Saturday 15 December 2012

[wanabidii] UNYONYAJI WA KUJITAKIA!

 
Ukitembelea mitaa ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam, nyakati za mchana utakuta vijana wengi wameketi na kompyuta zao juu ya meza wakidurufu kazi za wasanii mbalimbali, wa sasa na wa enzi hizo, bila hofu yoyote. Mbali na Kariakoo, shughuli hii hufanyika karibu kila mahali jijini Dar es Salaam na katika miji mingine ya Tanzania. Wala huhitaji kutumia nguvu nyingi kuwatafuta na kuwakamata watu hawa. Wanaonekana kabisa tena mchana kweupe! Tatizo ni kwamba hawa vijana wamekuwa wakifanya wizi huu kwa uhuru kabisa na bila bugudha yoyote hadi huo uharamia wao (plagiarism) wanaoufanya wanauona kama ni jambo la kawaida.
 
Siku zote wasanii wa muziki, maigizo, filamu na tamthlia wamekuwa wakilia 'njaa' wakati kazi zao zikiibiwa kirahisi namna hii. Utakuta mtu yupo kwenye gemu kwa muda mrefu lakini hatoki. Kumbe kuna mchwa wameketi kivulini mahali fulani wanakula jasho la wasanii kiulaini kabisa! Ukuaji wa teknolojia nao umerahisisha wizi wa kazi za wasanii, na hivyo kuendelea kuwadidimiza zaidi kiuchumi. Siku hizi ni rahisi sana kunakili, kutunza na kusafirisha kazi za wasanii kuliko ilivyokuwa zamani. Matokeo yake, mawakala na maharamia wa kazi za wasanii wamekuwa wakinuifaika zaidi kuliko hata wasaanii wenyewe wanaoumiza vichwa kutengeneza hizo kazi.
 
Wezi wanaodurufu kazi za wasanii na kuziuza kwa bei ya chini hawawatendei haki wasanii wa kazi husika. Kwanza, wanawanyonya na kuwafanya wasitoke kiuchumi na kimaisha. Pili, wanachangia kufifisha ubora wa bidhaa zenyewe kwa kuwa kazi iliyodurufishwa (counterfeit copy) ina ubora wa chini ukilinganisha na kazi ya awali (original copy). Jambo la kushangaza ni kwamba wizi huu umekuwa ukifanyika bila kificho, mchana kweupe, huku wanaoibiwa wakiona na wamekaa kimya! Na cha ajabu zaidi, hata chombo kinachosimamia kazi za wasanii, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), ambacho kinapaswa kuhakikisha kwamba wasanii wananufaika na jasho la kazi zao, nacho pia kimekaa kimya.
 
Si BASATA wala wasanii wenyewe, wanaojihangaisha kuchukua hatua za makusudi kukomesha wizi huu! Kama wasanii wenyewe wana ubia na hawa wezi, hilo ni swala jingine. Kama ndivyo, na kama nao wananufaika na vitendo hivi, basi sipaswi kuwaita wezi bali wabia. Pamoja na hayo, mimi nitaendelea kuwaita hawa watu kwamba ni wezi/wanyonyaji mpaka hapo nitakopojiridhisha vinginevyo. Kama ni kosa kuwaita hivyo, basi niko tayari kuhukumiwa kwa hilo. Ninapata jeuri hiyo kutokana na ukweli kwamba hata wasanii wenyewe wamekuwa wakilalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sasa.
 
Nina wasiwasi kama kuna sheria inayokataza wizi wa kunakili kazi za wengine. Kama  ipo basi itakuwa haifanyi kazi kabisa au haina meno ya kutosha kudhibiti wizi huu. Ni kawaida kusikia wasanii wakilalamikia kuibiwa na kudhulumiwa kazi zao kwa njia hii lakini ni nadra sana kuwaona wakichukua hatua madhubuti kuzuia uharamia huu. Katika siku za nyuma niliwahi kumuona promota mmoja wa wasanii wa miziki ya injili, Bw. Alex Masama, akipita madukani na kukamata kazi zilizodurufiwa. Alifanya kazi nzuri lakini sijui juhudi zake ziliishia wapi tena.
 
Sasa tuanze kuiona sanaa kama kazi nyingine na tuipe heshima inayostahili. Kwa upande wake, Serikali nayo itambue umuhimu wa sanaa na mchango wake katika kukabili tatizo la ukosefu wa ajira nchini. Sheria zenye meno zitungwe ili kudhibiti wezi wa kazi za wasanii. Na wasanii wapewe mikopo ya kuendelezea kazi zao badala ya kuwategemea wafadhili na mawakala (wadosi), ambao wapo kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi kuliko wasanii wanaovuja jasho. Pia na wasanii wenyewe waamke, waingie mitaani na kuwasaka wezi wa kazi zao. Wasiketi chini na kuanza kulalamika kuhusu kuibiwa bila kuchukua hatua zozote za kukomesha wizi wa kazi za mikono yao.
 
   
 

0 comments:

Post a Comment