Thursday 4 April 2013

[wanabidii] CCM YAKANUSHA KUINGIA MKATABA NA MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Jana Aprili 3, 2013, mmoja wa Viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema
alitoa tuhuma dhidi ya Chama Cha Mapinduzi kuwa kupitia kampuni ya
Chama ya Jitegemee Trading Company, CCM imeingia mkataba na Mamlaka ya
Bandari nchini (TPA) kwenye mradi wa upanuzi wa Bandari kavu kwa
kutumia eneo la SUKITA lililopo maeneo ya makutano ya barabara ya
Kawawa na Mandela ambalo ni mali ya CCM.

Tuhuma hizi zimechapishwa leo na baadhi ya vyombo vya habari na hasa
TanzaniaDaima zikidai "Chadema wameibua unaoitwa ufisadi wa Mwakyembe
wa kuipa CCM zabuni ya kupanua bandari".

Kiongozi huyo wa Chadema alikwenda mbali kwa kuishutumu Wizara ya
Uchukuzi na Waziri wake Dokta Harrison Mwakyembe kwa madai ya kukiuka
taratibu na kutoa zabuni ya upanuzi wa bandari ya Dar es salaam kwa
CCM kinyume na taratibu za manunuzi jambo ambalo ni uongo.

Ukweli ni kwamba Kampuni ya Jitegemee Trading Company ni mali ya CCM,
na pia ni kweli kuwa kiwanja kilichotajwa ni mali ya CCM
kilichokombolewa kutoka zilizokuwa mali za SUKITA ambayo pia ilikuwa
kampuni ya CCM.

Lakini TPA na Jitegemee mpaka sasa hawajaingia mkataba wowote. Eneo
hilo limeombwa na wawekezaji wengi wakiwemo TPA na masharti waliyopewa
waombaji wote ni kuleta mapendekezo ya mipango yao ya kibiashara kabla
ya kufikia uamuzi wa nani anawekeza kwa ubia na Jitegemee kwenye eneo
hilo.

Wanachokiita wenzetu wa Chadema kuwa ati ni zabuni iliyotolewa kwa
kampuni ya Jitegemee na Mamlaka ya Bandari ni barua ya TPA kwenda
Jitegemee wakiomba ridhaa ya kushirikiana kuliendeleza Eneo la kampuni
hiyo ya Jitegemee lenye ukubwa wa zaidi ya ekta 100, katika mfumo wa
ushirikiano yaani "Joint Venture" kupitia utaratibu wa PPP (Public,
Private Partnership) jambo ambalo ni la kawaida sana kwani linafuata
utaratibu na sheria zote husika.

Kama nilivyokwisha kusema Chama Cha Mapinduzi kinamiliki Kampuni ya
Jitegemee, na kwamba pamoja na umiliki huo, kampuni hiyo imekuwa
ikitekeleza shughuli za uwekezaji kwa muda mrefu kwa kufuata taratibu
zote na sheria za nchi kwa ujumla.

Tunatambua kuwa Chadema kwasasa wanapitia wakati mgumu sana kisiasa
kutokana na kuanza kuvuna walichopanda kwa muda mrefu katika siasa za
nchi yetu.

Lakini pia tunatambua tabia ya viongozi wa Chama hicho ya kudandia
kila gari linalopita bila kujua linakokwenda kwa kugeuza kila
kinachofanyika nchini, ilimradi hakifanywi na wao basi ni haramu.

Hata hivyo mazingira haya wanayopitia hayawapi uhalali wa kuwa wavivu
wa kufikiri kiasi cha kushindwa kutofautisha barua ya maombi ya
kushirikiana kuendeleza eneo na mkataba!.

Aidha mazingira wanayopitia kwasasa hayawapi uhalali wa kuwa wavivu wa
kufikiri kiasi cha kushindwa kujua kuwa kinachofanyika ni mawasiliano
ya awali sana ya kusudio la kuendeleza eneo husika na hakuna taratibu
zilizokiukwa.

Umbumbumbu wa aina hii unatia mashaka sana juu ya uwezo wao wa
kufikiri na kupambanua mambo. Jambo moja wanaloonekana kulimudu ni
uwezo wao wa kutunga uongo na kupanga machafuko. Na hii ndio siri ya
watanzania kuwakataa kila kukicha na ndio siri ya kufa kwa chama
hicho, kwani njia ya muongo ni fupi.

Lakini tunazo taarifa kuwa uongo huu wamelishwa na baadhi ya mafisadi
waliotaka kutumia eneo hili la CCM kujaribu kukaa katikati ya
mwekezaji yeyote atakayejitokeza na Jitegemee kwa lengo la
kujinufaisha wao binafsi. Na huu ni mwendelezo wa Chadema kutumiwa na
mafisadi katika kutimiza mambo yao. Kutumika huku kunasukumwa na kiu
yao ya kushika dola kwa gharama yoyote. Watanzania tuwapuuze na
kuwaepuka.

CCM inachukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Uchukuzi kwa kazi nzuri
inayoendelea kuifanya chini ya Dr. Harrison Mwakyembe hasa ya kuongeza
ufanisi kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam. Tunawataka wasikatishwe
tamaa na mafisadi wachache, wachape kazi kwa uzalendo huohuo
waliouonesha.

Imetolewa na:-

Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA, ITIKADI NA UENEZI
04/04/2013

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment