Monday 11 March 2013

[wanabidii] Taarifa ya Simba SC kuhusu Wachezaji kuzuiwa hotelini; Benchi la ufundi kufukuzwa

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SALAAM,
JANA na leo, zimetolewa habari tofauti kuhusiana na kalbu ya Simba
ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka
rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa taarifa hizo.

1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI

SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal Union ya
Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa
Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile anaidai Sh
milioni 25 na anataka alipwe zote jana.

Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda mrefu
sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Simba walifanya mkutano na wachezaji wote wa Simba katika hoteli hiyo
usiku wa kuamkia jana.

Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi wakati
huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya
mechi na walisubiri mpaka wakati timu inataka kuondoka ndiyo
wakachukua hatua hiyo.

Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno. Ifahamike
kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki
huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi 10
iliyopita.

Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire walilipwa Sh
milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu yetu ina utaratibu
wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki
wa Saphire inavyotaka kueleza.

Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa
baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati
wowote mwezi huu au ujao. Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa
wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na
inataraji kulipwa fedha hizo.

Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa kulipa madeni
yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado ikabaki na
fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.

Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa
madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa
chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za
udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.

Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza
mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili
kuongeza mapato yake. Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu wa
Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba
nayo ifaidike.

Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si
dhambi. Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani kama vile Manchenster
United, Real Madrid na Liverpool zina madeni, inakuaje madeni ya
Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza kuyalipa yote iwapo
wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu kigeni?

Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri
utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit worthiness ya mteja
inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba inapenda kusisitiza
kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa na bado inavutia
watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuchukua hatua za kisheria
dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha
kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya
jana.

Simba inachukulia kitendo kile kama hujuma na kisheria kinaangukia
katika kundi la Forced Imprisonment, kwa mmiliki kuwazuia watu
kinguvu. WAMILIKI hawakutoa notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya
mdomo au maandishi kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Lengo lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo
imetoka kulipwa Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita. Uongozi wa
Simba SC unaapa kuilinda na kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu
zetu zote, akili zetu zote na maarifa yetu yote.

2. WACHEZAJI, BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA

KUNA taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba
wamesimamishwa au kufukuzwa kuchezea Simba. Habari hizi nazo hazina
ukweli wowote.

Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba umetoa ruksa kwa benchi la ufundi
kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi husika. Uongozi
hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji wa benchi la
ufundi.

Hakuna mchezaji yeyote aliyesimamishwa hadi sasa. Pia uongozi
unakanusha taarifa kuwa Daktari Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga,
kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina ukweli kwani daktari huyo
ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili inayojulikana.

HITIMISHO

KATIKA namna ya kipekee kabisa, uongozi wa Simba unapenda kutoa
shukrani za dhati kabisa kwa washabiki wake waliojitokeza Uwanja wa
Taifa na kuisapoti timu kwa asilimia 100. Uongozi unathamini sana
mchango wa wanachama wake na unaahidi kufanya kila unachoweza
kuwarejeshea tena furaha mioyoni mwao.

Uongozi pia unatumia nafasi hii kuwapongeza wachezaji na benchi la
ufundi ambao walicheza mechi ya jana katika mazingira magumu.
Walicheza bila ya kufanya warm up na wakitoka kuwa wamezuiwa hotelini
jambo ambalo lingeweza kuwaondoa mchezoni.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
SIMBA SC

Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2NGDkyfMb

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment