Wednesday 23 January 2013

[wanabidii] HAIBA YA KINANA NA CCM

Hivi karibuni kampuni ambayo kati ya wamiliki wake ni Abrahaman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, ilihusika na usafirishaji wa pembe za ndovu kinyume na sheria za nchi, kinyume na sheria za kimataifa.
 
Vyombo vya habari viliripoti kuwa Kinana mwenyewe alikiri kuwa kampuni yake ilihusika na usafirishaji wa shehena hiyo haramu lakini kampuni haikujua kuwa shehena ile ilikuwa ya biashara haramu.
 
Kwa mtazamo mpana, kashfa hii na utetezi wa Kinana, kweli unatosha kumsafisha kiongozi mkuu huyu wa chama tawala na kashfa hii? Hivi kampuni wakala wa usafirishaji mizigo husafirisha mzigo wowote bila ya kujiridhisha kuwa mzigo unaosafirishwa ni mzigo uliotajwa kwenye nyaraka za usafirishaji? Mara nyingi katika biashara, mtoa huduma huwa na wateja wake wa muda mrefu na wale wa mara moja. Kutokana na kushamiri kwa biashara haramu ya pembe za ndovu, Je, kampuni hii ya usafirishaji wa bidhaa haramu inayomhusisha kiongozi mkubwa wa chama tawala, imesafirisha mizigo ya aina hii mara ngapi bila ya kukamatwa? Wamiliki wa mizigo hiyo haramu waliichagua kampuni ya mheshimiwa huyu kwa bahati mbaya au kulikuwa na sababu maalum ya kuichagua kampuni hii?
 
Swali jingine la kujiuliza, kumiliki kampuni inayosafirisha bidhaa haramu, japo inawezekana Kinana ni mmiliki tu wa kampuni na asiwe mtendaji wa kila siku wa shughuli za kampuni, je, hiyo pekee yake inaweza kuwa ni sababu tosha ya kumwona Mh. Kinana ana usafi wa kuongoza chama ambacho kinadai kipo kwenye hatua ya kujisafisha?
 
CCM kama chama cha siasa na chama tawala, kinapojiangalia kwenye kioo cha kujitathmini kinajiona ni chama cha namna gani, wakati viongozi wake wakuu majina yao yanatajwatajwa kwenye biashara chafu? Kwenye mambo kama haya, ndipo tunaposhangaa umakini wa CCM.
 
Bart

0 comments:

Post a Comment