Wednesday, 13 March 2013

[wanabidii] Siri ya kipigo cha Kibanda yafichuka

WADAU WA HABARI WAUNDA TUME KUCHUNGUZA

na Hellen Ngoromera

 

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006, Hussein Bashe, amefichua siri za njama za kuvamiwa na kupigwa kwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Absalom Kibanda.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa habari kilichoongozwa na Chama cha Wamiliki wa vyombo vya habari nchini (MOAT), Bashe alisema wiki tatu kabla ya tukio la kuvamiwa Kibanda, alishuhudia gari la polisi likiwa limebaki nje ya ofisi yao majira ya saa 5 usiku na walipotoka liliwafuatilia.

"Kabla ya tukio hilo kumkuta Kibanda wiki tatu kabla, tulitoka ofisini saa 5:00 usiku na kwa muda mrefu nje ya ofisi lilipaki gari la polisi aina ya gofu lililokuwa na namba za usajili PT 180.

Alisema kwa kuwa yeye na Kibanda wanaishi Mbezi, walipotoka walifuatana lakini cha ajabu gari hilo lililokuwa limepaki nje ya ofisi yao na kuelekea upande wa Shekilango, liligeuza na kuwafuata.

"Gari lile liligeuza likatufuata nyuma mpaka eneo la makaburini, mbele ya Mwika Baa, likazuia gari yangu na baadaye kupaki nyuma ya gari yangu.

"Hawakushuka lakini baada ya dakika tatu, nne hivi akashuka askari mmoja nikawasha taa za gari ndani kwa sababu nilikuwa na mwenzangu nikamuuliza unataka nini? Akasema tunalitilia shaka gari lako, nikamwambia nimewaona ofisini na sasa mnatufuata, mnataka nini? Lile tukio tuliripoti polisi," alisema Bashe.

Alisema wakati hayo yanatendeka, Kibanda alikuwa ameegesha gari lake upande wa kulia wa barabara na kwa kuwa naye aliona tukio zima, alimpigia simu na kumpa tahadhari ya kutoshuka kwenye gari.

Alisema pamoja na mambo mengine alimjulisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuhusu tukio hilo ambaye aliahidi kulifuatilia.

Kwa mujibu wa Bashe, yapo matukio ya namna hiyo, na kwamba kuna wanasiasa walishawahi kutangaza hadharani kwamba wana maadui hapa nchini, wakiwamo waandishi wa habari, lakini cha kushangaza hakuna juhudi zozote zilizofanywa na vyombo husika kuwataka wanasiasa hao kuwataja maadui hao.

Alisema mambo hayo na mengine yanawafanya waamini kwamba kuna matabaka ya watu ambao wanaweza kuamua kufanya jambo lolote bila kuguswa.

"Ni wakati sasa serikali ikafanya uchunguzi wa kina na kuja na majibu sahihi, wamefanya kazi nzuri, wameona wamefukuza mapolisi walioharibu ushahidi wa dawa za kulevya kuwa sukari, kwa hiyo watupe majibu sahihi kwamba wanaofanya haya matukio ni kina nani?

"Ndo maana tunasema kuna watu wanatumia watu ndani ya mifumo ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanikisha mambo yao, inaweza kuwa kisiasa, kiuchumi au vinginevyo," alisema Bashe.

Wadau wengine waliokuwepo kwenye mkutano huo mbali ya MOAT ni Misa- Tan, TMF, TAMWA, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri (TEF).

Tamko la wadau wa habari

Katika tamko lao lenye maazimio matano, wadau hao wamekubaliana kuunda kamati ya watu 16 ili kukutana na wakuu wa vyombo vya usalama nchini akiwemo Waziri Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na naibu wake, Jack Nzoka pamoja na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah.

Wadau hao walioongozwa na Mwenyekiti wa MOAT, Reginald Mengi, wamekubaliana kukutana na wakuu hao ili kuzungumzia kwa undani usalama wa makundi yanayolengwa na vitendo vya kushambuliwa, kuumizwa na hata kuuawa.

Kamati hiyo itaongozwa na Mengi na Katibu wake, Henry Muhanika. Wengine ni Bashe, Tido Mhando (Mwananchi Communications Ltd), Aga Mbuguni (Business Times Ltd), Abdallah Mrisho (Global Publishers) na Ansbert Ngurumo (Free Media Ltd).

Wamo pia Jesse Kwayu (The Guardian Ltd), Mikidard Mahmood (The Guardian Ltd), Godfrida Jola (Tamwa), Japhet Sanga (TMF), Neville Meena (TEF), Pili Mtambalike (MCT), Tumaini Mwailenge (Misa -Tan), Deodatus Balile (Jamhuri) na Samson Kamalamo (Changamoto).

Kwa mujibu wa wadau hao, wanaamini kwamba kuvamiwa na kuteswa kwa Kibanda kumetokana na msimamo imara wa kalamu yake na si kitu kingine.

Mengi alisisitiza kwamba suala hilo la kukutana na viongozi hao halitakuwa la wiki moja au tatu, bali ni la haraka na wanaamini watakapowafikishia ujumbe huo watalichukulia kwa uzito unaostahili.

Alisisitiza kwa kuwataka Watanzania kutoishi kwa woga kwani mlinzi mkuu wa yote ni Mwenyezi Mungu, hivyo ni vema wakaomba na kusali ili kuyaepusha.

Azimio jingine ni kwamba tukio la Kibanda ni mfululizo wa mashambulizi ya namna hiyo na kwamba katika mazingira hayo wamejiona na kutambua kuwa hakuna aliye salama.

"Kwamba shambulio lililofanywa dhidi ya Kibanda halikutokana na kitu kingine chochote zaidi ya kazi yake ya uandishi wa habari. Kutokana na hali hiyo, wadau wa habari wamelichukulia suala hilo kuwa ni shambulizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini na kuwajengea hofu wahariri, waandishi na wanaharakati wote ili wasitekeleze wajibu wao kwa umma," lilisema tamko hilo.

Walirejea matukio yaliyopita wakisema lilianza kwa waandishi wa habari wa gazeti la Mwanahalisi, Sued Kubenea na Ndimara Tegambwagwe, kutekwa kwa Dk. Steven Ulimboka, kuuawa kwa Daudi Mwangosi wa kituo cha Channel 10, na sasa mashambulizi dhidi ya Kibanda, hivyo hayo ni baadhi ya matukio yanayoonesha hali ya kuzidi kuzorota kwa mazingira ya utendaji kazi wa wanahabari na wanaharakati.

Wametoa azimio jingine wakieleza kusikitishwa na hatua ya baadhi ya maofisa na watumishi wa vyombo vya usalama, kutumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu ambavyo vinatishia usalama wa waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.

Alitolea mfano wa usumbufu alioupata mwandishi, Eric Kabendera na familia yake ambapo wazazi wake walihojiwa na waliojiita watumishi wa Idara ya Uhamiaji, uliofanywa kwa shinikizo na watu wanaotumia watumishi wa umma kutekeleza matakwa yao ya kuleta hali ya kuzorota kwa usalama wa waandishi wa habari.

Wametaka serikali kuunda tume huru ya wapelelezi kuchunguza undani wa masuala haya kwa kuwa kasi ya uchunguzi wa vyombo vya usalama hapa nchini hairidhishi, pia baadhi ya watendaji ndani ya vyombo hivyo wanahusishwa na kadhia hizi.

Hivi sasa Kibanda amelazwa katika Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini ambako amefanyiwa upasuaji wa jicho na baada ya siku 45, atafanyiwa upasuaji mwingine wa jicho na kuwekewa la bandia.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment