Friday 12 April 2013

[wanabidii] CAG Report 2012: Wizi Mtupu Wabainika

CAG abaini ubadhirifu mkubwa
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilitolewa jana ikiweka bayana madudu mbalimbali ya ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, udhaifu katika usimamizi wa mikataba na Serikali kushindwa kutoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Moja ya matatizo yaliyojitokeza ni Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kukusanya nyongeza ya mrabaha wa madini baada ya kuongezwa kutoka asilimia tatu hadi nne.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasilisha ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2012, CAG Ludovick Utouh alisema pamoja na kuwapo mafanikio ya kimahesabu ukilinganisha na miaka iliyopita, bado kuna mambo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.


Ashauri (POAC) irudishwe au kuundwa upya
Alilishauri Bunge kuangalia upya suala la kuivunja Kamati ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC) na kuunganisha shughuli zake na Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) na mkakati wa ofisi kufanya ukaguzi wa misamaha ya kodi ambayo imeongezeka kuangalia uhalali wake

Hata hivyo, Utouh alikataa katakata kuzungumzia deni la taifa ambalo pia limeongezeka akisema "amefanya hivyo makusudi".

Bajeti na miradi ya maendeleo
Kwa mujibu wa CAG, imebainika kuwa kuna tatizo kubwa la Serikali kushindwa kutoa kwa halmashauri mbalimbali fedha za maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge. Alisema Bunge lilipitisha vifungu vya fedha za maendeleo vyenye jumla ya Sh595,064,422,505 katika halmashauri 113, lakini fedha zilizopokewa ni Sh345,568,067,477 sawa na asilimia 42 tu, hivyo kufanya upungufu wa Sh249,496,355,027.

Licha ya fedha hizo kutokutolewa zote, kiwango kilichotolewa hakikutumika chote kutokana na kucheleweshwa. "Hadi mwishoni mwa mwaka, kulikuwa na baki ya fedha za miradi ya maendeleo kiasi cha Sh188,405,740,589 ambayo ni sawa na asilimia 55 ya fedha zilizotolewa na Serikali," alisema Otouh na kuongeza: "Tunashauri bajeti iendane na shughuli zilizopangwa, kwa sasa utaratibu wa bajeti haujawa mzuri." Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hata fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinazotolewa kwa wabunge hazikutumika zote. Sh2,561,882,820 zilizotengwa kwa ajili ya sampuli ya majimbo 69 zilibaki. "Sababu ya kutokutumika ni ama halmashauri hazina utaratibu maalumu wa kutumia fedha hizo au Serikali kutoa fedha hizo mwishoni mwa mwaka," alisema.

Udhaifu katika usimamizi wa mikataba ya madini
Katika ripoti hiyo, CAG alisema Wizara ya Nishati na Madini ilishindwa kukusanya Dola za Marekani 12,634,354 (sawa na Sh19,709,593,191) zilizotokana na ongezeko la mirabaha ya madini, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini. Katika iliyokuwa Wizara ya Miundombinu, ukaguzi huo umebaini kuwa madeni yake ya mwaka 2010/11 yanayofikia Sh253 bilioni yamelipwa kwa kutumia fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara mwaka uliofuata wa 2011/12.

Katika kipindi hicho, CAG alisema dhamana za Serikali za jumla ya Sh578.4 bilioni zilikuwa zimeisha muda wake na hivyo kuifanya Serikali ikiwa mdhamini kuwajibika kulipa deni hilo.

Ashauri serikali kupanua wigo wa kodi
Vilevile, CAG ameona kuna kodi inayopotea kutoka sekta isiyo rasmi, hivyo kuishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatumia vizuri makatibu kata kuwatambua walipakodi kama vile wamiliki wa kumbi za harusi na mikutano.

Alishauri kuwa TRA ianze kukusanya kodi kwenye huduma za kuhamisha fedha kwa njia ya simu za kiganjani maarufu kama M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money na nyinginezo.

Alisema kampuni hizo zinatakiwa kulipa kodi ya zuio ya malipo ya kamisheni inayolipwa kwa wanaofanya biashara hiyo na kodi hiyo ipunguzwe kutoka katika kodi ya mwisho itakayotakiwa kulipwa na kampuni za simu.

Misamaha ya kodi
Ripoti hiyo ya CAG ilishauri mikataba ya madini ijadiliwe na Kamati ya Bunge inayohusika na kutoa mapendekezo kabla haijasainiwa na hati za misamaha ya kodi ziwekwe bayana kuwa ni msamaha wa muda gani, inaanza na kumalizika lini. Alishauri pia vipengele vyote vya misamaha ya kodi vipitiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kushauri kabla ya kusainiwa na upande husika.

Katika mwaka 2013/14, CAG ameamua kuanza kuikagua misamaha yote ya kodi kwa madhumuni ya kuangalia manufaa yake kwa uchumi wa taifa, kwa kuwa misamaha hiyo pia ni fedha za Serikali. Hesabu za TRA zimeonyesha makusanyo ya kiasi cha Sh6,703,229,704,887 ikilinganishwa na makadirio ya Sh6,456,832,630,000 na kusababisha makusanyo ya ziada ya Sh 246,397,074,887 sawa na asilimia nne ya makadirio.

Taarifa ya CAG inaonyesha mwelekeo wa misamaha ya kodi unaonyesha ongezeko kwa kiasi cha Sh789,883,259,827 sawa na asilimia 78 kutoka kiasi cha Sh1,016,320,300,000 kilichoripotiwa mwaka 2010/2011 hadi Sh1,806,203,559,827 kwa mwaka 2011/2012.

Kuvunjwa kwa POAC
Utouh alisema kitendo cha kuvunjwa kwa POAC na kuunganisha majukumu yake na PAC ni bahati mbaya kwa kuwa sababu za kuanzishwa kwake bado zipo hai kama ilivyokuwa wakati inaanzishwa na kwamba uamuzi huo hautakidhi matarajio ya wadau.

"Kamati ya PAC itazidiwa na ukubwa wa majukumu, hivyo ofisi bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya kubadilisha jina lake," alisema.

Maamuzi ya Apika Makinda bila ushirikishwaji wahusika kuvunja kamati hizo
Spika Anne Makinda aliamua kuvunja kamati zote za Bunge kwa kuunda mpya na kuvunja nyingine. POAC iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe iliunganishwa na ile ya PAC, ambayo pia inaongozwa na mbunge huyo. "Kamati ya PAC itazidiwa na ukubwa wa majukumu, hivyo ofisi bado inashauri kuona uwezekano wa kurudisha kamati hii hata kama itakuwa na haja ya kubadilisha jina lake,"
 
QuoteBy Candid Scope View Post
CAG aibua madudu mapya

WIZARA ya Nishati na Madini imekumbwa na kashfa mpya ya kushindwa kukusanya kiasi cha dola 12,634,354, sawa na sh bilioni 19.7 kama sehemu ya mirabaha kutoka kwenye kampuni zinazochimba madini nchini.

Mbali na kushindwa kukusanya kiasi hicho cha mirabaha, pia imeshindwa kukusanya kiasi cha sh 1,645,582,899 kutoka vyanzo mbalimbali kama vile vitalu vya madini na leseni za umeme.

Hayo yamebainika katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2012, iliyowasilishwa bungeni jana.


Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Utouh alisema kuwa maduhuli yaliyoshindwa kukusanywa na wizara hiyo yalitokana na mabadiliko ya sheria ya madini iliyorekebisha kiwango cha mrabaha kutoka asilimia 3 hadi 4.

Mbali ya Nishati na Madini, wizara nyingine iliyokumbwa na madudu ni ya Ujenzi, ambayo kwa mujibu wa ripoti ya CAG, iliamua kutumia sh milioni 252.9 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya ujenzi wa barabara na badala yake ililipia madeni yanayowakabili.


Upungufu mwingine uliobainishwa katika ripoti hiyo ni pamoja na kuongezeka kwa fedha za misamaha ya kodi, ambapo katika kipindi hicho, serikali ilitoa misamaha ya kodi ya sh trilioni 1.9 kutoka trilioni moja, sawa na ongezeko la asilimia 27 kutoka 18. Alisema kuanzia mwaka ujao wa fedha, ofisi yake itakagua misamaha yote ya kodi inayotolewa na serikali na kuwatangaza hadharani makampuni, mashirika, wafanyabiashara na watu binafsi wanaopata misamaha ya kodi.


Akizungumzia upungufu uliojitokeza kwenye ukaguzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Utouh alisema kwamba kumekuwa na udhaifu mkubwa katika kusimamia mapato ya ndani. Alitaja upungufu huo kuwa ni vitabu 2,990 vya stakabadhi za mapato kutoka halmashauri 36 kutokutolewa kwa ajili ya ukaguzi wakati halmashauri 56 zilikuwa na jumla ya sh bilioni 4.4, ikiwa ni mapato yaliyokusanywa na mawakala ambao hawajawasilisha kwenye halmashauri hizo. "Halmashauri 17 hazikukusanya kodi ya majengo kiasi cha sh bilioni 4.3, sawa na asilimia 38," alisema.


Kama ilivyokuwa katika taarifa yake ya mwaka jana, ukaguzi wa mwaka huu pia umebaini kuwapo kwa watumishi 17,710 ambao wamekuwa wakipokea mishahara pungufu, 1/3 ya mishahara yao, kinyume cha sheria kutokana na watumishi hao kuelemewa na mikopo. Pia ripoti hiyo imeendelea kubaini kuwa kuna watumishi hewa, wakiwamo waliostaafu na waliofariki dunia, wameendelea kulipwa mishahara ya sh milioni 82.3.


Akizungumzia Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali Kuu, CAG alisema mfuko huo una hali mbaya, kwani hadi sasa una hasara ya sh trilioni 6.4, hivyo kuwa kwenye hatari ya kufa. Hata hivyo alisema pamoja na mfuko huo kuwa na hali mbaya kifedha, amebaini kuwa ulitoa mikopo ya sh bilioni 67 kwa taasisi za umma na nyingine bila riba na mikopo hiyo ilidhaminiwa na serikali. Alizitaja taasisi zinazodaiwa na kiasi cha fedha kwenye mabano kuwa ni pamoja na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) sh bilioni 54.6, PCCB (sh bilioni 6.6), Tan Power Resources (sh bilioni 5.4) na Kiwanda cha Madawa Tanzania (sh milioni 485).


Hata hivyo alisema matokeo ya ripoti ya mwaka huu, yameonesha kuboreka kwa hati zilizotolewa kwa Serikali Kuu na taasisi zake ikilinganishwa na miaka iliyopita. Alisema hati za kuridhisha zimeongezeka kutoka 69 mwaka 2011/2011 hadi 108 wakati hati zenye shaka zimepungua kutoka 12 hadi sita mwaka 2011/2012 na hapakuwa na hati isiyoridhisha wala hati mbaya kama ilivyokuwa mwaka 2010/2011.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (POAC), Zitto Kabwe, alisema pamoja na mabadilko machache, bado ripoti hiyo ni mbaya, kwani bado kuna matatizo makubwa ya usimamizi wa fedha za serikali. Alishangaa Wizara ya Nishati na Madini kushindwa kukusanya mirabaha kutoka makampuni ya madini na kusisitiza kwamba kuna kazi kubwa ya kuibana serikali katika kusimamia matumizi ya fedha za umma

Wakuu

Tafadhali mwenye hii report in full anitupie hapa




0 comments:

Post a Comment