Saturday 6 April 2013

[wanabidii] Zitto Kabwe: Barua yangu JF kuhusu Lwakatare

Nimetafutwa na uongozi wa JamiiForums ili kutoa maelezo kuhusu barua iliyowekwa jukwaani inayoonyesha kuwa ndani ya chama kuna kutoelewana kuhusiana na msimamo juu ya kesi inayomkabili mmoja wa viongozi waandamizi wa chama Ndg. Wilfred Lwakatare, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama.

Maelezo yangu ni kama ifuatavyo:

  1. Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa chama mnamo tarehe 15 Machi 2013 kutaka chama kifanye uchunguzi wake wa ndani kuhusiana na ukweli wa video iliyowekwa kwenye mitandao inayoonyesha kuwa Kiongozi wetu mwandamizi anapanga mipango ya kumdhuru Mhariri wa moja ya magazeti hapa nchini. Sikuamini kabisa mambo yale na hivyo kutoa ushauri kwa chama kwamba tufanye uchunguzi wetu wa ndani ili kujiridhisha. Uchunguzi wa ndani ungetufanya kuweka mikakati wa namna bora zaidi ya kulinda chama dhidi ya njama zozote, za ndani au za nje ya chama.
  2. Mapendekezo yangu ndani ya chama kamwe hayakulenga kumtosa ndugu Lwakatare wakati huu anakabiliwa na changamoto hii bali yalilenga kuhakikisha kuwa wakati tunamlinda na kumtetea ili haki itendeke, lazima tuhakikishe kuwa chama hakitaathirika na sakata hili kwa namna yeyote ile. Ni jukumu letu kuhakikisha sura (image) ya chama inabakia salama maana hatujui mikakati (game plan) ya maadui zetu kisiasa hasa baada ya kauli zao kwamba chama kitakufa kabla ya 2015 ambayo imerudiwa rudiwa sana. Ni lazima kutilia shaka (doubt) kila linalotokea sasa kwa kulipima kwa jicho la mbele zaidi. Ikumbukwe maneno ya Mwenyekiti wetu "Mwenyekiti Freeman Mbowe anataka ikithibitika kuwa Lwakatare alishiriki kurekodi mkanda huo iwe kwa kurubuniwa, 'kushikishwa' au kuingizwa mkenge, itamlazimu kuwajibika kwa kosa la kukosa umakini" (Gazeti la Jamhuri).
  3. Barua ile ya tarehe 15 Machi 2013 ilikuwa ni ya ndani ya chama, haikuwa ya kiofisi bali ya Zitto Kabwe kwa chama, ilisainiwa na haikukusudiwa kuwa 'public'. Nimeshangazwa sana kusikia na baadaye kuona barua yenye maudhui kama yale yale ya barua yangu kwa Katibu Mkuu imewekwa mtandaoni. Barua imewekwa masaa machache baada ya kikao cha Kamati Kuu kwisha ambapo tuliweka msimamo wa pamoja wa chama juu ya namna bora ya kushughulikia suala la Lwakatare kama chama. Wakati mweka barua anadai kuwa kulikuwa na mgawanyiko katika kikao, ukweli ni kwamba ajenda hiyo haikuwa na mjadala wenye mgawanyiko kabisa na msimamo wa chama ulipatikana kwa mwafaka bila mgawanyiko. Ni dhahiri kuwa maadui zetu walitaraji mgawanyiko na baada ya kushindwa sasa wanatengeneza mgawanyiko huo kwa kusambaza uwongo wenye uzandiki.
  4. Baada ya kufanya uchunguzi mdogo nimegundua kuwa ID iliyoweka video ya Lwakatare mtandaoni na ID iliyoweka barua hii mtandaoni ni IDs za mtu mmoja. 'Coincidence' ya namna hii inashangaza na kushtusha, lakini inatuambia jambo moja kubwa 'kwamba kuna kirusi ndani ya chama kilicho karibu sana na viongozi wa chama chenye kazi moja tu, yani kuonyesha kuwa CHADEMA hapako shwari, kuna migogoro na hatimaye kusambaratisha chama'. Kirusi hiki lazima kina nafasi andamizi au kipo karibu sana na viongozi waandamizi. Inawezekana kabisa kirusi hiki kinahusika na suala zima la Lwakatare katika kupanga, kuendesha na kutekeleza mpango mzima. Maswali kama 'kwanini Dennis Msacky na Zitto ndani ya Video ya 'Lwakatare' lazima sasa yaanze kutafutiwa majawabu.
  5. Natoa wito tena kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA kwamba, huu ni wakati wa kuwa na umoja na mshikamano kuliko wakati wowote ule katika uhai wa chama chetu. Chama cha Mapinduzi kitatumia njia zote kutugawa, kutugombanisha na kupenyeza chuki miongoni mwetu katika juhudi za wao kubakia madarakani. Umakini wa Kiongozi huonekana wakati wa changamoto kama hizi!
  6. Msimamo wa chama umetolewa na Kamati Kuu iliyomaliza vikao vyake jana siku ya ijumaa tarehe 5 Aprili 2013. Huo ndio msimamo wangu pia! Kesi ya Lwakatare ipo mahakamani, chama kimeonyesha dhahiri kumwamini Jaji aliyekabidhiwa kesi hii, sasa tuache mahakama ifanye kazi yake na tusubiri hukumu. Msemaji wa chama kuhusu suala hili ni ndugu Tundu Lissu na amekuwa akitoa ufafanuzi kila inapohitajika.

Asanteni

--- 
Kabwe Z. Zitto

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment