Monday 28 January 2013

[wanabidii] Hassani Samli : zinazoendelea Lindi, Mtwara, kamwe siyo siasa

KAMWE HAIWEZI KUWA SIASA!

Nisingependa kuendelea kusikia kuhusu vurugu zinazoendelea katika Mikoa ya Kusini hasa Mtwara na Lindi ikibezwa kwa kuitwa ni siasa na kwamba zinachochewa na wanasiasa katika kujitafutia umaarufu. Sipendi mtazamo huu kuendelea kupandikizwa vichwani mwa watu hasa wale ambao wako nje maneo ya matukio hayo. 

Pia sipendi propaganda hii kwa sababu ni miongoni mwa kauli ambazo zimeufikisha mgogoro huu hapa ulipo. 

Na kama ni sahihi kwamba wale wanaotoa kauli hizi hutoa kutokana na hisia za ndani ya mioyo yao kwamba ni sahihi, basi ni hatari.

Ni hatari kwa maana kwamba, kama ni kweli wanajiaminisha hivyo isije badala ya kutafuta suluhisho hasa la mgogoro huu isije wakajipanga kuleta MAKATIBU WA ITIKADI NA UENEZI WA CHAMA ili kuja kukabiliana kisiasa. Maana unaposema WASIASA WANAJITAFUTIA UMAARUFU watu pekee wenye uwezo wa kukabiliana na hali hiyo ni wataalamu wa ITIKADI na UENEZI na si vinginevyo, kitu ambacho sidhani kama itakuwa ni sahihi kulingana na uhalisia wa mgogoro huu.

Nadiriki kusema haya kwa kuona mitazamo hiyo bado ikiendelea kutolewa katika kauli mbalimbali za watawala wetu. Kumejitokeza msuguano baina ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini (George Simbachawene) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Zitto Kabwe) juu ya kauli ya Naibu Waziri huyo kumshutumu Zitto Kabwe kwa kuhusika kwake katika uchochezi wa mgogoro huu.  Naibu huyo anadaiwa kutoa kauli hiyo siku ya Jumamosi tarehe 26/01/2012 alipokuwa akiongea na Wahariri.

Napingana na mitazamo hii kwa sababu, Watawala hawa wamesahau kukumbuka kwamba baadhi ya kauli zao za hapo kabla za kuwaminisha Wananchi wa Mikoa hii juu ya ujenzi wa mitambo ya uzalishaji umeme, viwanda vya saruji, plastiki na kadhalika kwamba bado hotuba hizi na ahadi hizi zinaendelea kukumbukwa na kuwepo vichwani mwa watu? Je wanasahau hata maandiko yaliko katika ILANI YA UCHAGUZI WA CCM 2010 juu ya suala la gesi? Je! Matamko ya Viongozi wa Dini (KIISLAMU na KIKRISTU), na Taasisi za Kiraia na hata za baadhi ya Vigogo wa Ndani ya CCM akiwemo Mh. Nimrodi Mkono na Mzee Malechela, hizi zote ni siasa au ni kauli za kujitafutia umaarufu wa kisiasa?

Tamko la Makanisa ya PCT Mtwara iliyotolewa leo tarehe 27/01/2013 na kusainiwa na Bishop C. Chilumba na Pastor Selekwa imeanisha waziwzi vipengele vinavyowapa Wananchi wa Mikoa hii uhalali wa maandamano na madai yao. Mfano; Taarifa hiyo inasema "Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010 anatamka wazi katika Ibara ya 63 kifungu cha H na K juu ya gesi ya Mnazi Bay Mtwara na Songosongo Kilwa, Lindi". Kwamba "Umeme wa (240 MW) Kinyerezi na (300 MW) Umeme wa Mnazi Bay Mtwara". Vifungu hivi vinafafnua kwamba: "Gesi ya Mnazi Bay itakuwa kwa ajili ya Mitambo ya kuzalisha umeme ambayo itajengwa Mtwara (300 MW), Mitambo ya kuchakata gesi itajengwa Mtwara, Ujenzi wa viwanda Mtwara ili malighafi itokanayo na gesi itumike kutengeneza mbolea, plastic vikiwemo na viwanda vya Cementi. Gesi ya Songososngo inafafanua wazi kuwa gesi hiyo itapelekwa Kinyerezi Dar es salaam kwa madhumuni hayohayo".  Tamko hilo pia limenukuu baadhi ya ahadi za Raisi Kikwete alizozitoa tarehe 29/10/2010 juu ya gesi hiyo.

Ikumbukwe pia kuwa ni wajibu na haki ya Kisheria kwa vyama vya siasa kuihabarisha jamii juu ya MAOVU na mambo mbalimbali ya Kiserikali na hivyo wajibu wa raia ni kuchambua ukweli na uhalisia wa mambo hayo. Je unapokemea vyama vya siasa kuyafanya hayo ni chombo gani tena kinaweza kusimama badala ya raia? Je! Tangu wanasiasa hao KUENEZA UZUSHI kama mnavyodai, nyie kama Watendaji wa Kiserikali mlishathubutu kuja hadharani kukanusha uzushi huo mbali na kutoa matamko hayo kupitia kwenye vyombo vya habari?

Naomba tusiwe waoga, tusiwe waoga kwasababu tunastahili na tunawajibika kutoa majibu ya maswali ambayo Wananchi wanayauliza. Mnapaswa kutoa majibu, tena majibu yenye mantiki na si kama yale yakusema "GESI YENYEWE MTWARA NI KIDOGO TU" au "WANAODAI GESI ISITOKE NI MTWARA MJINI NA SI VIJIJINI AMBAKO GESI HIYO IPO" au "WENYEWE WA MSIMBATI WAMEKUBALI GESI HIYO ITOKE" au "MSIMBATI UMEME WAMEPEWA BURE" au pengine "GESI IKO 'DEEP SEA'" na hivyo si mali ya Wanamtwara ni mali ya Taifa.

Ni wajibu wa viongozi wanaokuja sasa Mtwara kwa nia ya kutatua mgogoro huu kuyatafakari mambo haya kwa umakini na kutafuta majibu. Uwepo wa Waziri Mkuu uwe ni mwanzo wa utoaji wa majibu sahihi kwa Wanannchi na si porojo tunazoendelea kuzisikia.

Hebu tujaribuni kupitia na kutafakari kwa kina hoja za Wananchi ili tuweze kupata kufahamu upana wa hoja lakini pia majibu yanayofaa angalau kutuliza jazba za Wananchi hawa badala ya kuanza kunyoosheana vidole ya ni nani anahusika kuchochea vurugu. Kwani isije tukatafuta majibu ya Kisiasa kama yaliyotewa hapo kabla wakati vichwa vya watu havihitaji kabisa kusikia maneno yenye muelekeo wa kisiasa isije tukaendeleza mgogoro badala ya kuumaliza. 

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Wabariki Watanzania.

Hassani Samli,
Mtwara
+255717340671
samlihassani@yahoo.com

Source: http://www.wavuti.com/4/previous/2.html#ixzz2JJKAOgRk

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
International Jobs - www.jobsunited.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Wanabidii" group.
To unsubscribe from this group, send email to wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com.
For more options, visit https://groups.google.com/groups/opt_out.
 
 

0 comments:

Post a Comment