Saturday 20 April 2013

[wanabidii] Nini kinaendelea Feri?


Jana nilikwenda Kigamboni, sijaenda huko muda kidogo umepita; nilishangaa sana sana niliyoyakuta Feri!!

Kwa bahati nzuri nilikuwa nimepewa lift, hivyo tulivyofika Feri tukaambiwa tushuke, naambiwa ndiyo sheria ya sasa hivi; zamani tulikuwa tunashuka tukishaingia kwenye pantoni, na mara nyingine mtu ungeweza kuuchuna ukakaa tu kwenye gari, ingawa si vizuri kwa usalama.

Kitu cha kwanza kilichonishtua hata kabla hatujafika kwenye lango la kuingia kwenye pantoni, pale kwenye soko la samaki, ni yale maji machafu yaliyojaa barabarani, na ile harufu mbaya iliyokuwa inatoka pale!! Pamoja na kwamba madirisha ya gari yalifungwa, lakini harufu mbaya ilikuwa inasikika! Mwenzangu akauliza, "hivi wale samaki tunaokula wanatokea hapa kweli"? Nami nilimjibu "haswaaa"!!

Hiyo ilikuwa tisa, kumi ni pale tulipofika kwenye kibanda cha kukata tiketi, ndo tukaambiwa tushuke abaki dereva tu kwenye gari,  hivyo mimi na mwenzangu tulishuka. Mama yangu, nilitaka kuzimia kwa ile harufu kali, mbaya sana ya choo iliyotapakaa pale!!!! Nilishangaa sana jirani kuna baa, watu wamekaa, wengine wanacheza "pool", yaani kwao ni "business as usual"!!

Tukaambiwa tukae kwenye lile banda la kusubiria pantoni; ni uchafu umezagaa kila mahali pamoja na ile harufu mbaya! Kusema kweli, nilisikia hasira sana, nilivyoangalia umati wa watu, na zile pesa zinazolipwa pale; hivi ni mamilioni mangapi kwa siku, na yanakwenda wapi na kufanya nini??

Pale nilikutana na wanakigamboni wawili, nao wakisubiri pantoni; niliwauliza "hivi kila siku mnapita na kukaa hapa na hii harufu na huu uchafu'? Wakanijibu kuwa, ndiyo kila siku wanapita hapo!!

Niliwauliza, mnachukua hatua gani sasa? Wakabaki wanajichekea tu!!
Mwishowe pantoni ilikuja tukapanda na kushuka mwisho wa safari. Pale napo hali ni mbaya sana na mambo hayaeleweki kabisa, pamoja na kwamba upande ule pia wanakusanya pesa kama kule kwingine.

Kwenye ule msafara, kulikuwapo pia watalii, wakienda kuiona Kigamboni!! Kusema kweli nilichukia sana na kushangaa kama kweli viongozi wetu hupita pale pale na kuiona ile hali!! Kama kweli wanaijua hali ile, ni dhahiri kuwa hawatutendei haki hata kidogo!!

Nawaomba kwanza waandishi wa habari watusaidie kuanika uozo huu; ni pesa nyingi sana sana inakusanywa pale kila siku; inatosha kabisa kurekebisha ile hali; ile pesa anakula nani???

Tukiweza kupata hili jibu, labda tunaweza kuanzia hapo kuona jinsi ya kuboresha Feri . Kwangu mimi ni bure kuweka majumba ya kifahari Kigamboni, na kuacha lango kuu la kuingia huko likiwa katika hali mbovu namna ile!! Unapita kwenye harufu ya choo asubuhi na jioni, halafu unaona fahari ya kuingia kenywe "bungalow" lako Kigamboni? Kwangu mimi hii si sahihi hata kidogo!! Au tunamsubiri Bush aje kuturekebishia?? LKK

0 comments:

Post a Comment