Monday 24 December 2012

[wanabidii] Re: KAFUMU AKATA RUFANI - AIBU NYINGINE KWA CCM

KAFUMU AKATA RUFANI

Simba aliliambia NIPASHE kuwa rufaa ya Dk. Kafumu ilikatwa kupitia Wakili wake, Kamaliza Kayaga, takriban wiki tatu zilizopita, na tayari taarifa kuhusu rufaa hiyo zimekwisha andaliwa kwa ajili ya kupelekwa Mahakama ya Rufani ili kupangiwa tarehe ya kusikilizwa.

"Wameshafaili na kulipia kila kitu. Notisi (taarifa) zao zimekwisha andaliwa. Tunasubiri kupeleka Mahakama ya Rufaa, ambayo ndiyo itapanga taratibu lini vikao vitafanyika," alisema Simba. 

Uamuzi uliotengua ubunge wa Dk. Kafumu ulitolewa na Jaji wa mahakama hiyo, Mary Shangali, Agosti, mwaka huu, baada ya kuridhika na pingamizi la mlalamikaji katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo, uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Shangali alisema kuwa Mahakama imeridhika na hoja saba za upande wa mlalamikaji, ambazo alisema zinathibitisha na kuonyesha kuwa uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Igunga haukuwa huru na haki.

Alizitaja baadhi ya kasoro zilizosababisha kutenguliwa kwa matokeo ya uchaguzi huo ni pamoja na ahadi iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi,  Dk. John Magufuli, kuhusu ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo wakati wa kampeni alidai kwamba kama wananchi hawataichagua CCM, daraja hilo halitajengwa. Waziri huyo alitoa ahadi hiyo katika kipindi hicho ambacho kulikuwa na shida kubwa ya usafiri katika eneo hilo.

Jaji Shangali alisema kuwa pia Waziri Magufuli alitumia nguvu  na kuwatisha wapiga kura kwamba kama hawatamchagua mgombea wa CCM, watawekwa ndani, kitu ambacho alisema kilitishia uchaguzi huo kuwa huru na wa haki.

Jaji Shangali alisema kitendo kilichofanywa na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM), kwamba mgombea wa Chadema amejitoa katika uchaguzi huo, hakikuwa cha kiungwana kwani alitumia lugha ya uongo kwa lengo la kupotosha wapiga kura.

Alisema pia Rage alihusika katika vitendo vya kujenga hofu kwa wapiga kura baada ya kupanda jukwaani na bastola, hali ambayo iliwafanya wapiga kura kuhofia na hivyo kuleta dosari katika uchaguzi huo. Jaji alisema kuwa hoja hiyo imezingatiwa na Mahakama.

Jaji huyo alioonyesha kusikitishwa na kitendo kilichofanywa na Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Igunga, Sheikh Swaleh Mohamed, kutangaza msikitini akiwataka waumini wa dini ya Kiislamu wasikichague Chadema kwa madai kuwa viongozi wake walihusika kumdhalilisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario.

Kadhalika, Jaji Shangali aliithibitisha kuwa kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kuwa Chadema kimeingiza makomandoo katika wilaya ya Igunga kwa lengo la kuvuruga uchaguzi huo mdogo, ilikuwa na madhumuni ya kupeleka vitisho kwa wananchi.

Kuhusu madai ya kugawa chakula wakati wa kampeni, Jaji Shangali alisema kitendo cha serikali kugawa mahindi ya msaada kwa wakazi wa Igunga katika kipindi cha kampeni kimeleta fedheha kubwa kwa wapiga kura. Alihoji, je; ni nani aliyekufa njaa katika kipindi hicho na kwamba kulikuwa na umuhimu gani kugawa mahindi katika kipindi cha kampeni?

Kesi hiyo ilifunguliwa na Kashindye, ambaye aliwakilishwa na wakili maarufu nchini, Profesa Abdallah Safari, akipinga matokeo ya uchaguzi huo kwa kulalamikia ukiukaji wa sheria ya uchaguzi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment