Tuesday 29 January 2013

[wanabidii] HIVI MCHAKATO WA VAZI LA TAIFA ULIISHIA WAPI?

Samahani, najua sasa hivi mjadala ulioshika kasi ni wa GESI YA MTWARA. Pamoja na hayo, tunapaswa kukumbuka kwamba nchi hii ina mauzauza mengi ambayo hatuna budi kuyajadili.
**********************************************************************

WAKATI nchi ikikabiliwa na matatizo mengi makubwa na mazito, serikali kwa kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ilizua mjadala usiokuwa na tija yoyote kwa wananchi hususani walalahoi – mjadala wa kutafuta vazi la taifa!
Mjadala huu haukuwa na tija yoyote kwa Watanzania, ukiondoa watu wachache ambao hawana mipango yoyote ya maana kwa jamii.  Hawa ni watu ambao wana fursa za kila siku kwenda Ulaya na sehemu nyingine duniani ambapo wanachokitaka ni kujulikana wanatoka Tanzania!
Ni aibu kwamba wakati kama huu ambapo serikali ingekuwa inaendesha mijadala muhimu kama  kuandikwa kwa katiba mpya, inakubali watu kupoteza muda na raslimali kwa ajili ya kujadili magauni na mashati ambayo Watanzania wanatakiwa wayavae wakiwa ndani au nje ya nchi hii.
Kwa kifupi, hivi tunatafuta vazi la taifa ili iweje?  Na tukishalipata vazi la taifa na kuanza kulivaa litatuongezea chumvi kwenye mboga au sukari kwenye chai?

Hebu tukae chini na kufikiria kama walimwengu wenzetu. Tuchukue mfano wa nchi zilizoendelea duniani kama vile Marekani, Canada, Japan, Ujerumani, Italia, Afrika Kusini, na kadhalika.

Je, nchi gani miongoni mwa hizi zina vazi rasmi la taifa?  Au, je, ni lini ziliwahi kukaa na kupoteza muda kujadili vazi la taifa?

Kwa nini Watanzania tusiutumie muda wetu wa masaa 24 ya siku moja kujadili ukosefu wa maji ya kunywa katika sehemu kubwa ya nchi hii?  Kwa nini tusianzishe mijadala angalau ya kurudisha uhai wa Reli ya Kati ambayo inabidi iwahudumie mamilioni ya watu nchini?

Nani aliwahi kusema vazi la taifa huja kwa kujadiliwa kwenye vikao?  Nani aliwahi kusema, kwa mfano, mtindo wa muziki hujadiliwa kwenye vipindi vya radio na televisheni?  

Hivi mtindo kama "Ndombolo" wa Congo na "Kwaito" wa Afrika Kusini ilijadiliwa kwenye vijiwe vya Kinshasa na Cape Town?

Mitindo hiyo ya muziki ilikuja yenyewe.  Haikujadiliwa vijiweni au redioni!

Vivyo hivyo, mitindo ya uvaaji wa watu wa Afrika Magharibi, kama vile Nigeria, Ivory Coast, Guinea, Mali, na kadhalika, ilikuja yenyewe. Hakuna vikao vilivyofanyika na kupendekeza aina hiyo ya uvaaji.

Kwa nini tunashindwa kuelewa ukweli huo mdogo ambao hata watoto wa shule za msingi wanaufahamu?

Kuna wakati wapenda muziki walikaa na kuamua eti mtindo wa dansi nchini uitwe "Achimenengule"!  Kilichofuata ni kwamba uamuzi huo uliishia kwenye meza walizokuwa wamezikalia wakati wa majadiliano hayo.

Hapakuwa na "Achimenengule" wala nini hadi leo!  
Mtindo wa mavazi au kitu chochote huwa havipangwi, hujitokeza vyenyewe kwa kukubalika kimyakimya kwa watu – si kwa kutangazwa!

Hivi hatuna kitu cha maana cha kujadili kwa manufaa ya watu wengi? Kwa nini Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni inakubali kujishusha kiasi hicho wakati majuzi tu ilishindwa kuisafirisha timu ya wanawake ya taifa ya soka kwenda Namibia wakati kila mwaka inapewa bajeti nono na bunge?

Iwapo tatizo ni Watanzania kutaka kujulikana nje ya nchi, basi dawa yake ni ndogo sana.  Mtanzania anayetaka kujulikana akiwa nje ya nchi hii ni kuvaa nguo yoyote na akaiandika kwa maandishi makubwa sehemu yoyote, kwa mfano: "I am a Tanzanian" (kwa Kiingereza), "Je suis un Tanzanien" (Kifaransa)  au "Yo soy on tanzano" (Kihispania).
Yote hayo yanamaanisha kwamba: "Mimi ni Mtanzania".
Hiyo inatosha kabisa kuwafanya watu wakufahamu kwamba unatoka katika nchi mojawapo za bara maskini la Afrika.  Inatosha!  

Huna haja ya kuchora picha ya twiga au mlima Kilimanjaro kwani twiga ni wengi sana duniani achilia mbali milima mirefu zaidi ya Kilimanjaro.

Hata hivyo, kwa kifupi kabisa: Watu waliopania kwamba Tanzania lazima iwe na vazi la taifa ambalo litawatambulisha wakiwa ndani na nje ya nchi hii, wasipoteze muda kulitafuta – watumie mavazi ya Kimasai!

Ni mavazi yenye kuvutia na ni ya kipekee ambayo Mtanzania akivaa nje ya nchi hii ni hakika watu watamshangaa na kumfurahia.

Kama vazi hili watu hawalitaki basi ni heri tujadili jinsi ya kuzipatia shule za sekondari za kata kompyuta, tujadili jinsi ya kusomesha na kuwalinda maalbino nchini, tujadili jinsi ya kupunguza bei za betri za radio ili mamilioni ya maskini nchini waweze kuzitumia kirahisi kwa radio na tochi zao.

Kujadili mashati na magauni ya kuvaa wakati tuko kwenye ndege tukielekea Ulaya au wakati tuko kwenye semina za kujadili posho ni kupoteza wakati na raslimali za taifa bure.
Hivi Watanzania hatuna cha maana cha kufanya kwa ajili yetu na wajukuu zetu?

0 comments:

Post a Comment