Sunday 14 April 2013

Re: [wanabidii] Sokoine

Joseph,
Umenikumbusha mbali lakini hiyo mheshimiwa meneja wa baa nayo kali sana.





Walewale.



From: Joseph Beda Rupia <rupia.joseph@gmail.com>
To: wanabidii@googlegroups.com
Sent: Sunday, April 14, 2013 2:16 PM
Subject: [wanabidii] Sokoine

RAI, April 11, 2013
Komredi Sokoine Dodoma bado ni mkoani tu
Na Joe Beda
'NDUGU wananchi, leo saa saba mchana; ndugu yetu na kijana wetu. Ndugu Edward Moringe Sokoine; alipokuwa safarini kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake ilipata ajali. Amefariki dunia.'
Unaweza kuamini kuwa hii nayo ni hotuba? Hakika ni hotoba, na huenda hii ndiyo hotuba fupi kuliko zote nilizowahi kuzisikia maishani.
Ni hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyoitoa jioni ya Alhamisi Aprili 12, 1984 na kurushwa na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kusikika kila kona ya nchi, kisha kuleta vilio kwa Watanzania.
Pamoja na ufupi wake, bado ujumbe uliokusudiwa uliwafikia walengwa bila kukosea. Ni kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Moringe Sokoine.
Sokoine, Mmaasai anayeaminika kuwa mchapa kazi na mzalendo pengine kuliko mawaziri wengi wa sasa na wa zamani, alifariki dunia kwa ajali ya gari akiwa safarini (kikazi) kutoka Dodoma.
Alipofika maeneo ya Dakawa, Morogoro, gari alilokuwa akisafiria liligongana na Toyota Land Cruiser iliyokuwa ikiendeshwa na 'mpigania uhuru' wa Afrika Kusini, Dumisan Dube.
Yalisemwa mengi wakati na baada ya maziko yake, huku kama kawaida viongozi wakiahidi kuyaenzi yale aliyokuwa ameyaanzisha au kuyafanya. Lakini ni kweli yalienziwa? Hata kidogo! Asiye kuwapo na lake halipo.
Mwanzoni mwa vuguvugu la vyama vingi, aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Mabere Marando, aliwahi kumzungumzia Sokoine akisema ndiye kiongozi mzalendo zaidi kuwahi kutokea nchini.
Marando alisema aliwahi kuwamo kwenye msafara wa Sokoine huko Kibaha. Baada ya shughuli za siku nzima, ilipofika saa tisa alasiri uongozi wa Kibaha ukamkaribisha Sokoine na msafara wake kwenye chakula kilichoandaliwa katika moja ya shule za msingi.
Kama kawaida kiongozi akitembelea sehemu, mapochopocho kibao yaliandaliwa. Kabla watu hawajaanza kujichana, Sokoine akauliza: "Hivi hawa watoto (wanafunzi) waliopo hapo nje wamenisubiri tangu saa ngapi?" Akajibiwa kuwa tangu asubuhi ya siku hiyo.
Akauliza: "Wameshakula?" Hakupata jibu.
Akasema: "Mimi ninarejea Dar es Salaam na hivyo kila mtu akale kwake. Hiki chakula wapeni hawa watoto wakile."
Duh! Ilikuwa bonge la sherehe kwa watoto wakati Waziri Mkuu akiamrisha msafara uondoke. Aliyenuna akanuna, aliyecheka akacheka!
Huyo ndiye Sokoine, Waziri Mkuu aliyekuwa akiwafikiria wengine zaidi. Waziri gani leo hii anaweza kuwaza watoto kama wamekula au hawajala? Yaani aache kufikiria posho na marupurupu mengine! Sidhani.
Hata kifo chake kilitokea baada ya kukataa kupanda ndege kurejea Dar es Salaam, akaamua kupanda gari ili njiani akague miradi kadhaa ya maendeleo.
Ninakumbuka nilimwona kwa mara ya kwanza siku alipofika Sumbawanga, bila shaka ilikuwa mwaka 1978. Baada ya mapokezi, akihutubia wananchi alishangaa na kusema: "Hivi Sumbawanga ni mji kweli? Hapana, labda tuuite 'mji-kijiji'."
Acha Wafipa wakasirike! Lakini ule ndiyo uliokuwa ukweli wenyewe na kauli hiyo ilikuwa changamoto, kwani watu walifanya kazi kweli kweli hadi leo hii Sumbawanga ni mji mkubwa.
Wengi wanajiuliza, ingekuwa vipi Sokoine angeendelea kuishi? Tanzania ingekuwa wapi leo? Ile ndoto ya kuifanya Dodoma makao makuu ingetimia?
Kwa kasi ya utendaji wake, lazima ndoto hiyo ingetimia. Mbona Malawi waliamua kuhamia Lilongwe kutoka Blantyre na Nigeria wakatoka Lagos kwenda Abuja kwa kasi ya ajabu - kwanini sisi tumeshindwa?
Mheshimiwa Sokoine… aaah! Samahani. Ndugu Sokoine, Dodoma hadi leo ni mkoa kama Lindi au Singida. Haujawa makao makuu wala hakuna dalili ya kuwa makao makuu kwa miaka 50 ijayo.
Ndiyo. Sokoine si Mheshimiwa, waheshimiwa ni hawa wa hivi sasa. Yeye na Nyerere walipenda kuitwa 'ndugu' wakiamini kabisa kuwa kama kuna 'mheshimiwa' basi lazima atakuwapo 'mdharauliwa'.
Kasumba ya uheshimiwa iliyoanzia Dodoma miaka ya 1990, imeambukiza Watanzania wengi sana. Utasikia mheshimiwa diwani, mheshimiwa mwenyekiti, mheshimiwa mwenyekiti wa mtaa, mheshimiwa meneja wa baa, mheshimiwa baamedi! Na siku si nyingi tutakuwapo waheshimiwa waandishi wa habari na baadaye waheshimiwa mahausigeli.
Sokoine, rejea uione Tanzania yetu iliyojaa waheshimiwa ingawa hawana lolote wanalolifanya zaidi ya kuitafuna nchi hii bila aibu. Sokoine njoo utukumbushe pilikapilika za uhujumu uchumi na nguvu kazi.
0684 419 506
mwisho
 
--
Send Emails to wanabidii@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 


0 comments:

Post a Comment