Sunday 26 May 2013

[wanabidii] TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU MTWARA

TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUFUATIA HELE TETE YA USALAMA MJINI MTWARA

 

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD-Coalition), mtandao pekee unaoshughulikia usalama wa watetezi wakiwamo wanaharakati wa haki za biandamu na waandishi wa habari, umepokea kwa masikitiko makubwa vurugu kubwa zilizotokea mjini Mtwara na kusababisha vifo viwili  hadi sasa kulingana na taarifa zilizotufikia mpaka sasa. Tunaungana na familia za wafiwa na watu wote waliopata adha kufuatia vurugu hizo.

 

Baada ya kupata taarifa za vurugu hizo tulimtuma mwakilishi watu katika Kanda ya Kusini, mkurugenzi wa asasi mwanachama wa Mtandao, ambaye ametuletea taarifa kwamba miongoni mwa watu walioathirika na vurugu hizo  ni watetezi wenzetu hususani waandishi wa habari na wengine ambao japo hawakudhurika lakini wanaendelea kuitwa kwamba ni wachochezi kwa upande wa serikali na wasaliti kwa upande wa wananchi.

 

 Miongoni mwa walioathirika na kadhia hiyo ni Bw. Kassim Mikongolo mwandishi   wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), ambaye amechomewa nyumba yake.

Wengine ni Bw Hassan Simba, mwandishi wa Habari Leo ambaye pia ni mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mtwara na vile vile ambaye aliokolewa na Jeshi la Polisi baada ya kupata misuko suko. Na vivyo hivyo kwa mwandishi wa Uhuru Rashidi Mussa ambaye maisha yake yamo hatarini.

 

Waandishi waliotajwa wamechukuliwa tofauti na wananchi na mwishowe kuamua kuwaadhibu kwa kudhani kuwa wanapotosha ukweli wa madai yao. Hata hivyo mtandao kushirikiana na wanachama wake wanaendelea kulifuatilia suala hili kwa undani na kujua hali ya sasa kwa waandishi na watetezi wa haki za binadamu Mkoani Mtwara.

 

Mtandao wetu unaomba wakazi wa Mtwara na Watanzania wote kwa ujumla wawe watulivu katika kipindi hiki ambapo bado hali haijaonyesha kumalizika kwa mgogoro huo ambao umechukua miezi kadhaa sasa. Hata hivyo tunaomba mambo yafuatayo ili kulinda amani na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu waliopo katika eneo hilo.

 

1.      Jeshi la Polisi na Serikali kwa Ujumla

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu unapinga vikali matumizi ya nguvu hususani Jeshi la Polisi katika kutatua migogoro mbali mbali. Tabia hii imeongezeka na kusababisha madhara makubwa ikiwamo vifo kama ilivyokwisharipotiwa mara kadhaa. Tunaamini njia muafaka ni ya kutumia ushirikishaji na uwazi katika kufikia muafaka wa mikataba mbali mbali.

 

2.      Vyombo vya Habari

Vyombo vya habari vya umma vijue jukumu lao kwamba vinatakiwa kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi zao. Tunaamini kwamba kushambuliwa kwa waandishi hao kumetokana na kukosa imani kwa wale walioamua kujichukulia sheria mkononi na kuwashambulia waandishi ambao wao wanaamini wameegemea katika upande fulani. Tunawasihi waandishi wa habari wa vyombo vya umma siku zote wabakie katikati hasa inapotokea mgogoro katika ya wananchi na serikali.

 

3.      Asasi za Kiraia

Aidha tunatumia nafasi hii kuwasihi watetezi, wanaharakati na watendaji wa asasi za kiraia kuendelea kutimiza majukumu yao bila woga lakini pia kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kazi zao. Tunaamini wapo wenye lengo la kutumia matatizo yaliyojitokeza Mtwara ili kuzifanya asasi za kiraia zionekana kwamba ni za kichonganishi jambo ambalo ni uzushi mtupu.

4.      Wananchi wa Mtwara

Pamoja na kwamba madai yenu ni halali, tunawasihi siku zote mjaribu kuwavumilia watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari mnaowadhania wanapotosha ukweli wa madai yenu badala ya kuwachomea nyumba na kuwatishia.

 

Kwa zaidi ya siku tatu sasa waandishi wa habari, watetezi wengine na wanachi kwa ujumla wanaishi katika mazingira ya hofu kwa kushindwa kujua hatima ya maisha yo iwapo wataendelea kuwa mitaani kama ilivyozoelweka.

 

Ahadi Yetu

Mtandao unaahidi kutoa msaada kwa waandishi wote watakaokwamisha katika jitihada zao za kutaoa taarifa juu ya mgogoro huo na mingine kadhaa. Mtandao kwa kushirikiana na wanachama wake utatoa taarifa kamili baada ya siku chache zijazo.

 

Tunatanguliza shukrani za dhati kwa uelewa wenu.

 

sign.png

 

ONESMO OLENGURUMWA

MRATIBU MTANDAO WA

WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment