Sunday 9 December 2012

[wanabidii] Bila mambo haya CCM hatihati 2015

IKIWA Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka kushinda Uchaguzi Mkuu mwaka
2015 ni lazima kijirekebisha sasa kwa upande wa Zanzibar.
Kijirekebishe kwa sababu mazingira ya uchaguzi yamebadilika, wapiga
kura wapya ni wenye matumaini ya maendeleo na kuondolewa matatizo yao
ya kijamii, ukosefu wa ajira, maisha bora kwao ndio kipaumbele.

CCM sio tena chama dola, hakilindwi na Katiba kwa kuwa Tanzania
ilirejea mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992, hivyo kudhani kuwa CCM
ina hakimiliki ya kutawala milele ni kujidanganya kwa dhamira yake
kubaki madarakani, CCM Zanzibar waelewe kuwa dhamira ya kila chama cha
siasa kushinda uchaguzi na kuunda Serikali.

Wazanzibari wa leo wengi wao wamezaliwa baada ya mageuzi ya kisiasa,
hawamjui Sultan wala Mapinduzi, mambo hayo yamebaki katika kumbukumbu
ya matukio ya kihistoria tu.

Ushindi wa chama chochote cha siasa Zanzibar unategemea nguvu ya
wapigakura wenye misimamo ya wastani katika siasa kwa ushawishi wa
hoja. Chuki, ubaguzi na kutegemea nguvu za dola sio mtaji sahihi kwa
chama cha siasa kushinda uchaguzi, kundi lililozuka Zanzibar
linalojiona kama lenye haki ya kutawala daima dumu kwa sababu ya jeuri
ya dola linajidanganya.
Hawa wanajidai wao ndio CCM kindakindaki, wanaona wengine hawana haki.
Wamekuwa wakitumia karata ya kulinda Mapinduzi na utetezi wa Muungano
kama ndio ngao yao.
Jambo moja ambalo tunataka kuwaeleza ni kuwa sehemu kubwa ya CCM
Zanzibar iliyopo leo, ni tafauti kabisa na ASP. Katu ASP hakikuwa
chama cha wababaishaji, mamluki; hakikuwa chama cha wazushi. Waasisi
wa ASP akina Mzee Karume, Thabit Kombo Jecha na wengineo walianzisha
chama kwa kuamini katika umoja, ndio maana waliunganisha African
Association na Shiraz Association.

Waasisi wale wa ASP walitoa mali zao, walitoa thumni zao na wakati wao
kwa manufaa ya kizazi cha baadaye cha Zanzibar. Waliwakaribisha watu
wa aina na kabila zote ndani ya cham na baada ya Mapinduzi kwenye
Serikali.
CCM imerithi utawala kutoka Tanu na ASP. Ni Chama kikongwe, lakini
tuwakumbushe CCM Zanzibar kwamba kubaki madarakani kwa kipindi kirefu,
kunaweza kukiponza chama kuliko kukisaidia katika mazingira mapya ya
demokrasia ya vyama vingi.
Tuwakumbushe CCM Zanzibar kuanguka kwa Chama cha Kanu-Kenya, jifunzeni
kutoka kwa Mzee Kenneth Kaunda na Chama chake cha UNIP kilichopigania
uhuru wa Zambia.
UNIP kulikuwa na watu na hata Kaunda mwenyewe hakuwa akiamini kuwa ipo
siku Wazambia watakikataa chama hicho, Mwaka 1992 uchaguzi wa kwanza
wa vyama vingi, yeye pamoja na UNIP yake walishindwa na mgeni katika
uwanja wa siasa, mwanamageuzi Frederick Chiluba. Hiyo ni kwa sababu
Wazambia walikuwa wamekwisha choka na wimbo ule ule ule, walitaka
maendeleo na sio ngonjera za kihistoria na kupigania uhuru, uhuru bila
shibe hauna maana kwao.

Ni funzo wanalotakiwa kupata hawa wanaojidai CCM ndio yenye hakimiliki
ya kutawala Zanzibar. Ukizitazama nyuso za wapigakura wengi utabaini
kuwa Wazanzibari wamechoka kiuchumi wanataka mabadiliko ya maisha yao,
kwa hiyo mgombea urais atakayejitokeza mwaka 2015 akawajaza matumaini
yenye kuingia akilini wapigakura, bila shaka kilichotokea kwa vyama
vya Kanu, UNIP na vyingine ndicho kitakachoikumba CCM.
Kisipojirekebisha kitakabiliwa na hali ngumu, kwani hali ya mambo kwa
miaka hii ya karibuni kuongezeka kwa wapigakura wapya kuna kila sababu
ya kuamini kuwa siku za kutamba kwa CCM Zanzibar na mahafidhina
zinakaribia ukingoni. Wazanzibari wamechoka na hadithi za Hizbu, ASP,
Sultan au Waarabu, Waafrika; watu sasa wanataka mabadiliko ya maisha
yao kutoka hali duni kuwa angalau na uhakika wa mlo wao.
Matokeo ya Uchaguzi uliopita yanapaswa kutazamwa kwa makini sana na
CCM kwani imetokea kwenye tundu ya sindano. Kimepoteza majimbo matatu
Unguja – Nungwi, Mtoni na Magogoni. Hili ni pigo kwa chama hicho
ambacho ngome yake kuu imeanza kumeguka kupitia uchaguzi mkuu mwaka
2010. CCM Zanzibar walipaswa kujitazama upya badala ya kushabikia
makundi, chuki na siasa zile zile za tishio la kurejea Sultan ambalo
halifanyi kazi tena, limesha-expire kwa sasa.

Lakini badala ya kutafuta njia ya kujihakikishia kubaki madarakani CCM
Zanzibar, makundi ndio mwelekeo mbadala wake. Kuna kundi la CCM
mahafidhina, CCM maslahi na CCM progressive.

Inaonekana CCM Zanzibar inapita katika kipindi kigumu na kama itavuka
salama katika hali ya makundi iliyonayo, basi kitakuwa na maisha
marefu kutawala Zanzibar, kinyume chake ndio mwanzo na mwisho wa
mahafidhina na tambo zao.

Siasa za kileo zinahitaji ujuzi, maarifa, sera zenye kuwavuta
wapigakura; matamshi ya ubaguzi, ubabe, vitisho havisaidii kukipa
ushindi chama cha siasa.

Mtihani mwingine wa CCM Zanzibar ni suala zima la mabadiliko katika
muundo wa Muungano. Wazanzibari wengi wanaonekana kutaka yafanyike
mabadiliko ya msingi katika muundo huo.
Muundo wa Muungano hauwezi kuendelea kubaki kama ulivyo. Lazima
wanasiasa wakubali kwamba matatizo ambayo yanatokana na mfumo wa
Muungano huu hayataweza kuondolewa kwa vikao vya Waziri Mkuu na Makamu
wa Pili wa Rais, wataendelea kukaa kila siku, lakini hakuna liwalo.
Msimamo wa kutaka mabadiliko ya muundo wenye maslahi kwa maana ya
mkataba wenye kuzingatia mfumo wa Serikali mbili zenye dola
zinazojitegemea, utakuwa ndio dawa na suluhu ya zile zinazoitwa kero
za Muungano.

Wazanzibari maskini wanazungumzia hali ngumu ya uchumi inayoikabili
Zanzibar na kuwa ugumu wa maisha unasababishwa na mfumo mbaya wa
Muungano. Mathalan,nionavyo mimi Zanzibar ilipojiunga na OIC sio kwa
kutafuta kuongeza idadi ya waumini wa Kiislamu kwani tayari asilimia
95 ya watu wote ni Waislamu, ilikuwa njia kuinusuru na dhiki
waliyonayo wananchi wake.

Kama sera za kiuchumi za Serikali ya Muungano zinakuwa zinainufaisha
Zanzibar kuwa na viwanda ambavyo bidhaa zake zinauzwa nje, vyenye
uwezo wa kuajiri watu 200,000 na kila mtu alipwe mshahara wa Sh300,000
kila mwezi, kutakuwa na zaidi ya Sh10 bilioni katika mikono ya
Wazanzibari.
Ufikapo mwisho wa mwezi kila mtu anakimbilia dukani, marikiti na
sehemu nyingine kutafuta mahitaji, mwenye kununua samani, nguo nzuri,
mchele wa basmati, pishori au siagi ya kismayuu ataweza, lakini pia
hata viwanda vidogo navyo vitachipuka na kufanya mzunguko wa pesa kuwa
mkubwa.

Wazanzibari wengi sasa ni maskini hawana uwezo wa kusomesha watoto wao
katika vyuo vikuu vyenye hadhi kubwa duniani, ikiwa Boflo, kimbilio la
wanyonge haishikiki, imepanda bei nani ataweza kumpeleka Oxford
University, University of Edinburgh?

Wazanzibari kwa muda mrefu wamepumbazwa na kauli za mtaji wa maskini
ni nguvu zake, katika zama hizi za sayansi na teknolojia masuala ya
nguvu kuwa mtaji hayana nafasi tena, akili na ujuzi ndio wenye
kuhitajika.
Lakini utapataje ujuzi ikiwa mtoto wako anashindwa kupata elimu bora?
Wakati tulionao elimu ndio mtaji wa maskini, lakini tujiulize kuna
vyuo vikuu vingapi hapa Zanzibar, mbona Serikali ya Muungano haijengi
vyuo vikuu zaidi ya kuweka tawi la utafiti wa sayansi za bahari ambapo
watumishi wanaletwa kutoka Tanganyika, Wazanzibari wataambulia
'uwochimeni', maana dereva pia katoka kwa kaka mkubwa, vyuo vinajengwa
Dodoma, Mwanza, Tanga, Moshi, Arusha na mikoa mingine.

Asilimia kubwa ya Wazanzibari wanaishi kwa kutegemea jembe la mkono,
kipato wanachopata kutoka katika kilimo cha aina hiyo sote tunakijua
hakiwasaidii kukidhi mahitaji yao muhimu ya kila siku seuze kuendelea,
kwa sasa walio wengi wanaishi chini ya mstari wa umaskini.
Hakuna jambo la kufichana, mfumo wa Muungano wa kikatiba umeshindwa na
ndio umetufikisha hapa tulipo.
Wengi wanadhani muundo wa Muungano ungekuwa kama ule wa Muungano wa
Ulaya kila mtu na chake, tunashirikiana kwa baadhi ya mambo ingekuwa
vizuri zaidi kuliko mambo yalivyo sasa. Ni jambo lililo wazi kuwa
Muungano wa kikatiba kinga yake ni CCM kuendelea kutawala.

Coated by mwananchi news paper.

--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

DELL LATITUDE D 620 & D30

80 GB HardDisk ,CORE 2 DUO , 2.0 GHZ CPU ,2 GB RAM
DVD/CD - RW ,WINDOWS 7 /WINDOWS XP ,WIRELESS , BLUE TOOTH .

TSHS : 380,000 , 1 YEAR WARRANTY

CALL : 0786 806028
Free Delivery in Dar es salaam

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment