Sunday 17 March 2013

[wanabidii] Kukamatwa Ludovick Joseph kuhusiana na tukio la Kibanda; Lwakatare

Habari kutoka kwenye gazeti la MTANZANIA:

MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph Ludovick, amekamatwa na
Jeshi la Polisi akihusishwa na matukio ya kigaidi ambayo yamelitikisa
taifa katika siku za karibuni.

Habari za kuaminika zilizozifikia MTANZANIA Jumapili zimeeleza kuwa,
Tume ya watu 12 iliyoundwa na serikali kupitia vyombo vyake vya
usalama kuchunguza tukio la kutekwa na kuteswa kinyama kwa Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd. Absalom Kibanda,
imemkamata Ludovick akiwa mkoani Iringa.

Kwamba, Ludovick amekamatwa na makachero wa polisi baada ya kupatikana
kwa taarifa zinazomhusisha kupanga njama za kudhuru watu na pia kuwepo
kwa mazingira yenye shaka kuhusu mwenendo wake usiku wa tukio la
kutekwa kwa Kibanda.

Hata hivyo, taarifa nyingine zilizopatikana zinadaiwa kuwa kukamatwa
kwa Ludovick, ambaye pia anadaiwa kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama
wa Taifa, ni mkakati unaoratibiwa kwa umakini wenye lengo la kupoteza
mwelekeo wa uchunguzi wa tukio la kutekwa na kuteswa kinyama Kibanda.

Kibanda alitekwa na kujeruhiwa usiku wa kuakia Machi 6 mwaka huu,
nyumbani kwake Mbezi, jijini Dar es Salaam, akiwa ndani ya gari lake
akisubiri kufunguliwa geti aingie ndani.

Katika tukio hilo, Kibanda alijeruhiwa kwa kupigwa mapanga kichwani,
kung'olewa meno na kucha, kutobolewa jicho na kunyofolewa kidole.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi zilieleza
kuwa Ludovick, ambaye ni mkazi wa Jijini Dar es Salaam, alikamatwa
juzi akiwa mkoani Iringa.

Habari za kukamatwa kwa Ludovick zilianza kuenea tangu juzi usiku
katika mitandao mbalimbali ya kijamii, kabla ya jana kuthibitishwa na
polisi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia kwa viongozi wake wakuu, akiwemo,
Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, walikwepa
kuzungumzia tukio hilo.

Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, alipotafutwa na MTANZANIA
Jumapili kupitia simu yake ya kiganjani ili kuthibitisha kukamatwa kwa
Ludovick alishindwa kukubali au kukataa.

Senso alilitaka gazeti hili liliache Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi
wake na kisha kutoa taarifa yake baadaye.

Kuhusishwa kwake na tukio la Kibanda
Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa siku na wakati ambao
Kibanda alitekwa na kuteswa, Ludovick naye alidai kutekwa na majambazi
akiwa eneo la Sinza, jirani na mahali ilipo ofisi ya Kibanda.

Duru za habari zinaeleza kuwa Ludovick alidai kutekwa na watu
wasiojulika majira ya saa tano usiku siku ya Jumanne ya Machi 5, mwaka
huu, ambapo watekaji wake walimnyang'anya vitu vyake mbalimbali na
kumvua nguo zote.

Taarifa hizo zinathibitishwa na mwanablog maarufu, Maggid Mjengwa,
ambaye katika andishi lake aliloweka kwenye mitandao ya kijamii jana,
anaelezwa kuwa Ludovick, alidai kutekwa na kuvuliwa nguo na kwamba
tukio hilo aliripoti katika kituo cha Polisi cha Kigogo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Mjengwa kwenye gazeti hili na yale
aliyoyaeleza kwenye mtandao wa Jamii Forum, siku ya kutekwa na kuteswa
kwa Kibanda alikuwa pamoja na Ludovick kwenye mgahawa wa Rose Garden,
ambako walikula chakula jioni kabla ya kuondoka pamoja kwenye gari
lake hadi eneo la Sinza Shekilango, alipomuacha akidai kuchukua
usafiri wa umma kuelekea nyumbani kwake eneo la Tabata.

Mjengwa anasema baadaye usiku huo, Ludovick alikwenda hadi hoteli
aliyofikia eneo la Kariakoo, huku akiwa hana nguo na kumueleza kuwa
alitekwa na majambazi muda mfupi baada ya kuachana naye.

Anasema taarifa za kutekwa kwake (Ludovick) aliziripoti katika kituo
cha Polisi Kigogo, ingawa kwa mujibu wa maelezo aliyompa Mjengwa ni
kwamba alipofika Shekilango, alichukua bajaj ambayo alipanda na watu
wengine wawili, yeye akiwa katikati na alipofika katika eneo la Relini
Tabata alihisi watu aliokuwa nao ni majambazi.

Hata hivyo, haijajulikana mara moja ni kwa nini akiwa alitekwa eneo la
Relini, alikwenda kuripoti tukio hilo katika kituo cha Polisi cha
Kigogo.

Pia haijajulikana sababu za kukimbilia hotelini alikofikia Mjengwa
badala ya nyumbani kwake, Tabata.

Maswali hayo pia yamempatia kigugumizi Mjengwa, ambaye hata hivyo
anakiri kumfahamu Ludovick anaeleza kuwa amekuwa akimsaidia baadhi ya
kazi zake za kihabari, lakini anasema hamfahamu sana.

Ludovick ni miongoni mwa watu waliofika katika Hospitali ya Muhimbili
asubuhi kumjulia hali Kibanda, na alikaa hadi Kibanda anasafirishwa
kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Ahusishwa na video ya Lwakatare
Habari zaidi zilizolifikia MTANZANIA Jumapili, zinadai kuwa Ludovick
ndiye mtu aliyerekodi video ambayo Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare,
anaonekana akipanga mipango ya kudhuru watu mbalimbali, wakiwemo
waandishi wa habari.

Wapasha habari wetu wanaeleza kuwa Ludovick ndiye mtu ambaye sauti
yake inasikika katika video hiyo, hata hivyo habari hizo
hazijathibitishwa na Jeshi la Polisi.

Katika video hiyo iliyosababisha Lwakatare atiwe nguvuni na Polisi
hadi sasa, Ludovick anadaiwa kuwa ndiye mtu ambaye alikuwa akimuuliza
maswali Lwakatare, wakati wakiandaa mipango hiyo.

Watu wa karibu na Ludovick waliliambia gazeti hili kuwa, Lwakatare na
Ludovick wana uhusiano wa karibu na kwamba wote ni wenyeji wa Mkoa wa
Kagera.

Kwa mujibu wa watu hao, ukaribu kati ya Ludovick na Lwakatare ni wa
muda mrefu na amepata kumsaidia kufanya kampeni za kuwania ubunge wa
Jimbo la Bukoba Mjini mwaka 2000.

Wakati huo huo, inadaiwa kuwa Lwakatare mwenyewe amekiri kuwa mtu
anayeonekana akizungumza katika mkanda wa video maneno ya kupanga
matukio ya utekaji ni yeye na pale anapoonekana akizungumza ni
nyumbani kwake, lakini amekataa kwamba maneno anayozungumza si yeye.

Ludovick ni nani?
Ludovick, mbali na kuwa na ukaribu na Lwakatare, pia ni mtu wa karibu
na Mjengwa, akimsaidia katika shughuli mbalimbali hususani katika blog
yake.

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba Ludovick ni mtu wa idara
ya usalama wa taifa na watu ambao wako naye karibu wanasema hawajui
anafanya kazi gani zaidi.

Alipoulizwa ni kazi gani ambayo Ludovick anafanya, Mjengwa alisema
hajui.

Ila katika maelezo yake aliyoandika kupitia kwenye mtandao wa Jamii
Forum, Mjengwa anasema anamfahamu Ludovick tangu akiwa Chuo Kikuu
(DUCE) na kwamba ni mmoja wa Watanzania wengi waliomfahamu kupitia
kazi zake magazetini.

Haijaeleweka mara moja uhusiano wake na Lwakatare ni wa aina gani na
katika kazi gani.

Source: http://www.wavuti.com/#ixzz2NnLqr19N

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group and stop receiving emails from it, send an email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.

0 comments:

Post a Comment