Thursday 24 January 2013

[wanabidii] SIYA KUKOSA! TAARIFA YA CHADEMA KWA WAANDISHI WA HABARI.

MKUTANO NA WAANDISHI MAKAO MAKUU YA CHADEMA JANUARI 22, 2012


NDUGU waandishi wa habari,


Kuna mambo mengi yamezungumzwa na CCM katika siku za karibuni, kuhusu CHADEMA.Nanyi waandishi wa habari mmekuwa mkitupigia simu, mmoja mmoja kutaka ufafanuzi na msimamo wa chama chetu kuhusiana na masuala hayo. Leo tumeamua kuwaita hapa ili kuwapa ufafanuzi mkiwa pamoja badala ya kila mmoja kuuliza akiwa kwenye chumba chake cha habari.


Kwanza, CCM kupitia kwa viongozi wao waandamizi, akiwemo Nape na Mwigulu,wanazunguka zunguka huko, kuwaambia Watanzania kuwa CHADEMA inakufa, tena wanatengeneza hata sababu za kifo, wanasema ni ubaguzi na kutokana na laana ya Mwalimu Nyerere.


Tunataka kuwaambia hivi: Kwamba CHADEMA haina ubaguzi na hivyo haiwezi kufa leo wala kesho, mpaka iwe imetimiza kazi yake ya kuwakomboa Watanzania. Na bahati mbaya, CCM wanaona CHADEMA kitakufa, wanasahau kuona kuwa chama chao tayari kinakufa tayari.


Kama suala ni laana ya Nyerere. Laana hiyo haiko CHADEMA; iko ndani ya CCM kwa sababu mbalimbali, leo hapa tutataja chache;


(i)
Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake, kwa kushirikiana na waasisi wengine,alijenga misingi ya utaifa wetu, ambapo CCM wameamua kuivunja kwa maslahi ya wachache. Akiwa bado hai, Mwalimu alitunga hata kitabu akasema CCM kimeoza na kinanuka rushwa. Akaongeza CCM kuna kansa ya uongozi na uchaguzi ndani ya chama hicho, ni gulio la wala rushwa (kura). Maneno hayo ni laana tosha.
(ii)
CCM kinapata laana ya Mwalimu Nyerere kwa sababu kimerasimisha ubaguzi kwa wanachama wao, viongozi wao na Watanzania kwa ujumla. Ni hawa hawaCCM wanaoeneza uongo wa hatari, wakiwatisha wananchi kwa kusema CHADEMA kina ukabila, mwaka 2005 walimzushia Dk. Salim Ahmed Salim uongo kuwa ni Mwarabu na alihusika na kifo cha aliyekuwa mmoja wa wasisi wa taifa hili, Abeid Amani Karume. Uchafu ulifanywa na wana CCM wa kundi lawanamtandao ambao leo ndiyo wanaongoza chama na serikali na ubaguzi huu dhidi ya Dk. Salim ndiyo uliowafanya washinde uchaguzi wa ndani ya chama chao, kwenye kura za maoni.
(iii)
CCM kinakufa pia kwa sababu ya laana ya ubaguzi wa kuwezesha raia kupata haki zao na badala yake vyombo vya dola chini ya Serikali inayoongozwa na CCM viko mstari wa mbele kukiuka haki za raia. Ninyi ni mashahidi namna ambavyo baadhi ya makundi ya wafanyakazi yamekuwa yakibaguliwa katika kupata stahiki zao. CCM na serikali yake, imekuwa ikijibu kwa kauli za kejeli na vitisho, ikiwemo kutekwa na kuteswa kwa mmoja wa viongozi wa wafanyakazi na kisha kutupwa katika Msitu wa Mabwepande na baadaye kulinda wahalifu kwa visingizio vingi vya kulindana huku wakichezea maisha na uhai wa Watanzania wenzetu. CCM inayokufa imeacha misingi yake ya kuwa chama cha wafanyakazi na badala yake imejichimbia kaburi kwa kuongeza pengo la tofauti za mishahara na maslahi ya wafanyakazi katika utumishi wa umma. Kwa upande mwingine, unaweza kuielezea vipi hali ya serikali ya CCM kutowalipa wazee wastaafu waliokuwa watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kama si ubaguzi! Wazee ambao wametumikia taifa hili kwa uwezo wao, akili zao na miili yao, wenzao wote katika nchi nzingine zilizokuwa zikiunda EAC wakati ule, walishalipwa, isipokuwa hapa Tanzania ambapo chama kinachotawala kimeamua kufanya ubaguzi wa haki za watu, nani apate na yupi asipate. Itakumbukwa kuwa wazee wale kutokana na kuyumbishwa na kubaguliwa katika kupata haki zao, waliamua kuvua nguo barabarani, pia kwa kiburi na ukosefu wa heshima ya serikali ya CCM kwa wananchi, wakawachapa viboko wazee wale! Laana ya wazee hawa inakiua CCM.



Si ubaguzi tu; bali pia CCM kinakufa kutokana na laana za watanzania wanaokerwa na sera mbovu na uongozi dhaifu wa chama hicho kusababisha ongezeko kubwa la gharama za maisha kwa wananchi. Hivyo basi, CCM kinakufa kutoka na laana hiyo na uongo uliosababisha na kushindwa kutekeleza ahadi zake za maisha bora kwa kila mtazania, ajira kwa vijana na kuwezesha wanawake. Hali hii inafanya umma uendelee kuunga mkono CHADEMA na vuguvugu la mabadiliko (M4C) bila kujali propaganda chafu za CCM.


CCM wajiandae kufuata njia za vyama vya KANU ya nchini Kenya, UNIP ya Zambia na chama cha ukombozi nchini Malawi.


Ndani ya CHADEMA kuna baraka za Mwalimu Nyerere. Hakuna laana. Ninyi ni mashahidi kuwa kabla ya Mwalimu kufariki dunia, alikimwagia sifa CHADEMA kwa kusema ni chama makini chenye sera bora.


Tofauti ya CCM na CHADEMA


Kwenye mikutano yao, sasa CCM wamejipatia majukumu wasiyoyamudu ya kujifanya ni maofisa waenezi wetu na moja ya majukumu waliyoamua kujipachika na kuyafanya ni kuwaonesha Watanzania, moja ya tofauti kati yetu na wao, ambazo ni uwezo wa kuchukua hatuana kuwa na sera sahihi mbadala kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Watanzania.


Kwenye mkutano wao uliomalizika hivi karibuni na kwenye shughuli zao za kila siku, CCM sasa wameamua 'kuimba' sera za CHADEMA, hasa zile za katiba mpya, elimu bure na kushusha bei ya vifaa vya ujenzi. Mambo ambayo miaka miwili tu iliyopita walikuwa wakiimba kinyume chake. Bahati mbaya hawana uwezo wa kuzitekeleza kwa ufanisi, kwa sababu si mawazo yao na hawana utashi huo.


Hili la pili la kuchukua hatua…bahati mbaya kwa sababu ya kuelemewa na kansa ambazo tumezitaja hapo juu, CCM wanaona kuchukua hatua ni 'kufukuzana', maneno ambayo hata jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari wameyarudia. Hawawezi kuona kwa sababu wote ni wachafu, wanaishi hivyo kwa kukubaliana.


Ndugu wanahabari, hii ni moja kati ya tofauti nyingi zilizopo kati ya vyama hivi viwili, ambazo zimeifanya leo CHADEMA ndiyo tumaini la watu wanaodai haki na uwajibikaji, tumaini la watu katika kupigania uhuru na mabadiliko ya kweli nchini, kimbilio la watu wasafi dhidi ya ufisadi, wanaopinga ubadhirifu na dhuluma ya CCM, ni tofauti hizo zinakifanya CHADEMA kuwachama kikuu cha upinzani na mbadala kinachoaminiwa na Watanzania kukabidhiwa dola.


Tukiwa chama imara na makini kinachoaminiwa na kubeba matumaini ya Watanzania, tutachukua hatua mbalimbali, dhidi ya makosa tofauti tofauti, kulingana na uzito wake, kama vile uzembe, udhaifu, ubadhirifu, ufisadi na usaliti.


Tuwachukulia hatua hata wale ambao wametumwa au wanaotumika na CCM kufanya kazi ya chama hicho kupitia jina la CHADEMA.


Ni uwezo na uthubutu wa kuchukua hatua mbalimbali, ndiyo umekuwa moja ya sababu kubwa ya Watanzania kuiunga mkono CHADEMA kila tunaponyoosha mkono kuikemea CCM na serikali yake juu ya ufisadi, ubadhirifu na uminyaji wa haki za Watanzania.


Zamani, CCM kilipokuwa bado chama cha siasa hasa, ambapo kilikuwa kinasimamia misingi ya umoja wa kitaifa bila kujali dini ya mtu, kabila au rangi; kilipokuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi rushwa na ufisadi na uwajibikaji wa pamoja, yaani CCM ya enzi za Mwalimu Nyerere na waasisi wengine waadilifu, hakika kilikuwa na uwezo wa kufukuza kila aliyeonekana kwenda kinyume na misingi yake.


Ni katika kipindi hicho, CCM kiliwavua uongozi na uanachama baadhi ya waliokuwa viongozi wake. Kwa mfano, Maalim Seif Shariff Hamad, Hamad Rashid Mohammed, Sudi Yusuf Mgeni, Fortunatus Lwanyantika Masha na wengineo. Baadaye mwaka 1984 kilimfukuza uongozi(msisitizo uongozi) aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, kwa kukiuka misingi yao.


Lakini leo hii, CCM hakiwezi kuchukua hatua hiyo hata kwa katibu wa tawi. Kwa sababu, hiki si chama cha siasa tena. Hili ni genge la wahuni, waliojikusanya pamoja na kujiita chama cha siasa. Ni wezi wa raslimali za taifa, waliotayari kulirejesha taifa kwenye utumwa kwa maslahi yao binafsi.


Ndiyo maana wameshindwa kuwafukuza mafisadi, badala yake ndiyo wanaoongoza chama na kuwatawala. Walisema wanataka kujivua gamba (la nyoka) baadae wakagundua kuwa gamba lao halisi (ufisadi) ni gamba la kobe, ambalo ili livuke ni lazima kobe afe!


CCM ya sasa, hakiwezi siyo tena kutetea wafanyakazi na wakulima. Hakitetei tena maslahi ya wanyonge. Kimebeba na kukumbatia ufisadi na mafisadi wa kila aina, na wabadhirifu wa mali za umma, ambao wameyafikisha maisha ya Watanzania na nchi yao hapa yalipo.


Lakini CHADEMA inachukua hatua kwa sababu hiki ni chama sikivu na kinachobeba matumaini ya wananchi. Hivyo, hatuko tayari kumuacha mtu yeyote ambaye anafanyakazi za CCM ndani ya CHADEMA, kisha kujiita yeye ni mwana-Chadema. Tutamfukuza.


Huwezi kuzusha uongo kwa viongozi wako na chama chako, kisha ukataka uachwe. Usijadiliwe. Usiguswe. Tutakujadili na tukibaini kuwa una makosa, tutakuomba ujirekebishe. Ukikataa, tunakuambia hutufai. Ondoka. Ukishindwa, tunakufukuza.


CCM kupitia mawakala wao wanasema: CHADEMA kinapokea ruzuku kubwa, lakini kimepanga ofisi. Hii nyumba ni mali ya Chadema. Lakini mbona hao mawakala wa 'status quo'hawasemi kuwa CCM haina ofisi? Maana ile inayoitwa ofisi ya CCM Makao Makuu Dodoma, ni mali ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).


Huyu Nape hana hata maadili ya uongozi. Alifukuzwa kwenye UV-CCM baada ya wenzake kumwambia amezusha uongo. Baada ya kuitwa kujitetea, akasingizia kuwa alilishwa maneno na waandishi wa habari. Kumbe wenzake walikuwa na mkanda wa hotuba yake aliyoitoa pale Peacock Hotel. Wakampa aisikilize. Eti ndipo akakiri na kuomba radhi. UV-CCM chini ya Emmanuel Nchimbi, ikamwambia hutufai. Muongo wee.


Hapa tunaweka rekodi zake sawasawa. Tunataka umma umfahamu vizuri, kwa sababu wasiomjua wanaweza kuamini maneno yake.


Kauli za Mwigulu Nchemba


Tunataka kuwaambia wahusika wa usalama na ulinzi nchini, hususan Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid, nini maana ya tafsiri ya habari za kutunga, lakini za hatari sana za Mwigulu Nchemba;


(i) Kwamba suala la yeye kusema CHADEMA inapanga mauaji, tunataka kumwambia Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othuman Rashid kuwa, kwa sababu wamekuwa kimya na kukubaliana na uzushi wa hatari wa Mwigulu, tafsiri yake ni kwamba Jeshi la Polisi limeasi na sasa linafanya kazi kwa maelekezo ya CHADEMA. Linatekeleza amri za CHADEMA!


Kwa sababu, iko wazi. Watanzania na dunia inajua kuwa mauaji yenye utata yanayohusishwa na siasa, yamefanywa na Jeshi la Polisi. Ushahidi upo. Polisi wameua watu Arusha, polisi wameua watu Songea, polisi wameua mtu Morogoro, polisi wameua mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi.


Orodha ya mauaji ya vitendo vya mauaji vinavyofanywa na Jeshi la Polisi nchini ni ndefu, kwa malengo ya kisiasa ya CCM. Lakini kama Mwigulu anasema, hiyo ni mipango ya CHADEMA, maana yake ni kwamba Jeshi la Polisi linatekeleza mipango ya chama hiki, tafsiri ya haraka hapo, Mwigulu anamaanisha, "basi jeshi limeshaasi."


Sasa mtu anayetangaza 'uasi' wa jeshi kwa kiwango cha kutekeleza mipango ya chama cha siasa badala ya kumsikiliza Amri Jeshi Mkuu, serikali inamnyamazia na kumchekea!


Tumeitaka serikali kufanya uchunguzi huru kwenye matukio ya mauaji yanayohusishwa na siasa, ikiwemo tukio la kifo cha kada na kiongozi wa CCM huko Ndago, Singida, lakini wamekaa kimya. Badala yake unatungwa uongo ambao Mwigulu anaendelea kuueneza.


(ii)Tafsiri nyingine ya maneno ya kutungwa hayo anayoeneza Mwigulu ni kwamba vyombo vinavyohusika katika ulinzi na usalama, vimeshindwa kazi. Ni maneno ya aibu kwa IGP Mwema na Othman Rashid, kwamba wao wameshindwa kazi zao na sasa wamemkabidhi Mwigulu, ambaye anaweza kuingia kwenye vikao vya CHADEMA, akarekodi, kisha badala ya kuwapelekea hao wenzake, ili serikali ya chama chake ichukue hatua, anazunguka nao kulia kwenye vyombo vya habari! Na wahusika wamekaa, wanamsikiliza na kumchekea!


CHADEMA kiko tayari kushika dola, kuwatumikia wananchi. Tunajua mipango yao katika hayo maneno ya Mwigulu. Tunaelewa wanachotaka kufanya. Tuko imara.


Tunawashukuru Watanzania kwa kuendelea kutuunga mkono, katika harakati hizi za ukombozi wa nchi yetu.


CHADEMA itaendelea na dhima yake ya kusimamia uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu na wananchi wake.


Asanteni sana kwa kunisikiliza.





Imetolewa leo tarehe 22 Januari 2013 na:


…………………………………………………


Benson Singo Kigaila,


Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo (CHADEMA)
Sent from my BlackBerry® smartphone on the Tigo Tanzania Network

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment