Thursday 16 May 2013

[wanabidii] Thamani ya Fedha Kenya 'Yawaachisha' Shule Wanafunzi Rombo

Thamani ya Fedha Kenya 'Yawaachisha' Shule Wanafunzi Rombo

Na Thehabari.com, Rombo

KUFANYA vizuri kwa thamani ya fedha ya Kenya (Kshs) tofauti na ile ya Tanzania (Tshs) kumechangia kwa namna moja kuiathiri Wilaya ya Rombo maeneo ya mpakani mwa Kenya na Tanzania kitaaluma kwa kile baadhi ya wanafunzi wa sekondari kuacha shule na kwenda kufanya vibarua vijiji vya jirani.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni mjini hapa kumebaini kuwepo na idadi kubwa ya wanafunzi wa sekondari wa shule za mpakani wanaotoroka shule, ama wengine kuacha shule kuendelea na shule baada ya kumaliza elimu ya msingi hata kama wamefaulu na kwenda kufanya vibarua mpakani kwa kuvutiwa na thamani ya fedha ya Kenya.

Uchunguzi uliofanywa katika sekondari za Ngaleku, Tanya, Holili, Nduweni na Urauri zote zilizopo maeneo ya mpakani mwa Kenya wilayani Rombo umebaini idadi kubwa ya wanafunzi huzikimbia shule kabisa na wengine kufanya utoro wa rejareja wawapo shuleni kwa malengo ya kufanya vibarua mpakani.

Kwa shule ya Sekondari Urauri kati ya wanafunzi 238 waliopangiwa kujiunga na shule hiyo kwa mwaka huu ni wanafunzi 178 tu ndiyo walioripoti huku idadi kubwa ikidaiwa kukimbilia nchi jirani ya Kenya kufanya vibarua anuai zikiwemo kazi za ndani na mashambani kwa kuvutiwa na thamani ya fedha nchini humo.

Licha ya idadi hiyo kutojiunga na shule na kudaiwa kukimbilia Kenya, baadhi ya wanafunzi waliojiunga na shule nao huendelea na utoro wa rejareja hasa kipindi cha msimu wa kilimo, mavuno na palizi na kwenda kufanya vibarua hali ambayo huathiri maendeleo ya kitaaluma kwa shule na wanafunzi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Holili, Benson Samizi alisema kati ya wanafunzi 140 waliofaulu na kupangiwa kujiunga na shule hiyo kwa mwaka huu ni wanafunzi 85 tu ndiyo walioripoti. Alifafanua kuwa 30 alipata taarifa waliamua kujiunga na shule nyingine huku idadi iliyobaki wakitokomea kusiko julika na shule inaendelea kuwatafuta.

Kwa upande wa Mkuu wa Sekondari ya Tanya, Victus Kiwango alibainisha kati ya wanafunzi 94 waliopangiwa kujiunga na shule hiyo kwa mwaka huu ni wanafunzi 79 tu ndiyo waliripoti shuleni. Aidha alisema utoro pia umeiathiri shule hiyo kitaaluma kwani matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana jumla ya wanafunzi 71 wamepata sifuri, hakukuwa na ufaulu wa daraja la kwanza wala la pili na wanafunzi wawili walipata daraja la tatu huku wanafunzi 18 wakipata daraja nne.

Mzazi mmoja aliyejitaja kwa jina la Protus Shirima alisema si wanafunzi pekee ambao huvutiwa na thamani kubwa ya fedha ya Kenya kwani hata wapo wazazi ambao hukimbilia kufanya vibarua Kenya vijiji vya mpakani kutokana na thamani ya fedha. Alisema kibaya zaidi wapo baadhi ya wazazi ambao huambatana na watoto wao katika vibarua hivyo ili kuongeza kipato cha familia.

"Mi nakushauri jaribu kuja msimu wa kilimo ukichanganya ukae eneo hili (Tarakea) utaona makundi makubwa ya wananchi wakivuka mpakani nyakati za asubuhi kuelekea Kenya kufanya vibarua na kurejea tena jioni...hali hii hufanyika vivyo hivyo wakati wa mavuno na palizi, fedha ya Kenya ipo juu na ndiyo inayotuvutia wengi," alisema Shirima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rombo, Judethadeus Mboya akizungumzia hali hiyo alikiri kuwepo na wimbi la wananchi kujiushisha na shughuli za mpakani maeneo hayo, japokuwa alisema wameanza utaratibu wa kuwatoza faini baadhi ya wazazi wanaoshindwa kuwazibiti watoto wao kiutoro shuleni kwa kuwatumia viongozi wa vijiji.

Aidha aliongeza kuwa ni vigumu kuwadhibiti wanafunzi kufanya shughuli za mipakani kwa kuwa wanapokwenda maeneo hayo hawaendi na sare za shule, ukiachilia mbali kuwa wapo baadhi ya wanavijiji wa Tanzania pia huendesha shughuli za kilimo nchini Kenya katika vijiji vya jirani.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com

Maelezo Picha:-
Masoko 1-2
-Sehemu ya Soko la Tarakea, Rombo. Soko hili ni miongoni mwa masoko yaliopo jirani na mpakani wa Kenya na Tanzania wilayani Rombo ambapo wananchi wa pande zote za mpaka huingia na kujipatia mahitaji yao kama wanavyoonekana.

-Mkuu wa Sekondari ya Tanya, Victus Kiwango akizungumza na mwandishi wa www.thehabari.com hivi karibuni wilayani Rombo. 

-Hizi ni baadhi ya njia zisizo rasmi kwenda nchini Kenya zilizopo eneo la Rongai, Rombo

____________________________________________________________________
Joachim Mushi, Mhariri Mkuu wa gazeti tando la Thehabari.com
Mail address:- mushi@thehabari.com/ jomushi79@yahoo.com/ info@thehabari.com
Mobile:- 0717 030066/ 0786 030066/ 0756 469470
Web:- www.thehabari.com  
          http://joemushi.blogspot.com

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment