Sunday 24 March 2013

[wanabidii] MAONI YA PROF HARUNA LIPUMBA KUHUSU UJIO WA RAIS WA CHINA NCHINI

Tarehe 24 Machi 2013, Rais Xi Jiping wa China atazuru nchi yetu.
Tanzania itakuwa nchi ya pili baada ya Urusi kwa Rais Xi kutembelea
tangu achaguliwe rasmi na Bunge la Jamhuri ya Watu wa China kuwa Rais
wa nchi hiyo tarehe 14 Machi 2013. Kuteuliwa kwake kuwa Rais wa China
kunafuatia uteuzi wake wa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti
cha Jamhuri ya watu wa China na kuwa Mwenyekiti wa Tume Kuu ya Majeshi
ya China (na kwa hiyo kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Ukombozi la
China) Novemba 2012 katika mkutano mkuu wa 18 wa chama hicho.

Utaratibu wa kuwa na uongozi wa juu wa Chama na Serikali wa muda wa
miaka 10 na viongozi wasizidi umri wa miaka 70 uliasisiwa na Deng
aliyeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini China kuanzia mwaka
1978. Uhusiano wa China na Tanzania ni wa muda mrefu. China waliunga
mkono mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12 1964. Mwalimu Nyerere
alitembelea China mwaka 1965 na alivutiwa sana na sera za Ujamaa za
Mwenyekiti Mao. Katika uhai wake kabla na baada ya kun'gatuka wadhifa
wa Urais, Mwalimu alitembelea China mara 13.

Katika nyanja za uhusiano wa kimataifa Dr. Salim Ahmed Salim aliyekuwa
balozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York alisimamia kidete
kukubaliwa kwa China kujiunga katika Umoja wa Mataifa na kuchukua kiti
kilichokuwa kinakaliwa na Taiwan tarehe 25 Novemba 1971. Sherehe
aliyofanya Balozi Salim katika ukumbi wa Umoja Mataifa tarehe 25
Oktoba 1971, wakati Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lilipopitisha
azimio la kuifukuza Taiwan na kuikaribisha China, ulimuudhi sana
George W. H. Bush ambaye alikuwa balozi wa Marekani wa wakati huo na
hatimaye akawa Rais wa Marekani 1988 – 92.

Ushirikiano na China katika miaka ya 1960 na 1970 ulifanikisha miradi
kama vile Kiwanda cha nguo cha Urafiki, kiwanda cha zana za kilimo cha
Ubungo na mradi mkubwa wa reli ya TAZARA. Kwa sababu ya udhaifu wa
kiutendaji miradi hii imekuwa siyo endelevu. Kiwanda cha zana za
kilimo kimekufa. Hata baada ya kubinafsishwa kiwanda cha
Urafiki kinasuasua. Reli ya Tazara haifanyi kazi kwa kiwango chake.
Mwaka 2002 ilisafirisha mizigo yenye uzito wa tani elfu 677 lakini
mwaka 2011 kiwango hicho kilipungua na kufikia tani elfu 248.

Katika Mkutano wa Tano wa Mawaziri kuhusu ushirikiano wa China na
Afrika uliofanyika Beijing Julai 18-20 2012, Rais Hu Jintao wa China
aliahidi nchi za Kiafrika mikopo ya riba nafuu ya dola bilioni 20
katika kipindi cha miaka 3 ijayo.Hili ni ongezeko la mara mbili ya
msaada uliotolewa wa dola bilioni 10 katika mkutano kama huu mwaka
2009.

Mikopo itakayotolewa na China itasaidia ujenzi wa barabara, reli na
miundombinu mingine, kilimo, viwanda na shughuli za uzalishaji na
biashara ndogo na kati. Katika miaka 12 iliyopita biashara kati ya
China na Afrika imeongezeka kwa kasi kubwa. Mwaka 2011 thamani ya
biashara yote kati ya China na Afrika ilikuwa dola bilioni 166.

Afrika iliuza China bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 93. Bidhaa
hizo zilikuwa malighafi hasa mafuta ghafi ya petroli, madini megine
kama vile shaba na chuma. Afrika iliagiza toka China bidhaa zenye
thamani ya dola bilioni 73 nyingi kati ya hizo zikiwa ni bidhaa za
viwandani. Katika nchi nyingi za kiafrika kuna manun'guniko makubwa
kuwa bidhaa kutoka China zinaua viwanda vya Afrika. Makampuni ya China
yanawekeza katika nchi za kiafrika hasa katika sekta ya madini na
yanashiriki katika ujenzi wa miundombinu hasa barabara.

Wafanya biashara ndogo ndogo toka China wamejitokeza katika nchi
nyingi na kuzua mjadala kuwa wanachukua fursa zinazopaswa kuachiwa
Waafrika wenyewe. Baada ya kifo cha Mwenyekiti Mao mwaka 1976, Deng
Xiaoping alishika uongozi wa China 1978 na kuanza kubadilisha sera za
Mao hatua kwa hatua. Kwanza alianza kwa kuachana na mashamba ya ujamaa
na badala yake akawapa fursa familia za wakulima kulima mashamba kwa
mkataba wa kuuza sehemu ya mazao yao kwenye vyombo vya dola kwa bei
zilizopangwa na ziada kuuza kwenye soko huria ambako bei ilikua juu.

Wakulima wakawa na shauku ya kupata ziada kubwa ya mazao ili kuyauza
kwenye soko huria na kuongeza kipato chao. Mabadiliko ya sera kutoka
mashamba ya ujamaa na kwenda kwenye mashamba yanayomilikiwa na familia
yaliongeza kasi ya ukuaji wa pato la sekta ya kilimo na kusaidia
kupunguza umaskini.

Wakati China imeanza mabadiliko ya sera za uchumi mwaka 1978, pato la
wastani la Mchina lilikuwa dola za Marekani 190 chini ya wastani wa
pato la taifa la Mtanzania. Mabadiliko ya uchumi yamefanikisha ukuaji
wa pato la taifa kwa kasi ya juu ya wastani wa asilimia 10 kwa mwaka
kwa muda wa miaka 34. Katika historia ya dunia hakuna nchi
iliyofanikiwa kukuza uchumi kwa muda mrefu na kwa kasi ya juu kama
China ilivyofanya. Katika kipindi hiki biashara na nchi za nje ilikua
kwa kasi ya wastani wa asilimia 16.3 kwa mwaka.

China yenye watu bilioni 1.34 hivi sasa ina wastani wa pato la taifa
la dola 4930 wakati Tanzania ina wastani wa pato la taifa la dola 530.
Ukuaji wa uchumi umepunguza umaskini wa kipato. Inakadiriwa Wachina
zaidi ya milioni 600 wameondokana na umaskini wa kipato katika kipidi
cha miaka 30. Mwaka 1979 asilimia 86 ya wananchi wa China walikuwa
maskini wakiishi kwa kutumia chini ya dola 1 kwa siku. Kwa sababu ya
ukuaji wa kilimo, asilimia ya watu maskini ilipungua na kufikia 54
mwaka 1987 na asilimia 36 mwaka 1996.

Ukuaji wa uchumi kwa wastan wa asilimia 10 kila mwaka kwa muda wa
miaka 30 umepunguza sana umaskini na kufikia asilimia 13 mwaka 2008
kwa kutumia kigezo cha kimataifa cha mtu mzima kutumia dola 1 kwa
siku. Maendeleo ya viwanda yaliongezeka kwa kasi kwa serikali kuruhusu
uongozi wa vijiji kuanzisha viwanda vidogo na vya kati ambavyo
viliwanufaisha wafanyakazi na mameneja wa viwanda hivyo ambavyo
havikuwa mali ya serikali kuu. Mwaka 1980 China ilifungua eneo moja la
Shenzen kilichokuwa kijiji kidogo cha wavuvi na kukifanya eneo maalum
la uchumi ambapo wawekezaji kutoka nje waliruhusiwa kuanzisha viwanda.

Eneo la Shenzen lilikuwa na wakazi laki 3 mwaka 1980. Sasa limekuwa
jiji kubwa la watu zaidi ya milioni 10 na maarufu kwa uzalishaji wa
kila aina ya bidhaa za viwandani. Sera ya kufungua maeneo na
kukaribisha wawekezaji toka nje imefanikiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa
uzalishaji za bidhaa za viwandani na umeifanya China kuwa karakana ya
dunia. Kwa nini China ilifanikiwa kukuza uchumi wake kwa kasi ya juu
baada ya mabadiliko ya sera.

Ukuaji wa uchumi unaambatana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka
kutegemea sana kilimo na kuelekea kwenye ongezeko la ajira viwandani,
kutoka nguvu kazi inayoishi vijijini kuelekea nguvu kazi inayoishi
mijini. Mabadiliko ya mfumo wa uchumi husababishwa na ushindani wa
soko.

Serikali ya China ilikuza uchumi kwa kuruhusu ushindani wa soko na
kuyapa fursa makampuni mapya yenye tija kuanza na makampuni yanayopata
hasara kufilisika. Soko la ajira ukiacha mashirika ya umma liliruhusu
makampuni mapya kuajiri wafanya kazi na makampuni yanayopata hasara
kupunguza wafanyakazi. Sheria za kazi zilijikita katika kurahisisha
uanzishwaji wa ajira. Ni vizuri kuwa na utaratibu wa hifadhi za jamii
kwa wafanya kazi wanaopoteza ajira ili kupunguza makali na kuwepo kwa
soko la ajira linalonyumbulika.

Wanaopoteza ajira wapate kipato cha kuwawezesha kuishi wakati
wakitafuta ajira mpya. Katika kipindi cha mabadiliko ya mfumo wa
uchumi, China haikuwa na mfumo mzuri wa hifadhi za jamii. Wafanyakazi
wengi wanaotoka vijijini hawakuwa na huduma za jamii na vibali vya
kuishi katika miji walioenda kufanya kazi. Kwa sababu ya ukosefu wa
hifadhi za jamii, familia ziliwajibika kuweka akiba itakayowasaidia
watakapougua na pia kuwaelimisha watoto wao.

Nchi yeyote haiwezi kuondokana na umaskini bila kukuza uchumi
unaoongeza ajira. Katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi
unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko
la raslimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanisi na tija
katika uzalishaji na utoaji wa huduma. Maendeleo ya teknolojia ndiyo
yanayochea ukuaji wa uchumi. Kabla ya mapinduzi ya viwanda ya karne ya
18, maendeleo ya teknolojia yalitokana na uzoefu wa wakulima kwenye
mashamba yao na mafundi kwenye karakana zao.

Baada ya mapinduzi ya viwanda maendeleo ya teknolojia na uvumbuzi
ulitokana na majaribio ya maksudi na badae uliimarishwa na matumizi ya
sayansi katika majaribio. Ukuaji wa uchumi wa nchi ambazo ziko mstari
wa mbele wa maendeleo na matumizi ya teknolojia uvumbuzi wa teknolojia
mpya au oboreshaji wa teknolojia ya zamani. Kasi ya uvumbuzi wa
teknolojia mpya unategemea uwekezaji katika elimu ya sayansi,
teknolojia na utafiti. Nchi ambazo ziko nyuma katika maendeleo ya
uchumi na matumizi ya teknolojia zina fursa ya kutumia teknolojia
ambayo tayari imeisha gunduliwa.

Kinachohitajika ni kutumia teknolojia iliyopo ukizingatia raslimali
ulizonazo, nguvukazi yako na elimu na ujuzi wake na mazingira ya nchi
yako. Wakati wa uongozi wa Mwenyekiti Mao, mkakati wa maendeleo ya
uchumi ulijikita katika kuwekeza kwenye viwanda vizito na
kujitosheleza bila kushiriki sana katika biashara za nchi za nje.
Taratibu za uchumi wa soko hazikukubaliwa.

Lengo ilikuwa kujenga jamii mpya ya kikomunisti ambapo kila mtu
alitegemewa achangie katika jamii kwa kuchapa kazi kwa kadri ya uwezo
wake na jamii imuwezeshe kupata mahitaji yake muhimu sawa na wananchi
wengine. Matumizi ya bei za soko na motisha kwa wafanyakazi
vilionekana kuwa nyenzo za kibepari. Sera nyingine kama za Hatua Kubwa
Mbele (The Great Leap Forward) na Mapinduzi makubwa ya utamaduni (The
Great Cultural Revolution) yalileta vurugu na kusababisha kuanguka kwa
uzalishaji.

Baada ya kufanikisha mapinduzi ya kikomunisti mwaka 1949 na kuanzia
mwaka 1953 China ilianza kutekeleza mipango ya maendeleo ya miaka
mitano. Mipango hii ilikuwa na lengo la kujenga viwanda vizito na
kutumia utaratibu wa kiutawala wa kugawa raslimali, malighafi na nguvu
kazi katika sekta za uchumi. Pamoja na upungufu wa tija katika
uzalishaji, jambo moja ambalo China ilifanikiwa ni kuboresha huduma za
afya na hasa huduma za kinga ya maradhi na kusambaza elimu ya msingi
kwa wananchi wote.

Katika uongozi wa Deng Xiaoping, China ililegeza masharti ya biashara
na ikaanza kuagiza bidhaa na teknolojia kutoka nje ili kusaidia kuleta
maendeleo ya haraka ya uzalishaji viwandani. Ilianza kutumia vizuri
fursa za kuwa nyuma na kuzalisha bidhaa katika viwanda vilivyoajiri
watu wengi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu, vifaa vya
umeme na elektronoki.

Sehemu kubwa ya bidhaa za viwanda hivi viliuzwa nchi za nje. Ukuaji wa
uzalishaji viwandani ulisaidiwa na ujenzi wa miundombinu imara ya
kufua na kusambaza umeme, ujenzi wa njia za usafirishaji hasa
barabara, reli na viwanja vya ndege. Sera za thamani ya sarafu ya
China zilihakikisha kuwa bidhaa za China zinakuwa na ushindani mkubwa
katika soko la dunia.

China haikusita kupunguza thamani ya sarafu yake ili kuongeza
ushindani wa bidhaa zake katika soko la dunia. Thamani ya sarafu ya
China ilishuka toka yuan 1.5 mwaka 1980 na kufikia yuan 8.6 mwaka 1994
kwa dola moja ya Marekani. Baada ya 1994 sarafu ya China ilikongomewa
kwenye dola ya Marekani, yuan 8.3 zikiwa sawa na dola 1. Ushindani wa
bidhaa za China katika soko la dunia uliongezeka kwa sababu ya
kuongezeka kwa tija na ufanisi uliopunguza gharama za uzalishaji za
China ukilinganisha na nchi nyingine.

Sera za China zimehamasisha uwekaji wa akiba na uwekezaji wa raslimali
na vitega uchumi. Sehemu ya pato la taifa linalowekwa kama akiba
limeongezeka toka wastani wa asilimia 37 katika kipndi cha miaka 1982
– 92 mpaka kufikia asilimia 50 katika miaka ya 2003 – 2010. Uwekaji
mkubwa wa akiba umeiwezesha China kugharamia uwekezaji wa raslimali na
vitega uchumi mkubwa sana uliofikia wastani wa asilimia 42 kwa mwaka
katika kipindi 2003 – 2011. Katika miaka 10 iliyopita ukuaji wa uchumi
wa China umechochewa na uuzaji wa bidhaa nchi za nje na uwekezaji wa
raslimali na vitega uchumi ndani ya China.

Kwa kuwa China inauza bidhaa nyingi nchi za nje kuliko inazoagiza,
imekuwa na ziada katika urari wa malipo ya nchi za nje na kwa hiyo
kuwa na akiba kubwa ya fedha za kigeni. Akiba ya fedha za kigeni ya
China inazidi dola trilioni 3.2 sehemu kubwa ikiwa imewekwa Marekani.
Tangu mwaka 2002, Marekani imekuwa inategemea akiba ya China kuziba
pengo la nakisi ya bajeti ya serikali. Hivi sasa China inashinikizwa
ibadilishe sera, iongeze thamani ya sarafu yake na kuongeza matumizi
ya kawaida ndani ya nchi na kupunguza uwekaji mkubwa wa akiba ili
inunue bidhaa nyingi kutoka nje na ipunguze uuzaji wa bidhaa zake nchi
za nje.

Sera ya Ujamaa ya Tanzania ilishawishiwa sana na ujamaa wa China.
China ilipoanza kubadili sera mwaka 1978, Tanzania iliendelea
kusisitiza msimamo mkali wa ujamaa kama ulivyoainishwa katika Mwongozo
wa CCM wa mwaka 1981. Mabadiliko ya sera Tanzania yalishinikizwa na
mashirika ya kimataifa hususani IMF na Benki ya Dunia na wahisani wa
nchi za magharibi baada ya uchumi luporomoka mwanzoni wa miaka ya
1980. Mabadiliko ya sera nchini China ulitokana na mapambano ya
kisiasa na fikra ndani ya China yenyewe.

Deng alitumia ushauri hasa wa Lee Kuan Yew, Waziri Mkuu wa Singapore
na wataalam wa Benki ya Dunia lakini Wachina wenyewe ndiyo
walioendesha usukani wa mabadiliko. Utekelezaji wa sera za mabadiliko
nchini Chinaulifanywa kwa majaribio. Mabadiliko ya sera za kilimo
yalijaribiwa katika eneo dogo. Yalipoonekana kuwa na mafanikio
yalisambazwa maeneo mengine. Ukaribishaji wa wawekezaji viwandani
kutoka nje ulianza Shenzen eneo lilioko karibu na Hongkong na
ulipofanikiwa maeneo mengine yaliruhusu uwekezaji toka nje.

China haikubinafsisha mashirika ya umma, bali hatua kwa hatua
waliruhusu makampuni binafsi kuanzishwa na kushindana na mashirika ya
umma. Sekta ya fedha na mabenki bado inashikiliwa na dola. Serikali ya
China iliweka kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu na kwa hiyo
kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa vitega uchumi katika sekta ya
viwanda. Mambo muhimu tunayoweza kujifunza kutoka China.

Kwanza Watanzania wenyewe ndiyo tuendeshe usukani wa mabadiliko.
Tujifunze toka uzoefu wa nchi nyingine lakini tusiendeshwe na wengine.
Katika utekelezaji wa sera mpya serikali inapaswa kufanya majaribio
eneo dogo, kujifunza kama sera ina mafanikio itekelezwa katika maeneo
mengine. Kama haifai iachwe. Kwa mfano sera ya maeneo maalum ya uchumi
itekelezwe vizuri katika eneo moja na kuona matunda yake badala ya
kuanza maeneo mengi madogo madogo yasiyokuwa na miundombinu ya kutosha
kama ilivyo hivi sasa.

Serikali ya China imeweka kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu.
Kila inapowezekana China inatumia utaratibu wa wale wanaonufaika na
huduma za miundombinu walipie huduma hizo. Tanzania inaweza kujifunza
toka China kwa kukamilisha miradi ya miundombinu inayoanzishwa kabla
ya kuanza mingine na kuwa na mipango ya ujenzi wa miundimbinu
inayotekelezeka.

Sera za sarafu zinazohakikisha ushindani wa kibiashara ni muhimu
katika maendeleo ya viwanda. Hata hivyo izingatiwe kuwa ongezeko la
tija na ufanisi katika uzalishaji liambatane na sera ya sarafu
inayohakikisha ushindani wa kibiashara. Tanzania inaweza kutumia fursa
zilizopo katika kuwa nyuma katika maendeleo ya uchumi na teknolojia.
Ikiwa tutajipanga na kutumia teknolojia iliyopo tunaweza kuongeza tija
na ufanisi katika uzalishaji kama walivyofanya Wachina. Mfumo wa soko
unaofanya kazi kwa ufanisi ni sharti muhimu la kuchochea ukuaji wa
uchumi unaoongeza ajira. Bei ya bidhaa na mishahara ya nguvu kazi
iambatane na upatikanaji wake.

Uongozi wenye dira na uliyo tayari kujifunza na serikali madhubuti
ndiyo msingi wa kujenga uchumi unaoongeza ajira. Changamoto ya ziada
kwa Watanzania ni kupata uongozi wenye dira na serikali madhubuti kwa
njia za kidemokrasia ili tuweze kujenga uchumi utakaoleta neema kwa
Watanzania wote.

Katika mahusiano yetu ya biashara na uwekezaji ni muhimu kwa Tanzania
kuwa na sera na mpango madhubuti ya uwekezaji wa miundo mbinu na
kuusimamia ipasavyo. Misaada ya China itusaidie kutekeleza mpango
wetu. Tatizo ni udhaifu mkubwa wa mipango yetu. Serikali imekuwa na
mipango mingi isiyo tekelezwa au kutekelezeka.

Kuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 ambayo inalenga kuwa Tanzania
iwe ni nchi yenye kiwango cha kati cha mapato (middle income country)
na hali bora ya maisha kwa wananchi. Mpango Maalum wa Kuharakisha
Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Mini Tiger Plan 2020) ambao
haijulikani umeishia wapi.

Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania – MKUKUTA I na
MKUKUTA II na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2010-15. MKUKUTA I
na MKUKUTA II hazikufanyiwa makadirio ya gharama za utekelezaji wake.
Gharama za mpango wa miaka mitano ni kubwa mno na serikali haina fedha
ya kuugharamia. Serikali imevamia mkakati mwingine wa Big Results Now.

Lazima tuwe na mkakati wetu wa kujenga viwanda. Tanzania isiwe chanzo
cha malighafi tu za kuuza China. Gharama za uzalishaji viwandani
katika nchi ya China zinaongezeka na ajira ya watu milioni 90
inategemewa kuhamia nchi nyingine. Ni vyema Tanzania ikajipanga kuwa
nchi itakayoweza kuongeza ajira kwa wingi kwa shughuli za uzalishaji
viwandani zinazohama toka China.

Tunapaswa kutenga eneo kubwa la kilomita za mraba 100- 200 karibu na
bandari ya Tanga na Mtwara na kwa kushirikiana na sekta binafsi
kulisheheni miundombinu na kulifanya kuwa eneo maalum la kuendeleza
viwanda vya kuuza bidhaa nch za nje. Wawekezaji wa ndani na nje
wajengewe mazingira mazuri yanayovutia kuwekeza na kuongeza ajira.
Wawekezaji toka China watumie wafanyakazi wa Tanzania na siyo kuleta
wafanyakazi toka China kwa shughuli zinazowezwa kufanywa na
Watanzania.

Serikali iwe makini na kuhakikisha hatuleti Wawekezaji matapeli kama
muwekezaji wa Ujenzi wa Terminal ya Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam.
Ulinzi wa mazingira uzingatiwe katika uwekezaji wa viwandani na katika
uvunaji wa maliasili yakiwemo madini.

China ni taifa kubwa litakalokuwa na uchumi mkubwa kuliko nchi zote
duniani katika miaka 20 ijayo. Tanzania tujipange vizuri kuwa na
mahusiano ya kiuchumi na China yatakayokuwa na manufaa kwa nchi yetu.

Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa, CUF

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment