Saturday 8 December 2012

[wanabidii] Haya mauaji yanayofanywa na polisi yatakoma lini?


Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Emmanuel Nchimbi aliunda tume kuchunguza chanzo cha mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Bw Daudi Mwangosi, anayedaiwa kuuwawa na askari polisi wakati wakiwadhibiti wanachama wa CHADEMA waliokuwa wakiwazuia wasifungue tawi la chama chao ktk Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi. Kwa upande mwingine, Baraza la Wahariri Tanzania (MCT) nao waliunda tume nyingine kuchunguza chanzo cha kuuliwa kwa mwandishi huyo.

 

Matokeo yaliyotolewa na kamati hizi mbili yalitofautiana kwa kiasi kikubwa sana. Wakati tume iliyoundwa na MCT ikiwatia hatiani polisi na kuwanyooshea kidole kwa kusababisha mauaji hayo, tume ya Nchimbi iliwasafisha polisi kwa kudai kwamba hawakuhusika na kadhia ya kuuwawa kwa Mwangosi. Ushahidi wa picha za video na mnato zilizopigwa na vyombo mbalimbali vya habari unaonesha kwamba Mwangosi aliuawa kwa bomu lililorushwa na mmoja wa askari polisi waliokuwa wakimchapa bila huruma mwandishi huyo.

 

Badala ya tume ya Nchimbi kutoa majawabu juu ya nini kilichotokea, ilijitahidi kuficha ukweli kwa kisingizio cha kwamba hilo swala liko mahakamani. Huenda hayo ndiyo majibu waliyoagizwa na bosi wao, Nchimbi, waje wayatoe kwa wananchi, ambao wengi wao hudhaniwa kuwa mbumbumbu na wasiokuwa na uwezo wa kuchambua mambo. Pamoja na umbumbumbu wao, wananchi wengi wamebaki wakijiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu (ambayo yalipaswa yajibiwe na tume ya Nchimbi).

 

Mosi, ikiwa polisi hawakuhusika kumchapa na hatimaye kumuua Mwangosi, je, polisi anayeshikiliwa kwa sababu ya mauji yaliyotokea katika hizo vurugu, anashitakiwa kwa kumuua nani, hasa ikizingatiwa kwamba katika hizo vurugu kilitokea kifo cha mtu mmoja pekee ambaye ni marehemu Daudi Mwangosi? Pili, je, zile picha za mnato na za video zinazoonyesha kundi la polisi wasiopungua wanane wakimpiga vibaya marehemu Mwangosi zilipigwa kutoka nchi gani kama sio kutoka Tanzania, mkoani Iringa? Tatu, inasemekana lile kundi la askari lilikwisha kumuua Mwangosi hata kabla yule polisi mmoja hajamlipua kwa bomu. Nne, je, ni kwa nini wale polisi walioshirikiana kumuua wasitiwe hatiani wote na badala yake akamatwe mmoja tu (aliyerusha bomu) ilihali wote walishiriki kufanya mauaji?

 

Maswali haya, pamoja na mengine mengi, ndiyo yanayohojiwa na wananchi, na ndiyo yanayoifanya ripoti iliyotolewa na tume ya Nchimbi kuwa batili na ya kugushi. Kwa maana nyingine ni kwamba ripoti hiyo haikukata kiu ya wananchi walio wengi ambao walitaka kufahamu, kwa undani, juu ya utata mzima uliokuwa umegubika kisa cha kuuliwa mwandishi huyu wa habari kufuatia kipigo kikali cha polisi, licha ya kwamba marehemu alikuwa akifahamika kwa polisi wa Iringa kwa muda mrefu.

 

Ni sababu hizo ndizo zinazowashawishi wananchi kuamini kwamba pesa zao za kodi zimetumika vibaya kwa kuunda tume kanyaboya yenye lengo la kuficha ukweli badala ya kuuanika na hatimaye kutoa majawabu muafaka juu ya nini kifanyike ili kutokomeza ukatatili wa polisi kwa raia wasiokuwa na hatia. Ikumbukwe kwamba kabla ya tukio la kuuwawa kwa Mangosi, polisi walikwishaua wananchi kadhaa katika maeneo tofauti ya nchi, wengi wao wakiwa wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakipigwa risasi za moto kiholela, na hayo yamekuwa yakifanyika hadharani na mchana kweupe!

 

Wakati bado tunatafakari mauaji ya Daud Mwangosi, majuzi tumesikia kwamba mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, Shaban Matutu, naye kapigwa risasi na polisi na kunusurika kuuawa. Kama ilivyo kawaida, Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kinondoni akaibuka na kutetea uovu huo. Watu tumebaki tunajiuliza bila majibu: 'Ni lini hasa haya mauaji ya kionevu yatakoma?' Je, tubaki tukiuawa hivi hivi mpaka Yesu atakaporudi? La hasha! Uvumilivu huo unakaribia kufikia kikomo sasa. Kila jambo likizidi kipimo huleta madhara yasiyovumilika, hasa linapokuwa linatendwa kwa makusudi bila kuzingatia weledi na utumiaji wa akili!

 

Jeshi la polisi, pamoja na wale wanaowatuma kufanya hayo mauaji (kama wapo) wanapaswa kufahamu kwamba mauaji wanayoyafanya ni ya kiuonevu na kishetani, na kwamba risasi wanazotumia kuua zinatokana na kodi za wananchi wanaowaua. Damu ya hawa watu haiwezi kwenda bure. Iko siku wananchi wataishiwa uvumilivu na kuamua kuwa sugu, kisha wachukue sheria mikononi mwao. Hapo ndipo wanasiasa wanaowatumia polisi kufanya mauaji ya kiholela watakapolia na kusaga meno.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
DELL LATITUDE D 620 & D30
 
80 GB HardDisk ,CORE 2 DUO , 2.0 GHZ CPU ,2 GB RAM
DVD/CD - RW ,WINDOWS 7 /WINDOWS XP ,WIRELESS , BLUE TOOTH .
 
TSHS : 380,000 , 1 YEAR WARRANTY
 
CALL : 0786 806028
Free Delivery in Dar es salaam
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment