Thursday 13 December 2012

[wanabidii] Mama wa Kikurya aua jambazi kwa shaba


Juzi kwenye blogu ya Michuzi kulikuwa na habari ya mama wa miaka 61 wa kikurya mkazi wa Bagamoyo aitwaye Mwajuma Marwa Magaina ambaye alifanikiwa kupambana na majambazi kumi yaliyokuwa na bunduki na kuliua moja kwa bastola yake usiku wa manane akiwa peke yake na wanae/wajukuu waliokuwa wamejifungua vyumbani.
 
Mama huyo alihojiwa na video yake kubandikwa kwenye blogu huku akizungumza Kiswahili chenye lafudhi ya kikurya safi na papo hapo kuweka Kimombo kila ilipobidi. Mama Mwajuma Marwa ambaye wengine wanamwita "bibi" alielezea jinsi mkasa huo ulivyomkuta kwenye nyumba yake ya kisasa, kwamba walikuja majambazi anaodhani walikuwa kama kumi hivi kwa kuwa alikuwa akipambana nao madirishani na mlangoni. Majambazi yalianza kuvunja mlango wa nondo na yeye akayatupia risasi za bastola yake na ndipo yaliponza kumtupia risasi za bunduki huku zikipita mlangoni na madirishani na yeye akihaha sebuleni huku akijibu mpaka alipoishiwa magazini ya kwanza ya risasi kumi.
 
Mama Mwajuma Marwa alieweka magazini ya pili na akashambulia tena kwa kupitia dirishani kabla ya kuamua kwenda mlangoni walipokuwa wanakaribia kuuvunja na kupiga risasi moja iliyomuua jambazi kwa nje bila yeye kujua. Anasema kwa kuwa alitumia dakika karibu 30, alichoka hasa kwa kuwa miguu inamsumbua na akakaa kwenye kochi akiwa ameshika bastola akisubiri jambazi wa kwanza kuingia ambebeshe chuma cha mwili. Ghafla akasikia kimya. Kwa kuwa alikuwa ameshapiga simu polisi na kwa mwenyekiti wa kijiji, aliambiwa na mwenyekiti huyo kwamba polisi wanakuja.
 
Polisi walipofika walikuta majambazi yamekimbia na kuacha mwili wa mwenzao ukiwa umeanguka chini nje ya mlango tu. Mama yuko safi na alikuwa akihadithia kwa ushupavu bila woga wala nini. Tunamshukuru Mungu mama wa watu amesalimika.
 
Pia blogu hii nayo ilimtoa mama huyu: http://tulonge.com/profiles/blog/list.
 
Matinyi.

0 comments:

Post a Comment