Monday 28 January 2013

[wanabidii] Kinana: Serikali iwasikilize wananchi wa Mtwara

SAKATA la gesi sasa limeingia hatua mpya, baada ya watendaji wakuu wa CCM; Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kuitaka Serikali ikae na wana-Mtwara ili kuona namna ya kumaliza mgogoro huo kwa amani.

Kinana na Nape walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti jana. Wakati Kinana alisema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara mkoani Kigoma, Nape alifanya hivyo kupitia mtandaowa Twitter na baadaye kuthibitisha kauli hiyo alipoulizwa na mwandishi wetu.

Wakati watendaji hao wa CCM wakitoa matamko hayo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alifanya vikao mfululizo mkoani Mtwara akisaka suluhu ya mgogoro huo.

Kinana na Nape
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Ofisi za CCM Wilaya ya Uvinza, Kigoma, Kinana aliitaka Serikali isikilize hoja za wakazi wa Mtwara na kuzitafutia usumbufu sahihi.

Mbali na kutoa ushauri huo, aliitaka pia Serikali kuwasaka watu wanaochochea mgogoro huo kwa kufanya vurugu na kuharibu mali za watu na kuwafikisha mbele ya sheria.
"Serikali ikae na wana-Mtwara na kuwasikiliza, wananchi hao wana hoja na Serikali inapaswa kutoa majibu sahihi kwa hoja hizo. Lakini pia iwasake na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha uvunjifu wa amani," alisema Kinana.

Kwa upande wake, Nnauye aliitaka Serikali kuwasikiliza wananchi wa Mtwara kwa kuwa madai yao ni ya msingi... "Wakazi wa Mtwara na Lindi wanazo hoja za msingi juu ya suala la gesi, hoja ambazo ni muhimu kusikilizwa na kupatiwa majibu sahihi."

Nape alisema hoja za wakazi hao ni za msingi lakini akaongeza kuwa kuna baadhi ya wahuni ambao wanatumia mwanya huo kupora na kuharibu mali za watu. "Kuna uhusiano gani kati ya hoja yao ya madai ya gesi na kuchoma nyumba za watu, kuharibu mali za umma na magari ya watu. Kuna kundi la wahuni ambalo Serikali inatakiwa kuhakikisha inapambana nalo na kuwachukulia hatua kali za kisheria," alisema Nape.

Pinda asaka suluhu
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alikuwa na kibarua kizito kusaka suluhu ya mgogoro wa gesi baada ya kuzungumza na makundi mbalimbali ya kijamii kupata mawazo yao.

Pinda aliyeongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja alianza kazi hiyo juzi kwa kufanya vikao vya ndani na viongozi wa Serikali mkoa wa Mtwara. Habari kutoka Mtwara zinaeleza kuwa kutwa nzima ya jana, Waziri Mkuu Pinda alikuwa akifanya mikutano mbalimbali na makundi kadhaa kwa lengo la kupata suluhu ya mgogoro huo wa gesi.

"Alianza kwa kufanya mazungumzo ya ndani na viongozi wa dini, wanaharakati, wanasiasa na baadaye viongozi wa Serikali za Mitaa," kilieleza chanzo cha habari kutoka Mtwara.
Mbali na viongozi hao, Pinda pia alizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa CCM na madiwani kabla ya mkutano wake na waandishi wa habari aliopanga kuufanya baadaye jioni.
Mmoja wa madiwani waliohudhuria mkutano huo wa Pinda alilieleza gazeti hili kuwa, Waziri Mkuu aliwaambia kuwa mkutano wake huo ni kwa ajili ya kukusanya maoni.

"Amesema amekuja kukusanya maoni na baadaye atakwenda kushauriana na Rais Jakaya Kikwete na atatoa tamko kuhusu hatima ya suala hilo baadaye," alisema diwani huyo akimnukuu Waziri Mkuu Pinda.

Gesi kuteka Bunge
Mkutano wa Kumi wa Bunge unaanza leo mjini Dodoma, huku suala la gesi likitarajiwa kutawala mijadala mbalimbali ya wabunge.

Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa ni miongoni mwa wabunge waliotangaza mapema kuwa watazungumzia suala hilo bungeni. Mnyaa alisema anakusudia kuwasilisha hoja binafsi za maombi ya wakazi wa Mtwara kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.

Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Mawasiliano ya Bunge, Deogratius Igidio aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa shughuli zote zitakazofanyika ndani ya ukumbi huo zitajulikana leo baada ya Kikao cha Kamati ya Uongozi.Katika kipindi cha wiki nne sasa kumekuwa na maandamano, malumbano na vitendo vya ghasia kuhusiana na mradi wa kujenga bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam hatua ambayo inapingwa na wananchi wa eneo hilo ambao wanadai kuwa wamesahauliwa katika miradi ya maendeleo.

Wananchi hao wa Mtwara wanataka kusitishwa kwa mpango wa kusafirisha gesi hiyo kwa madai kuwa, eneo la Mtwara halijaendelezwa na mara zote Serikali haijaweka vipaumbele kwa ajili ya kusukuma mbele eneo hilo.

Wanataka uendelezwaji wa gesi hiyo ufanywe mkoani humo kwa madai kuwa utasaidia kuchochea shughuli za maendeleo na kuufanya uanze kuinuka kiuchumi.

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye pia ni mwenyeji wa mkoa huo ametoa wito wa pande zote kukutana na kujadiliana ili kumaliza mvutano huo akisema ni jambo la kufedhehesha na kusikitisha kuona wananchi wakianzisha maandamano na kupinga mradi huo wa Serikali.

Chadema hakitaki
Chadema kimeitaka Serikali kusitisha mpango wa kusafirisha gesi iliyogunduliwa mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam mpaka itakapokutana na wananchi na kufikia maridhiano kwa pamoja.

Chama hicho pia kimeitaka Serikali iweke wazi mikataba yote 26 ya kampuni ilizoingia nayo kwa ajili ya kuchimba nishati hiyo ili wananchi waweze kuijua.

Mwenyekiti Freeman Mbowe alitoa wito huo jana alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa Baraza Kuu la chama hicho, Dar es Salaam... "Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakiuliza Chadema nini kauli yenu kuhusu mgogoro huo na kutaka kujua tuko na wananchi au Serikali? Chadema iko nyuma ya wananchi," alisema Mbowe na kuongeza:

"Serikali iache kufanya kazi ikiwa Dar es Salaam iende kwa wananchi na kuzungumza nao na wakikubaliana kwa pamoja ndipo mradi huo utekelezwe."
Habari hii imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Kigoma; Ibrahim Yamola, Dar na Habel Chidawali na Ibrahim Bakari, Dodoma. 
Fred 
MATURITY does not come with age, it begins with acceptance of Responsibility
Change is Essence to maturation 

0 comments:

Post a Comment