Friday 14 June 2013

[wanabidii] TAMKO LA CHADEMA DHIDI YA SIASA CHAFU ZA CCM

Ndugu wanahabari 

Kwanza tunawashukuru nyote kwa kukubali na kuitikia wito wetu, kama ambavyo imekuwa ada. Leo tunapenda kutumia fursa hii, kuzungumzia suala moja, ambalo litakuwa na 'matawi' kadhaa yatakayoweza kulifafanua suala hilo.....

Sasa anguko la CCM kwa kukosa sera na hoja liko wazi mno

Kwa takriban wiki kadhaa sasa, CCM kupitia kwa mtu mmoja anayeitwa Lameck Madelu Nchemba Mwigulu na wenzake kadhaa, wakiwemo wakubwa wake na wadogo zake kazini, wamekuwa wakipita pita huko, hasa yale yenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani zinazoendelea maeneo mbalimbali nchini, wakijianika namna gani ambavyo chama hicho sasa ni mufilisi na hakina hoja tena mbele ya Watanzania. Chama hicho kimekuwa kikitembea na mtu mmoja ambaye kimemgeuza kuwa bango 'jipya' la propaganda za siku zote za hovyo za chama hicho zinazokiuka hata misingi ya haki na kudhalilisha heshima na utu wa mwanadamu, kikidai kuwa alimwangiwa tindikali na CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa Igunga, Tabora. 

Tunasema, kama chama hiki kimefikia mahali kimekosa hoja na sera za kuwaambia wananchi wachache sana wanaodiriki kwenda kutazama mikutano yake, badala yake kinamgeuza binadamu aliyepaswa kuwa hospitali, ni dalili ya kiwango cha juu cha kufilisika kisera na hoja, hivyo kuanza kufanya viroja, hivyo kudhihirisha anguko la wazi la chama hicho. Wanahabari, mtakumbuka kuwa katika moja ya mikutano yetu na ninyi (au wenzenu katika vyombo vya habari nchini) kule Igunga, tuliwahi kutoa ufafanuzi wa suala hili hili, linalomhusu huyo kijana anayeitwa Musa anayetembezwa na Mwigulu Madelu Lameck Nchemba. 

Tulionesha kwa ushahidi ambao CCM hawawezi kuupinga wala kuukanusha, kuwa ukatili wa kumwagiwa tindikali aliofanyiwa kijana huyo wanayetembea naye, ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa mbinu walizopewa vijana wa green guards, waliowekwa kwenye makambi ya Ulemo, kule Singida, Nzega na Uyui, wakifundishwa mbinu za kijeshi ili kushughulikia wapinzani.
 Upo ushahidi wa kutosha kuwa vijana hao wa CCM, chini ya ushirika wa baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola, walipewa mafunzo ya kuua, kutumia silaha, tindikali, asidi, kuteka, kutesa, kuumiza na hata namna ya kutumia sindano kwa ajili ya kuua kwa sumu au kusambaza virusi vinavyosababisha Upungufu wa Kinga Mwilini. 

Mara kadhaa sasa, tumekwenda mbali na kutoa hadi mfano mmoja tu wa silaha inayomilikiwa na CCM, ambayo ililetwa na kupelekwa kwenye kambi hizo. Tumetaja aina na namba yake na nchi ilikotoka na kwamba iliingizwa nchini bila kibali, tukamtaka Amiri Jeshi Mkuu atuambie nani alitoa ruksa kwa CCM kuwa na kikundi cha kijeshi, kumiliki silaha ambazo zimekuwa zikitumiwa na vijana wao kudhuru watu? Hadi leo hawajawahi kutoa majibu!
 Aidha, mtu huyo anayeitwa Lameck Madelu Mwigulu Nchemba, anapita huko akidanganya bila haya kama ilivyo kawaida yake kuwa CHADEMA kimekuwa kikiua watu kwenye mikutano yake na hadi sasa kimeua watu wanane. Ametaja matukio kama ya Morogoro, Igunga, Iringa na Ndago, huko Singida. 

Anaivua zaidi nguo CCM, Rais Kikwete na serikali yake 

Mtu yeyote makini au anayefikiriwa kuwa makini asingeweza kusema uongo wa wazi kama anaofanya Lameck Madelu Mwigulu Nchemba. 
Katika hotuba za Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, hususan katika bajeti ya mwaka 2012/2013 na 2013/2014, tumeonesha kwa ushahidi wa wazi namna ambavyo CCM na serikali yake imekuwa ikishiriki katika vitendo viovu dhidi ya raia wasiokuwa na hatia kwa kuua au kufanya majaribio ya kuua, kuteka na kutesa. 

Kwa uchache matukio hayo ni; mauaji ya mwanachama wa CHADEMA, Mbwana Masoud aliyetekwa, kuteswa na kuuwawa huko Igunga wakati wa uchaguzi mdogo, Msafiri Mbwambo, kiongozi wa CHADEMA kule Arumeru Mashariki, aliyeuwawa kwa kuchinjwa shingo kisha baadhi ya silaha zilizotumika kukutwa kwa kiongozi wa CCM na tukio la kuuwawa kwa Ali Singano Zona, kuke Morogoro. 

Kuna tukio la jaribio la mauaji baada ya wabunge wa CHADEMA, Hyness Kiwia na Salvatory Machemli kuvamiwa na kundi la wana CCM wakiwa na mapanga na mashoka, kisha kuanza kuwashambulia viongozi hao mbele ya polisi waliokuwa na silaha, lakini hawakuchukua hatua yoyote. 

Tukio la Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa kushambuliwa kwa silaha na watu wanaodaiwa kutumwa na Diwani wa CCM, Idd Chonanga.
 

Aidha, tukio la Yohana Mpinga anayesemakana kuwa kiongozi wa UVCCM ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA kata ya Urughu, aliyeuwawa kwenye vurugu huko Ndago, Singida. Pia tumeeleza namna ambavyo watu wengine wasiokuwa wanachama wala viongozi wa vyama vya siasa nao wamefanyiwa unyama, wa kuuwawa, kutekwa, kuteswa na majaribio ya kuuwawa, bila serikali hii ya CCM kuchukua hatua, wakiwemo Kiongozi wa Madaktari, Steven Ulimboka, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, Mwandishi wa Habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi. Matukio ni mengi mno.
 

Hatukuishia kuorodhesha matukio na ushahidi, tulienda hatua mbele na kuitaka serikali hii ya CCM ifanye uchunguzi huru wa matukio hayo ya vifo vyenye utata, utekaji na utesaji wa binadamu. Tulimtaka Rais Jakaya Kikwete atumie mamlaka yake ya kikatiba, kuunda tume huru ya kijaji/kimahakama kuchunguza matukio yote hayo ili hatua za kisheria zifuate kwa wote watakaobainika kuhusika. Ameshindwa hadi leo.
 

Hivyo kwa mtu huyo aitwaye Lameck Madelu Mwigulu Nchemba kuendelea kupita barabarani akijaribu kuyahusisha matukio yanayofanywa na CCM na serikali yake, huku akijua inatakiwa kufanya uchunguzi huru, ni kuitanganzia dunia kuwa Rais Kikwete hana uwezo wa kusimamia uongozi bora na demokrasia ya kweli, na kukivua nguo chama chake kwa kuonesha jinsi kisivyowesa kuwajibika hata katika haki ya msingi kabisa ya binadamu; uhai wake!


Wao wanashindwa; sisi tunasonga mbele 

Kuna aina mbili (walau kwa muktadha wa leo) za kushindwa kwa CCM na sasa tunawataka wakae mkao mzuri wa kukalia benchi la upinzani. Wajigunze kuwa wapinzani.
 Kwanza kushindwa kabisa kuwashawishi wananchi wanaoendelea kuwakataa katika uchaguzi huu wa marudio wa madiwani katika kata 26. Hakuna haja yabkwenda mbali kujua kuwa CCM wamezidiwa kabisa kwa hoja, sera na mikakati ya kampeni kwa wapiga kura. 

Ndiyo maana wameanza tayari kutumia vikundi vya kufanya majaribio ya mauaji, kuteka, kutesa, kushambulia kwa silaha na kuumiza.
 Mifano hai ni makambi yaliyoanzishwa Mbeya mjini na tayari yameanza kuleta madhara ambapo usiku wa kuamukia jana, watu wetu walioko Kata ya Mabalamaziwa, wamevamiwa na kukatwa mapanga na watu wa CCM! Pili, ni kushindwa kwa hoja na sera zao. Wananchi wamezidi kuwakataa na kwa kweli katika uchaguzi huo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika kesho kutwa, yaani Jumapili ya Juni 16, wananchi wa maeneo mbalimbali wanakwenda kuwapiga CCM kikumbo ambacho hawataamini.

Kama ilivyoshindwa katika kudhibiti ufisadi na ubadhirifu kwa kusimamia uwazi na uwajibikaji, CCM inazidi kudhihirisha kushindwa katika siasa za hoja na sera, ndiyo maana imeamua kufanya kampeni za majitaka ya mtaroni, huku ikilazimika 'kuitangaza' CHADEMA zaidi kuliko kusema imefanya nini kwa miaka 52! Kama ambavyo CCM imeshindwa kusimamia ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania, badala yake inazidi kufanya maisha ya wananchi wanyonge kuwa maskini zaidi kupitia bajeti mbovu inazowasilisha bungeni kila mwaka, pia sasa inadhihirisha kuwa ni mfilisi wa siasa za ukweli na kutafuta dhamana ya uongozi. 

CCM hii iliyoshindwa hata kusimamia maamuzi ya vikao vyake vilivyoazimia kujivua magamba ya ufisadi, haina uwezo wala ushawishi wa kuwazuia au kubadili mawazo ya Watanzania ambao wameamua kuiunga mkono CHADEMA na kumiliki harakati za Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) na kukitaa chama hicho cha zamani. Wanahabari, mtakumbuka kuwa dalili za CCM kuishiwa sera na hoja na kukimbilia kwenye siasa chafu, za maji ya mtaroni (gutter politics) hazikuanza leo kwa kuihusisha CHADEMA. Walianza kwa masuala ya ukabila, udini, ukanda, ambayo yote yalishindwa na sasa wamekuja na masuala ya utekaji, utesaji na mauaji, maana la ugaidi nalo limeshindwa baada ya Lwakatare kuwashinda mahakamani. Ndugu wanahabari, tungependa kusisitiza kwamba CHADEMA katika kueneza sera sahihi, kuleta uongozi bora, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania, tutaendelea kusonga mbele kwa sababu ya nguvu ya umma inayosukuma kasi kubwa ya mabadiliko nchini. 

Siasa chafu tunawaachia CCM ili ziwe ziwe ni sababu ya ziada ambayo wananchi wataitumia kuendelea kuwakataa, ikiwemo kwenye kura za udiwani tarehe 16 Juni 2013. Aidha, wakati CCM wanaendelea kushindwa kutekeleza bajeti za maendeleo na pia kushindwa kuleta bajeti zenye kumsababishia mzigo wa gharama za maisha mwananchi, ambayo ni sababu nyingine ya wananchi kuichagua CHADEMA, ambayo imedhihirisha kuwa mbadala na tumaini jipya la Watanzania, sisi tutaendelea kusimamia maslahi ya Watanzania na kuwa sauti ya wanyone ambao wako tayari kuiona nchi yao ikipata mabadiliko makubwa ya kiutawala na kimfumo.

Imetolewa na:

Benson Kigaila(kny)

Kurugenzi ya Habari na Uenezi

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment