Wednesday 13 March 2013

[wanabidii] Sera mpya ya elimu Zanzibar na kisa cha wapepea ‘mwiku’

Na Maalim Kisisyina,

Labda nianze kwa kufasili neno 'mwiku' kwani wasomaji wangu wengi yawezekana hawalifahamu neno hili. Kwa wenyeji wa kisiwa cha Pemba neno 'mwiku' maana yake ni chakula kilichobakia baada ya kuliwa jioni kikaachwa ili kiliwe asubuhi.

Kwa Kiswahili Sanifu 'Mwiku' huitwa Uporo. Na mpaka hapa naamini nishawatoa tongo wale wasomaji wangu wenye kuchukua sekunde zao nne hadi tano kusoma makala zangu.

Naamini muda si mrefu tumeona mabadiliko makubwa ya sera ya Elimu. Mabadiliko hayo ambayo kwa kaisi kikubwa yameandikwa kumshawishi kila mtu aamini kwamba sasa nusura ya vijana wetu ya kufeli na mapanga ya NECTA imefika.

Kwa maana hio taswira inayojengwa hapa ni kuwa sera yetu ya Elimu imekuja kuongeza ufanisi na kiwango cha Elimu sambamba na kurekebisha mapungufu kadhaa yaliyokuwemo kwenye sera ya mwanzo.

Bila shaka sera ya Elimu ni muhimu sana kwa maendeleo ya kila nchi. Lakini kwa vile tumetoka msibani hivi juzi na hata matanga hatujachawanyika baada ya vijana wetu wa kidato cha nne kufeli kwa kupigiwa pembe na zumari, tena wamefeli siku chache tu baada ya kutawanyika arubaini ya msiba wa wenetu walioghariki katika jahazi la mitihani ya kidato cha pili pia mwaka huu huu. Kwa hali hii napata shaka.

Yawezekana kwamba uamuzi huu wa kuibuka mbio mbio na kutafutwa mtu anaejuwa kuandika kizungu japo chenye machulechule aje atuandikie sera mpya ya Elimu, ni moja kati ya mbinu ya serikali kujifariji na kuwapiga ghubari ya macho wananchi waamini sasa imejipanga kijeshi kukabiliana na majanga ya kufeli mitihani. Kama kuna mtu mwenye fikira kama hizi basi ajiunge na wale wanaopepea uporo. Hakuna jipya na gharika iko pale pale.

Nasema gharika iko pale pale kwa sababu Serikali inakimbilia kutatua tatizo bila kulijua tatizo hasa ni nini? Ukweli ni kwamba tatizo la kufa kwa Elimu hapa kwetu halitokani pekee na sera ya Elimu, la hasha. Suali la kufeli linachangiwa na mambo farike ya Sera na ndio nikasema Serikali haijatibu tatizo kwa kuleta sera mpya ya Elimu.

Kwa kila mtu aliepitia shule na kwa wale waliobahatika kushika chaki, wanajua kwamba mambo lukuki yanachangia kushuka kwa kiwango cha Elimu hapa kwetu. Kubwa ni kukosa usimamizi mzuri wa Serikali katika sekta ya Elimu. Serikali zetu za siku hizi zimelipiga mgongo sana suala la Elimu. Leo hii shule zinajitegemea kwa chaki na kila kitu. Kwa pesa ni miradi ipi?

Kuna tatizo la walimu mashuleni. Tulishasema kuwa Zanzibar inakosa walimu wengi wenye sifa kwa sababu mbalimbali zikiwemo za usiasa na mapuuza ya kudharau wataalamu. Pia tumesema kuwa walimu wetu wengi tulionao hawana viwango vya kutufikisha hatua nyengine ya Elimu, na hakuna anaesikia kwa hili.

Tukasema sana kuwa walimu wamepoteza ari ya kufundisha kwani hawana msaada wowote, maisha magumu na malipo duni, na kwa maana hio hawasomeshi kwa roho safi wala utulivu. Nani kasikia.

Tumesema sana hapa kuwa wenzetu wa NECTA hawatutakii mema, wana ajenda ya siri dhidi yetu lakini wapi? Tunaogopa kumuudhi bwana mchinja mbuzi, tusijekukosa mchuzi. Tunao NECTA, watoto wetu wanafelishwa maksudi na sisi kimya, mpaka atoke bwana bara aje atwambie, tuunde tume tuchunguze matokeo ya mtihani.

Lakini cha ajabu, tume hiyo inaundwa wanaokula pesa na kufaidika ni wao, sisi huku watoto wetu hawajui hatma yao na wala hakuna anaesema kuwa Serikali itawasaidia vipi vijana wetu hawa, na itafanya vipi kuondoa mushkeli mkubwa wa uadilifu uliopotea kule NECTA. Hili sisi Zanzibar hatulioni.

Tumefika pahala tunatunga vitabu vya Kiingereza na kufundishia shuleni hapa nyumbani bila kuangalia viwango vya utunzi huo na uwezo wa wanaotunga. Tulipoona hapo hapakutosha, tukaacha Kiswahili Unguja na kwenda kuwatafuta Wakurya na wamakonde watuandikie vitabu vya Kiswahili.Tusimtafute jinni anewamaliza watoto wetu hapa!

Sasa haya yote na umayamaya wa utendaji duni zaidi ya huu, mwisho tunakuja tunatafuta kisa cha kupeana ulaji kwa kujifungia ndani kuandika sera ya Elimu upya iwe ndio suluhisho la matatizo yetu. Kama huku sio kupepea Uporo ni kitu gani? Nijuavyo mimi uchomeako ndiko utokako mwiba, na kwa hivi tuendavyo basi nusura haipo. Tuendelee kupepea mwiku!

Nawasilisha.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment