Saturday 12 January 2013

[wanabidii] MAONI KUHUSU KATIBA MPYA Kutoka kwa: M.M. Mulokozi

DEMOKRASIA NA KATIBA MPYA NCHINI TANZANIA

 

MAONI KUHUSU KATIBA MPYA

 

Kutoka kwa: M.M. Mulokozi [Januari 2013]

 

Profesa Mstaafu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, S.L.P. 35110, Dar es Salaam: [tamulokozi50@yahoo.co.uk]

 

Wakati tunajadili utungaji wa Katiba mpya ya Tanzania, ni vizuri tukatafakari kwanza misingi itakayotuongoza katika kuandaa maudhui ya Katiba hiyo. Katika waraka huu napenda kutoa mawazo machache kuhusiana na suala hilo. Napendekeza misingi ifuatayo:

-       Kujenga umoja na utambulisho wa kitaifa

-       Kupanua uhuru na haki za msingi za raia

-       Kupanua demokrasia

-       Kuweka mfumo wa uwazi wa utawala na uongozi, na kudhibiti ufisadi

-       Kuimarisha uchumi na uzalishaji

-       Kujenga umoja na ushirikiano wa kikanda,na hatimaye Umajumui wa Afrika nzima.

 

Kabla sijajadili misingi hiyo nizungumzie kidogo suala la mchakato wa kuandaa Katiba. Katiba ni chombo chenye mamlaka juu ya kila mtu na kila chombo katika jamii. Katiba lazima itawale mamlaka zote – kuanzia kwa Rais hadi kwa balozi wa nyumba kumi, hadi kwa mtu binafsi. Katiba sharti itawale asasi zote, kuanzia kwa Bunge, hadi mahakama, polisi, asasi za kiraia na kidini, n.k. Ndiyo maana haifai kwa Katiba kuamuliwa na vyama vya siasa, ambavyo ni vikundi vyenye maslahi maalumu ndani ya Katiba hiyo.

 

Kujenga Umoja na Utambulisho wa Kitaifa

 

Katiba yoyote ile ya nchi huwa na jukumu la kujenga utaifa na utambulisho wa Taifa linalohusika, na hivyo kuchunga na kulinda usalama na uzalendo wa Taifa hilo. Ndiyo maana katiba za mataifa mengi hutaja mipaka ya nchi, Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, Lugha ya/za Taifa, na lugha nyingine rasmi kama zipo. Katiba za baadhi ya nchi, hutaja hata hati za maandishi za lugha yao, na vipengele muhimu vya utamaduni wa Taifa, kama vile dini, mila, na kadhalika. Katiba ya sasa ya Tanzania inataja baadhi ya mambo haya, lakini si yote. Kwa mfano, haitaji Lugha ya Taifa!

 

Kujenga utambulisho na utaifa ni pamoja na kujenga umoja wa kitaifa, kuweka misingi imara ya umoja inayokubalika kwa wananchi wote wa makundi na matabaka yote, kujenga uzalendo, mapenzi ya nchi, na moyo wa kuwa tayari kuitetea na kuifia nchi ikibidi.

 

Ni wazi kwamba suala la kuruhusu uraia wa nchi mbili au zaidi ambalo linapigiwa debe sana hivi sasa na baadhi ya watu inabidi litazamwe kwa kuzingatia msingi huu wa uzalendo na maslahi ya Taifa: Mathalan, itakuwaje iwapo raia wa Marekani [au nchi nyingine], ambaye pia ni raia wa Tanzania, atatumwa na Rais wake wa Marekani na kupewa nyenzo zote kuja kututawala na kutekeleza matakwa ya nchi yake [ya Marekani] hapa kwetu? Utamzuiaje? [Haya tayari tumeyaona katika baadhi ya nchi]. Hatusemi kwamba kiongozi asiyekuwa na uraia wa nchi ya kigeni hawezi kutumiwa na nchi hiyo kutekeleza maslahi yake katika nchi anayoiongoza. Tunawafahamu viongozi vibaraka wengi waliotumiwa hivyo. Tunachosema hapa ni kwamba tusiwarahisishie maadui zetu mchakato wa kupata vibaraka miongoni mwetu.

 

Suala la utamaduni sharti lipewe uzito kikatiba, maana bila utamaduni hakuna Taifa, na njia ya uhakika ya kumdhibiti na kumtawala mtu ni kumteka kitamaduni na kiakili. Hapa suala la lugha sharti lipewe uzito unaostahiki; lugha ya Taifa – Kiswahili – ipewe nafasi muhimu kikatiba, na lugha za kijamii na za kigeni tunazozihitaji zisisahaulike. Katiba itaje wazi kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa na lugha rasmi ya kwanza, na Kiingereza ni lugha rasmi ya pili; Katiba ielekeze kwamba itatungwa sheria mahsusi itakayofafanua nafasi, dhima na matumizi ya lugha ya Taifa na lugha nyinginezo katika jamii.

 

Kupanua Uhuru na Haki za Raia

 

Katiba inapaswa kulinda uhuru na haki za raia, ambazo ni pamoja na haki za kuishi, kuheshimiwa kama binadamu, kufanya kazi na kupata malipo ya haki kwa kazi hiyo, kupewa pensheni ya uzeeni, kujumuika, kusafiri, kuishi popote, kuabudu au kutokuabudu. Haki za lugha na utamaduni pia zinahusika hapa. Na haki hizo lazima ziwe ni kwa raia wote bila kujali jinsi, kabila, rangi, dini, cheo, umri au nasaba. Katiba ya sasa inatoa haki hizo kwa kiasi fulani; Katiba ijayo ingefaa isisitize na kufafanua zaidi haki hizi za msingi.

 

Kumtaja Mungu katika Katiba

Hapa tunaweza kueleza kuwa pendekezo la Jaji Mstaafu Samatta katika kongamano moja kuwa Katiba mpya itaje "Mwenyezi Mungu" halikubaliki kwa sababu linakwenda kinyume na uhuru wa kuabudu tunaouzungumzia. Kwa kuwa Katiba tayari inatoa uhuru wa kuabudu, hakuna sababu ya kuufunga uhuru huo kwa kuuhusisha na imani fulani maalumu – zile zinazozingatia dhana ya "Mungu." Ni vyema Katiba iendelee kutofungamana na imani ya dini yoyote.

 

Kupanua Demokrasia

 

Katika ulimwengu wa sasa na ujao utawala wa kidemokrasia hauepukiki. Hivyo tunahitaji Katiba inayotambua haki na haja hiyo ya kujenga na kuimarisha demokrasia. Demokrasia tunayozungumzia hapa ni demokrasia pana inayojumuisha wananchi wote wa makundi yote; hatuzungumzii demokrasia ya vyama vya siasa tu. Katiba yetu ya sasa, kwa kiasi kikubwa, inajikita katika demokrasia ya vyama badala ya demokrasia ya Umma. Labda hili linahitaji ufafanuzi zaidi:

 

Miaka kadha iliyopita makundi mbalimbali ya wanasiasa yalianza kufanya kampeni ya kutaka majimbo ya uchaguzi yaongezwe ili "kuimarisha" uwakilishi na demokrasia. Tulishuhudia madiwani wa halmashauri mbalimbali wakipitisha maazimio ya kuongeza majimbo ya udiwani na ubunge. Baadhi ya wabunge na vyama vyao vilevile walipendekeza majimbo mapya yaanzishwe. Kampeni hiyo ilifanikiwa kwa kiasi fulani, na majimbo mapya kadha yaliundwa, japo ilitolewa tahadhari kuwa jengo la sasa la Bunge mjini Dodoma halina nafasi ya kuongeza wabunge wengi. Msingi wa kampeni hii ni dhana potofu kuwa demokrasia maana yake ni kuwa na wawakilishi wengi wa vyama katika bunge na mabaraza ya madiwani.

 

Mtazamo huu wa kimajimbo kuhusu uwakilishi unadaiwa kutokana na mfumo wa Westminster, yaani mfumo wa bunge la Uingereza. Hii ni kweli kwa kiasi fulani tu. Waingereza wana utaratibu wa uwakilishi wenye historia ya karne nyingi za mapambano ya kitabaka na kikatiba kati ya mamwinyi, mabwanyenye, watwana na wafanyakazi, na kati ya ufalme wa England na falme za Wales, Scotland na Ireland, ambazo kwa pamoja zinaunda Ufalme wa Muungano wa Uingereza (UK). Baada ya miaka mingi ya kupambana na kumwaga damu, na baadhi ya viongozi na wafalme kukatwa vichwa, hatimaye Waingereza walikubaliana kuwa na bunge lenye chemba au mabaraza mawili ili kuzingatia maslahi ya pande zote. Mabaraza hayo ni lile la Mamwinyi (House of Lords) na lile la Makabwela (House of Commons). Wajumbe wa Baraza la Mamwinyi hawachaguliwi na wananchi, na hujumuisha mamwinyi wenye kumiliki ardhi kubwa na viongozi wakuu wa kanisa la Uingereza. Wajumbe wa Baraza la Makabwela huchaguliwa majimboni.

 

Mapambano ya kudai demokrasia nchini Uingereza vilevile yaliibua vyama vikuu viwili, kile cha Conservative (chenye kuwakilisha maslahi ya mamwinyi na mabwanyenye), na kile cha Labour (ambacho awali – siyo sasa - kiliwakilisha maslahi ya matabaka ya wazalishaji – wafanyakazi, vibarua, n.k.). Siku za karibuni, mwaka 1988, kimezuka chama kingine kikuu cha tatu, Liberal Democrats,  ambacho kimetokana na muungano wa vyama vidogo viwili vya Liberal Party naSocial Democratic Party; hicho ni chama cha kiliberali cha mrengo wa kati. Vipo vyama vingine vidogo vidogo lakini havina athari kubwa kiutawala. La muhimu kufahamu kuhusu mfumo huu wa Uingereza ni kwamba vyama vyote vinavyoshika utawala huendeleza takriban sera zilezile za uchumi, utaifa na mambo ya nje, na hakuna hata kimoja kwa sasa kinachowakilisha maslahi ya mnyonge. Jingine la kukumbuka ni kwamba mfalme au malkia wa Uingereza ni nguzo mojawapo ya Bunge la Uingereza, kama alivyo Rais hapa kwetu.

 

Hivyo, madai ya kwamba Tanzania inafuata mfumo wa Westminister yana walakini, maana hayasemi ukweli wote. Hata hivyo, kuna jambo moja la Westminister ambalo Tanzania na nchi nyingi za Jumuiya ya Madola zinaling'ang'ania, nalo ni uwakilishi na utawala kupitia katika vyama. Huu ni utaratibu ulioletwa kwetu na nchi za Magharibi, nasi tukaupokea na kuukubali bila kuusaili. Lakini je, utaratibu huu unahakikisha kuwapo kwa mfumo bora wa uwakilishi wa makundi yote ya wananchi?

 

Jibu ni kwamba utaratibu huu hautuhakikishii uwakilishi wa kweli kwa sababu zifuatazo: Kwanza, wawakilishi wote sharti watoke katika vyama rasmi vya siasa vilivyosajiliwa. Kwa kuwa vyama vinawakilisha itikadi na maslahi ya wanachama wake, hususani viongozi, hatuwezi kudai kuwa aghalabu vinawakilisha itikadi na maslahi ya wananchi. Kwa hakika uzoevu umeonesha kuwa takriban vyama vyote nchini Tanzania vinatetea itikadi ileile ya ubepari na uliberali, hivyo vinawakilisha kundi lile lile la mabwanyenye au wamiliki mali kiuchumi (hata kama katika maandiko yake rasmi vinadai kufuata sera ya "Ujamaa na Kujitegemea", "Nguvu ya Umma" n.k.). Tofauti yao iko katika njia na mbinu zao za kulifikia lengo hilo la ubepari. Haya yanadhihirika tunapoangalia sera na manifesto zao. Hali hii ni tofauti na ile ya Chama cha TANU/CCM kabla ya Azimio la Zanzibar la 1991, ambapo utetezi wa Umma na makundi ya wazalishaji ulikuwa ni nguzo mojawapo ya itikadi, sera na utendaji wa chama-tawala. Kwa ufupi, ukiritimba wa vyama katika siasa unaua demokrasia badala ya kuijenga.

 

Pili, mfumo wetu wa ukiritimba wa vyama unahakikisha kwamba hatuwezi kuwa na wagombea binafsi, ambao labda wangewakilisha makundi yaliyosahaulika, na hatuwezi kuwa na wawakilishi wa kweli wa Umma. Wawakilishi wachache wa sasa wanaojaribu kuutetea Umma aghalabu wanajikuta wakikemewa na hata kuenguliwa na vyama vyao, maana wanaonekana kuwa ni waasi wa tabaka lao au vyama vyao.

 

Uwakilishi wa Majimbo dhidi ya Uwakilishi wa Umma

 

Uwakilishi wa majimbo si uwakilishi wa Umma ndani ya majimbo hayo, bali ni uwakilishi wa kundi au makundi fulani maalumu, ndani ya jimbo, kulingana na itikadi ya chama kinachohusika, na nguvu (ya ushawishi na fedha) ya wapiga kura wanaohusika. Aghalabu makundi hayo yanayowakilishwa na maslahi yao kutetewa ni yale ya tabaka tawala – mabepari, mabwanyeye, mafisadi na matajiri wa aina mbalimbali. Makundi ya wakulima na wafanyakazi huwekwa pembezoni, yaani maslahi yao ya msingi hugusiwa mara chache sana, hasa wahusika wanapohitaji kura zao.

 

Kuongeza majimbo, basi, hakutaimarisha demokrasia kwa maana ya kuimarisha utetezi au sauti ya wanyonge; sana sana kutaimarisha utetezi wa matabaka yaleyale ya wenye mali. Na hilo ndilo lengo kuu lisiloelezwa la mfumo wa Westminster. Ili kurekebisha hali hii tunahitaji kubuni mfumo tofauti wa uwakilishi badala ya kuiga ule wa nchi za Magharibi.

 

Hivyo pamoja na uwakilishi wa majimbo, ambao unawachukulia watu wote katika jimbo kuwa wenye hali, maslahi na malengo sawa, tunahitaji pia uwakilishi wa makundi maalumu ya kijamii. Makundi hayo ni yale yenye maslahi maalumu ya kiuchumi, kijamii, kiitikadi au kitabaka. Hapa tunaweza kuorodhesha machache:

 

1.      Wakulima

2.      Wafugaji

3.      Wavuvi

4.      Wachimba migodi

5.      Wafanyakazi wa viwandani

6.      Wafanyakazi wa serikali

7.      Wafanyakazi wa mashirika

8.      Walimu (wa shule za msingi na sekondari)

9.      Wahadhiri, wakufunzi na maprofesa wa vyuo

10.  Weledi na wataalamu wengine (k.m. madaktari, wahandisi, n.k.)

11.  Askari wa Jeshi la Ulinzi, JKT na Jeshi la Kujenga Uchumi

12.  Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza

13.  Usalama wa Taifa

14.  Walemavu

15.  Wanawake

16.  Vijana

17.  Wasanii

18.  Wazee na wastaafu

19.  Wanafunzi wa msingi na sekondari

20.  Wanafunzi wa vyuo/vyuo vikuu

21.  Vikundi vya kidini – Waislamu, Wakristo, Wanajadi, Wahindu/Wabudha, Wayakinifu (wasioamini), n.k.

22.  Vyama vya ushirika (vya wakulima, wafanya biashara)

23.  Wachuuzi wadogowadogo

24.  Wanyabiashara wa kati (wenye maduka)

25.  Watoa huduma (mahoteli, bima, ushauri, n.k.)

26.  Mabepari/wafanya biashara wakubwa wa viwanda na madini (k.m.  kupitia Chamber of Commerce)

27.  Wakulima wakubwa.

 

Haya ni baadhi tu ya makundi ya kijamii ambayo nimeweza kuyaainisha. Bila shaka yapo mengine. Baadhi ya makundi, k.m. lile la madhehebu ya dini, yatahitaji wawakilishi zaidi ya mmoja – kila dhehebu na mwakilishi/wawakilishi wake, bila kusahau wanajadi, ambao aghalabu huwa wanabaguliwa. Makundi ya wakulima na wafanyakazi nayo yanahitaji wawakilishi wengi; vivyo hivyo kundi la wanawake.

 

Hapa tunazungumzia uwakilishi wa kweli wenye kuzingatia vikundi amali na vikundi maslahi, sio ule wa vyama vya siasa ambao unazingatia maslahi ya kundi moja au mawili tu. Wagombea wa ubunge kupitia makundi ya kijamii wasilazimishwe kupitia au kuungwa mkono na chama chochote cha siasa, na wachaguliwe kidemokrasia ndani ya makundi yao kulingana na taratibu zitakazowekwa.

 

Bunge la sasalina wabunge wengi sana wa kuteuliwa na Rais, wakiwamo mawaziri na wamaziri wadogo. Hali hii inapunguza udhibiti wa Bunge kwa serikali. Aidha, mawaziri ama wanalazimika kupendelea majimbo yao katika mipango ya maendeleo ya wizara zao, ama hawapati nafasi ya kutosha ya kushughulikia matataizo ya majimbo yao. Hivyo inapendekezwa Mawaziri wasiwe wabunge wa kuchaguliwa; wateuliwa na Rais kulingana na sifa zao za kitaaluma na kiutendaji tu.

 

Kama mfumo huu utafuatwa, itawezekana kabisa nusu ya wabunge wote wakawa ni wawakilishi wa makundi-maslahi badala ya vyama vya siasa. Hii ina maana kwamba idadi ya wabunge wa majimbo, na hivyo idadi ya majimbo, itabidi ipunguzwe ili kutoa nafasi kwa wabunge wa makundi. Aidha, wagombea Urais wanaopata asilimia 10 au zaidi ya kura zote wawe ni Wabunge wa Kitaifa ndani ya vyama vyao. Pendekezo langu ni kwa kila wilaya kuwa jimbo moja tu la uchaguzi. Hivyo, kwa wilaya kama 150 zilizopo sasa, tutakuwa na majimbo 150 na wabunge wa vyama wasiozidi 150. Wakiongezwa wabunge wengine kama 100 wa makundi tuliyoyataja, na 50 wa kitaifa na kiwadhifa (k.m. mawaziri), tutakuwa na jumla ya wabunge 300. Wanatosha kabisa.

 

Kuweka Mfumo wa Uwazi wa Utawala na Uongozi, na Kudhibiti Ufisadi

 

Katiba kwa vyovyote itaelezea na kufafanua mfumo wa utawala na uongozi kuanzia ngazi za juu [Rais na Baraza la Mawaziri] hadi zile za chini, mihimili ya dola [Bunge, Mahakama na Serikali] uhusiano wa mihimili hiyo, na mgawanyo wa madaraka kati yao. Hili halina utata sana; la muhimu ni kuweka uwiano mzuri unaofafanua wazi ni chombo kipi ni kikuu zaidi – serikali au Bunge? Hapa tungependekeza utamalaki wa Bunge juu ya mihimili mingine [pasina kuingiliana bila shaka] utiliwe mkazo. Hatimaye, Bunge nalo liwajibike kwa wananchi, ambao ndio waliolichagua.

 

Uzoevu wa miaka ya karibuni unaonesha kuwa uongozi unapochanganywa na ubepari au biashara ya binafsi maslahi ya Umma hutelekezwa kwa minajili ya kuendeleza maslahi ya binafsi. Muungano huu wa siasa na biashara huzaa ufisadi, ukiwamo wizi wa kura au kung'ang'ania madaraka, ambao hatimaye huvuruga na hata kukwamisha maendeleo ya nchi, na hali hiyo isipodhibitiwa huweza kusababisha vurugu, mauaji na hata mapinduzi ya serikali.

 

Hili ni jambo ambalo inabidi lishughulikiwe katika Katiba. Mathalan, Katiba itenganishe biashara na uongozi, itaje itikeli(ethics) za uongozi, na iwe na vifungu vyenye kuwabana wanaoiba au kuchakachua kura [watu binafsi na vyama]. Mimi ningeshauri wizi au uchakajuaji wa kura wakati wa uchaguzi uchukuliwe kuwa kosa la uhaini. Kadhalika, Katiba iweke kikomo cha muda wa uongozi wa ngazi na kada zote za viongozi, siyo kwa Rais tu. Siku hizi nafasi za uongozi zimekuwa ni ajira ya kudumu badala ya kuwa fursa tu ya kuhudumia Umma kwa zamu. Tumefikia hatua ya baadhi ya watu kuandaa mazingira ya kuhakikisha kuwa wao, wake/waume zao, watoto na hata wajukuu zao wanarithishana uongozi. Hivyo ningependekeza wabunge na madiwani waongoze kwa vipindi visivyozidi vitatu kwa mfululizo [yaani miaka 15]. Aidha, kiongozi anayefanya makosa makubwa au ambaye chombo anachokiongoza kinasababisha matatizo yanayotokana na uzembe, ufisadi, uongozi hafifu, n.k. alazimishwe na Katiba kujiuzulu uongozi.

 

Kujenga na Kuimarisha Uchumi na Uzalishaji

 

Hakuna Taifa lolote duniani linaloendelea bila kujenga uchumi na uzalishaji, ambao ni pamoja na kuendeleza kilimo, viwanda, teknolojia, n.k. Hapa inabidi kuwa waangalifu; Katiba ikiruhusu umiliki holela wa njia kuu za uzalishaji kama ardhi , migodi na viwanda vikubwa, ikiizuia serikali kushiriki katika masuala ya "biashara" na "uzalishaji" hata pale ambapo maslahi ya Taifa yanahusika, itakuwa ni kikwazo badala ya kuwa kichocheo na nyenzo ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Katiba sharti iweke uwiano mzuri kati ya uzalishaji holela wa watu au makampuni binafsi na ule unaoongozwa au kusimamiwa au kumilikiwa na serikali kwa manufaa ya nchi. Tusijidanganye: Hata nchi zilizoendelea sana kibepari kama Japan, Marekani na Uingereza bado zina sekta ya Umma. Ni vizuri Katiba ikaainisha maeneo ambayo serikali itawajibika, pekee au kwa ubia, kuyaendesha. Hapa nafikiria maeneo kama miundo-mbinu mikubwa kama ya reli, barabara na usafiri wa meli na ndege, viwanda vikubwa vya msingi [vya chuma, utengenezaji wa mitambo mikubwa, mashine, n.k.], nishati, maji, uhifadhi wa mazingira, elimu, utafiti, na uendelezaji wa teknolojia, na sekta muhimu za utamaduni [kama vile Makumbusho, Makavazi, lugha, fasihi na vitabu], na baadhi ya maeneo ya sekta ya Fedha.

 

Kujenga Umoja na Ushirikiano wa Kikanda na Hatimaye Umajumui wa Afrika Yote

 

Katiba izungumzie, kwa mtazamo chanya, suala la umoja na ushirikiano wa kikanda, na kuweka misingi ya kuiwezesha Tanzania kuunda Shirikisho na nchi nyingine za ukanda huu, na hatimaye kushiriki katika Shirikisho la Afrika Nzima. Msingi huu ulikuwamo katika Katiba ya TANU tangu miaka ya 1950, na ni msingi muhimu tunapofikiria maslahi ya Tanzania na Afrika ya sasa na baadaye. Tutake tusitake, usalama wa Tanzania kama Taifa na nchi umefungamana na hatima ya ukanda huu na bara zima la Afrika.

 

Hivyo Katiba mpya itaje suala la Shirikisho na Umajumui wa Afrika kama lengo na dira mojawapo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

MUHTASARI WA MAPENDEKEZO

 

Ili kutekeleza mawazo tulioyoyaeleza hapo juu, tunapendekeza:

 

1.      Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibadilishwe ili iwe na mtazamo mpya usiokuwa wa ki-Westminster;

2.      Katiba itaje alama zote za Utambulisho wa Utaifa wa Mtanzania, ambazo ni pamoja na lugha ya Taifa – Kiswahili.

3.      Katiba ikatae Uraia wa Nchi Mbili.

4.      Majimbo ya ubunge na udiwani yapunguzwe; kila wilaya iwe ni jimbo moja tu la ubunge (kwa upande wa Zanzibar itabidi mfumo wa wilaya urekebishwe kwa kuzingatia hali hii mpya). Uwakilishi zaidi utokane na vikundi vya kijamii tulivyovitaja.

5.      Chama kinachopata angalao 50% ya wabunge wote wa majimbo kiunde serikali; kama hakuna chama kilichopata 50% ya wabunge, iundwe serikali ya mseto;

6.      Mawaziri wasiwe wabunge wa majimbo; waingie Bungeni kwa sababu ya nyadhifa zao tu, na wathibitishwe na Bunge;

7.      Mawaziri na wabunge wengine wa kiwadhifa wasiwe na haki ya kupiga kura wakati bunge linapofanya maamuzi;

8.      Pasiwe na wabunge wa kuteuliwa na Rais au chombo kingine, isipokuwa wale wa kiwadhifa.

9.      Wagombea Urais wanaopata 10% au zaidi ya kura zote wawe Wabunge wa Kitaifa papo hapo.

10.  Mbunge/Diwani ashikilie wadhifa huo kwa vipindi vitatu tu vya mfululizo. Anaweza kugombea tena baada ya kukaa nje ya Bunge/Baraza kwa angalao kipindi kimoja.

11.  Wakuu wa wilaya wachaguliwe na wananchi wa wilaya zao kwa kura ya siri kupitia katika vyama vya siasa, na wawajibike kwa wananchi hao.

12.  Katiba iweke kanuni ya uwiano wa kijinsia katika uwakilishi.

13.  Mamlaka ya Rais, ambayo kwa sasa ni makubwa mno na hayasailiwi popote, yapunguzwe. Mathalan, Baraza la Mawaziri lithibitishwe na Bunge, watendaji wakuu wa asasi na mashirika ya Umma wateuliwe na Mabaraza au Halmashauri za mashirika hayo, na Katiba iruhusu Rais kushitakiwa kwa makosa anayoyafanya [aweze kushitakiwa akiwa bado na wadhifa huo au baada ya kustaafu].

14.  Katiba isitaje Mungu au Miungu yoyote katika kifungu chochote, bali itoe tu uhuru wa kuabudu.

15.  Haki ya kufanya kazi, na stahiki ya pensheni na mafao ya haki kwa wastaafu iingizwe katika Katiba.

16.  Mgawanyo wa mikoa na wilaya usifanywe na Rais au serikali peke yake, bali upendekezwe na serikali na kuthibitishwa na Bunge.

17.  Mgawanyo wa Majimbo ya Uchaguzi upendekezwe na Tume ya Uchaguzi na kuthibitishwa na Bunge. Hii itaepusha mwenendo tunaouona sasa wa watu maalumu kuundiwa majimbo ya ubunge au udiwani.

18.  Mwanasheria Mkuu wa serikali apendekezwe na Rais na kuthibitishwa na Bunge.

19.  Pawe na Tume Huru ya Uchaguzi na isiteuliwe na Rais bali iteuliwe na Bunge kwa kuzingatia Sheria itakayotungwa kwa ajili hiyo.

20.  Pawe na Tume Huru ya kushughulikia maslahi na mafao ya viongozi wakuu, wakiwamo Wabunge. Maamuzi ya Tume hiyo yaheshimiwa na Bunge na Serikali. Hii itapunguza mwanya wa viongozi na wansiasa kujilipa mafao na marupurupu yalisiyolingana na hali ya uchumi wa nchi.

21.  Katiba itaje mji mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuondoa utata uliopo sasa ambapo Dodoma inashindana na Dar es Salaam kubeba majukumu ya "mji mkuu" na hivyo kutoa mwanya kwa warasimu na mafisadi kuitumia hali hiyo tata kwa manufaa yao.

22.  Azma ya kuleta Shirikisho la Afrika Mashariki na hatimaye lile la Afrika iwemo katika Katiba.

 

Naamini kuwa utaratibu wa aina hii, iwapo utatekelezwa, utahakikisha uwakilishi halisi zaidi wa wananchi, maana wawakilishi watatokana na wananchi wenyewe katika makundi yao ya kikazi na kimaslahi. Hivyo utetezi utakuwa ni wa dhati, mawaziri watawajibika kwa Bunge la Umma, na ukiritimba wa vyama hautakuwapo.

 

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment