Monday 22 April 2013

[wanabidii] KILIMO KUTUMIA SHS. 328,134,608,000 KATIKA MWAKA WA FEDHA 2013 / 14

Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inatarajia kutumia jumla ya shilingi 328,134,608,000/- katika mwaka ujao wa fedha.

Takwimu hizo zimetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2013/14.

Alisema kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi 247,094,320,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na Shilingi 81,040,288,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya maendeleo.

Chiza aliongeza kuwa  Shilingi 210,175,943,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengine (OC) kwa ajili ya Wizara hiyo .

Aidha ,shilingi 25,602,969,000 ni kwa ajili ya Mishahara (PE) ya Wizara na Shilingi11,315,408,000 ni Mishahara (PE) ya Bodi na Taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Kwa upande shughuli za maendeleo, Chiza alisema kuwa Wizara hiyo imetenga kiasi cha shilingi 23,927,000,000 ikiwa ni fedha za ndani na shilingi 57,113, 288,000 ni fedha za Nje.

Wabunge wanatarajia kujadili bajeti ya Wizara ya Kilimo , Chakula na Ushirika kwa kipindi cha siku mbili ambapo itahitimishwa kesho.

Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhe. Chiza amesema Serikali inatarajia kufufua Kituo cha Kilimo Anga ili kukiwezesha kuwa na ndege na Wataalam watakaosaidia kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mazao hasa Nzige.

Mhe. Chiza amesema kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikitegemea huduma ya ndege kukodi kutoka kwenye mashirika ya kikanda ya kudhibiti nzige wekundu na nzige wa jangwani ambazo wakati mwingine hazipatikani wakati zinazohitajika.

Kufuatia hali hiyo amesema Wizara katika mwaka wa fedha 2012/13 imekamilisha viwango vya kiufundi (Technical Specifications) kwa ajili ya kutangaza zabuni ya ununuzi wa ndege moja ya kunyunyuzia viuatilifu.
---

SERIKALI ITAENDELEA KUWAENDELEZA WACHIMBAJI WADOGO WADOGO NCHINI

SERIKALI inatekeleza mkakati wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wadogo wa madini nchini kwa kuwatambua wao na mahitaji  ya mitaji na vifaa ili kutekeleza kazi yao kwa ufanisi.

Kauli hiyo imetolew na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Julius Masele wakati akijibu swali na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani leo mjini Dadoma aliyetaka kujua ni lini wachimbaji wadogo wadogo wa Ng'ombeni, Kalalami, Kigwase watatambuliwa na Serikali na kupewa kipaumbele kwenye uchimbaji, na kupewa mikopo ya kujikimu wakati wakitafuta Madini.

Amesema kuwa katika kutambua umuhimu wa wachimbaji wadogo wadogo Wizara hiyo imeshakwishatoa imetoa jumla ya viwanja 612 vya uchimbaji mdogo wa madini katika maeneo ya Ng'ombeni, Kalalani na Kigwase ikiwa ni hekta 3,864. 

Aidha, Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa na Wakala wa Jiolojia inaendelea kubainisha maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo ili yaweze kutengwa kisheria na kugawiwa kwa wachimbaji hao.

Masele alisema kuwa katika utekelezaji wa mkakati huo unashirikisha wachimbaji wenyewe kwa kuimarisha vyama vyao vya kimkoa na chama cha kitaifa (FEMATA) na kujadili masuala yao katika vikao vya pamoja vya kila baada ya miezi sita baina ya wawakilishi wao na Wizara.

Ameongeza kuwa Wizara ya Nishati na Madini inakamilisha taratibu za Mfuko rasmi wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kupata mikopo ya vifaa vya uchimbaji wenye tija.

Aidha , Naibu Waziri huyo amewasisitiza wachimbaji wadogo wadogo kuwa mikopo hiyo wanayopata inapaswa itumike vizuri katika malengo waliyoombea ili wajihakikishie kuzalisha madini mengi na kujiongezea kipato.
--

UDHIBITI WA VISUMBUFU VYA MAZAO

SERIKALI itafufua kituo cha Kilimo Anga kwa kukiwezesha kuwa na ndege na Wataalam ili kujenga uwezo wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Masoko kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mazao hasa Nzige.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza wakati akiwasilisha Bungeni Makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo leo.

Mhe. Chiza amesema kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikitegemea huduma ya ndege kutoka kwenye mashirika ya kikanda ya kudhibiti nzige wekundu na nzige wa jangwani ambazo wakati mwingine hazipatikani wakati zinazohitajika hali ambayo husababisha Wizara kutegemea kukodisha ndege kutoka sehemu nyingine.

Amesema Wizara katika mwaka wa fedha 2012/13 imekamilisha viwango vya kiufundi (Technical Specifications) kwa ajili ya kutangaza zabuni ya ununuzi wa ndege moja ya kunyunyuzia viuatilifu.

Aidha, Wizara itaweka utaratibu wa kuingia ubia na makampuni binafsi na taasisi zinazotoa huduma kama hizo ili kukijengea uwezo kituo cha Kilimo Anga.

Wakati huo huo, Wizara ya Kilimo, Ushirika na Chakula ilisambaza lita ,6000 za kiuatilifu cha kudhibiti milipuko ya viwavijeshi katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Geita. Dodoma, Morogoro na Tanga kunusuru hekta 16,418 za mazao ya nafaka.
---

SERIKALI IMEFANIKIWA KUONGEZA WATAALAM WA KILIMO NCHINI HADI KUFIKIA 7,974

Wataalam wa ugani wameongezeka kutoka 3,379 waliokuwepo mwaka 2007 hadi kufikia 7,974 mwezi Juni jana(2012) baada ya Serikali kuajiri wahitimu kutoka vyuo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akijibu swali Mhe. Mch. Dk. Getrude Rwakatare (Viti Maalum kupitia Chama cha Mapinduzi).

Amesema kuwa mwaka 2007 Serikali ilifanya tathmini ya upatikanaji wa huduma za ugani nchini na kubaini kwamba mojawapo ya vikwazo vikubwa vya upatikanaji wa huduma za ugani kwa ufanisi nchini ni upungufu mkubwa wa wataalam.

Malima ameongeza kuwa matokeo ya tathmini hiyo yalionyesha kuwa kulikuwepo na wataalam 3,379 nchini ikilinganishwa na mahitaji halisi ya wataalam 15,082.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo , Serikali ilianza kutekeleza Mpango wa kuimarisha huduma za Ugani nchini ambapo kuanzia mwaka 2007 Serikali imevifufua vyuo 13 vya kilimo nchini (MATIs) vilivyo chini ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika.

 "Ukarabati mkubwa wa vyuo vitatu MATI Ukiriguru, Maruku na Naliendele-Mtwara na ukarabati mdogo kwa baadhi ya vyuo kumi vingine umefanyika". Mhe. Malima alisema.

Aidha, Mhe. Malima amesema kuwa vyuo viwili vya mashirika yasiyo ya kiserikali vilishirikishwa katika kutoa mafunzo yaliyolenga kuongeza idadi ya wataalam wa Ugani na vyuo hivo kwa sasa vina uwezo wa kudahili wanafunzi 3,500 kwa wakati mmoja ikilinganishwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 600 uliokuwepo kabla ya mwaka 2007.
 
Habari zote za Bunge na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.

--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment