hashim Msafiri Twakyondo. Tanzania imejaa wataalamu wengi wa fani ya Sayansi ya Kompyuta ambao kwa namna moja au nyingine walikuswa na utumishi wako katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani.

 

MM


--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment