Wednesday 12 December 2012

RE: [wanabidii] KATA 7 SERENGETI HAZITATOA MAONI KATIBA MPYA

Kivuyo na LKK,
 
Naomba niwapatie ukweli ninaoujua kwa kutafiti na kufuatilia kuhusu uwepo wa Wakurya wengi jeshini na madai kwamba Nyerere aliwapeleka jeshini - si kwa kuwa mimi ni mkurya! La hasha!
 
Kwanza niseme hivi, ni kweli kwamba Wakurya ni wengi sana jeshini kulinganisha na makabila mengine ya Tanzania ingawa katika miaka ya karibuni wamekuwa wakipungua kutokana na sababu nyingi ambazo hapa si mjadala wake.
 
NANI ALIWAINGIZA JESHINI
 
1. Wakurya waliingizwa jeshini kwa mara ya kwanza na Waingereza wakati wa kuandaa jeshi la kikoloni ambapo ilipotokea vita ya pili ya dunia, Waingereza walikwenda vijijini kwa Wakurya na kuwakamata ama kuwahamasisha vijana wao waingie jeshini ili kwenda kupigana. Baadhi yao waliporejea, akiwemo Marehemu babu yangu mzaa mama na baba yangu mkubwa, walikataa kuingia jeshini wakisema wana mali nyingi na wakaenda kuangalia ng'ombe zao. Hawa walipigania nchini Burma huko Asia. Utamaduni huu wa kuingia jeshini ukaanzia hapo na kuendelea.
 
2. Kwa nini Waingereza waliwachukua Wakurya wengi kwenda jeshini? Ni kwa sababu ya dhana kwamba makabila ya Waafrika yana vipaji tofauti na kwamba ili kuwatawala Waafrika kwa urahisi, inabidi kuvitumia vipaji hivyo. Mfano, Waingereza walisema kwamba ukitaka madaktari wengi watiifu na wapole wachukue Wasukuma kwa sababu ya upole wao na utiifu na kweli tunao wengi sana. Waingereza wakasema tena, wafanyakazi wazuri wa ndani ni Wanyasa - kweli, wafanyakazi wa ndani wa balozi na maofisa ubalozi wa Uingereza hata sasa hivi ni Wanyasa kwa sababu ya uaminifu wao. Walisema pia kwenye elimu weka Wachaga na Wahaya na ni kweli hadi leo waliobobea shuleni zaidi nchini na nani? Tunajua wote! Wakasema, kule Kenya, ukitaka wasomi chukua Wajaluo na Uganda wakasema ukitaka wasomi chukua Waganda. Kwenye uaskari walisema kwamba kwa Uganda chukua Walango, Waacholi na ikibidi sana Wakakwa (kabila la Idi Amin). Nchini Kenya walisema kwamba kwa askari bora uchukue Wakamba. Kwa Tanganyika wakasema chukua Wakurya na ongeza Wangoni na Wahehe. Wakaongeza zaidi na zaidi kwenye mpangilio wao. Ipo orodha ndefu. Waingereza walifanya utafiti mzuri na walipoondoka walimwachia kila kiongozi wa Afrika (makolonini) matokeo ya utafiti wao ingawa akina Nyerere hawakuzifuata. 
 
MATOKEO YA SERA YA WAINGEREZA
 
3. Nini matokeo ya mpangilio huu wa Waingereza? Kule Uganda karibu wanajeshi wote wakati Amin anaichukua nchi (walikuwa 8,000 hivi), walikuwa Walango, Waacholi na Wakakwa lakini kwa kuhofia kupinduliwa akaanza kuwaua Waacholi na Walango na kuwajaza Wakakwa na baadaye akawaweka mpaka Wazaire na Wanubi wa Sudan kusini na kaskazini mwa Uganda. Kule Kenya hadi kesho, majeshi ya Kenya yamejaa Wakamba na kwa mnaofuatilia mtamkumbuka Jenerali Muringe. Kwa kuwa Wakikuyu wamekuwa wakishika dola, Wakamba waliminywa kwenye vyeo vya chini lakini wamejaa majeshini Kenya kupita kiasi, hasa kutokana na umaskini wa nchi yao ya Ukambani ambayo ni kame pia.
 
NYERERE KUUNDA JWTZ 1964
 
4. Kwa Tanganyika Wakurya walijaa jeshini mno wakati tunapata uhuru kiasi kwamba Nyerere akasema hili ni tatizo. Alipovunja Kings African Rifles na kuunda JWTZ baada ya maasi ya 1964, Nyerere aliamua kuweka sera kimya kimya kwamba jeshi hili litakuwa na watu wa makabila yote. Ilikuwa kazi ngumu kwake kwa kuwa waliokuwa wanakuja kujiandikisha kwa wingi walikuwa ni Wakurya zaidi kutokana na utamaduni wa kawaida wa Wakurya wa kupenda kupigana, vita, ukakamavu, umwamba, n.k. Wakurya, kama Wakamba, Waacholi, Walango, na Wakakwa waliitwa na Waingereza "Marshal Tribes" - yaani makabila la wapiganaji. Hata hivyo, Nyerere alifanikiwa kuwapunguza mno lakini bado alibakia nao wengi kutokana na utamaduni, historia na ukweli wa mambo, kwamba ukitaka askari mzuri chukua anayependa vita, siyo mtu mwoga. Kama si Nyerere, jeshi lingekuwa wakurya watupu, siyo wakurya wengi, bali wao wenyewe kwa hata 90%.
 
WAKURYA NA NYERERE
 
5. Wakurya hawakuwa na urafiki wowote na Nyerere kama watu wanavyodhani kutokana na fikra za Kiafrika kwamba kila kitu kina nguvu za siri nyuma yake, iwe baraka za Mungu, rushwa, udini, mapenzi, ukabila, uchawi, fitna, mkosi, n.k. Mwafrika haamini kwamba kitu kinaweza kutokea kwa sababu zake chenyewe bali mpaka kuwe na mtu mwingine anayekifanya kitokee. Kati ya watu waliotaka kumpindua Nyerere kwenye miaka ya 1960 mwishoni, kwa mnaofuatilia, walikuwepo akina Chacha (nahifadhi jina lake kamili), na kutokana na tabia ya Wakurya kumtukana Nyerere alipokwenda ziarani Tarime, aliamua kuacha kufanya ziara huko. Si hivyo tu, Nyerere alikwepa hata kuwapa nafasi za juu Wakurya na mkurya pekee aliyewahi kushika uwaziri katika miaka 25 ya Nyerere ni Bhoke Munanka ambaye walikorofishana hata hivyo (waziri pekee aliyemwambia kwamba huu ujamaa wako utaumiza watu na hakuna anayeutaka). Kama mjuavyo, Munanka alikuwa mfanyabiashara mkubwa katikati ya ujamaa.
 
6. Aidha, Rais Nyerere hakuwahi kumteua mkurya kuwa mkuu wa majeshi wala msaidizi wala chochote cha juu ingawa ukiongea na watu wanakwambia mambo mengine kabisa. Mkuu wa kwanza wa JWTZ alikuwa Sarakikya kutoka Meru; akaja Twalipo kutoka Songea; akaja Musuguli kutoka Bunda (si mkurya). Rais Mwinyi ndiye aliyekuwa wa kwanza kumteua mkurya kuwa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Kyaro, na baadaye Mkapa akamteua Jenerali Waitara. Hata kwenye Vita ya Uganda, Nyerere hakumpa mkurya kuongoza vita ile ingawa kwenye makamanda wa chini Wakurya walijazana kama utitiri, achilia mbali askari wa kawaida. Ni Mwita Marwa pekee ndiye aliyekuwa kwenye makamanda wa kuongoza brigedia, lakini wengine wote walibanwa pembeni........Nyerere hakutaka taabu baadaye.
 
WAKURYA KUPENDA VITA/JESHI
 
7. Kwa wenye kumbukumbu na wanaofuatilia, tulipovamiwa na Amin Oktoba 31, 1978, na baadaye Nyerere kutangaza vita, serikali ilitoa mwito kwa wananchi kujiunga na mgambo/jeshi kwa hiari. Nafasi zilikuwa 2,000 kwa kila mkoa. Wakurya walilaani kitendo hicho cha kuweka ukomo wa idadi na wakatuma wajumbe kwenda kulalamika kwa Nyerere kwamba idadi ya 2,000 ni ndogo mno kwa mkoa wa mashujaa. Nyerere akasema hawezi kuondoa ukomo huo. Wakatuma tena ujumbe wa pili, na Nyerere akashauriwa na makamanda wake kwamba kwa kuwa mikoa mingine imeshindwa hata kufikisha 500 tu, basi ni heri Wakurya waachiwe waje tu. Nyerere akasema kwamba basi anaruhusu nafasi 4,000 kwa mkoa wa Mara. Hii imeandikwa kwenye vitabu na waandishi wasiokuwa Watanzania.
 
8. Wazee wa mkoa wa Mara walikerwa mno na uamuzi wa Nyerere wa kuweka ukomo mwingine wa 4,000 na wakaamua kwamba dawa ni rahisi sana, kwamba vijana wao waende kwenye mikoa ambayo ilikuwa imeshindwa kufikisha idadi ya 2,000 ya awali. Huu si utani. Kaka yangu alikwenda Morogoro. Baba yangu mkubwa alikwenda Moshi na ndugu yangu mwingine alikwenda Usukumani na wote wakaenda vitani na wakarejea kwa ushindi na furaha. Wote wapo hai hadi leo na kaka yangu huyu aliingia Magereza baadaye. Kwa kifupi, Nyerere aliwabana Wakurya wasiende vitani kwa wingi kama walivyotaka. Mjomba wangu Nyaronyo Kicheere alipata medani ya vita pia kwa kujitolea kwenda vitani akitokea JKT - yumo humu ukumbini muulizeni.
 
KWA NINI WAKIMBILIE JESHINI
 
9. Mimi binafsi, wakati ninamaliza kidato cha sita na huku nikiwa nimefaulu, uamuzi wangu ulikuwa kwenda JWTZ kwanza na mambo mengine yafuate baadaye. Kama si wazee wangu kunikatalia, leo hii ningekuwa kwenye magwanda. Naomba Kivuyo na LKK mniambie, mimi niliyezaliwa mjini, nikakulia Dar es Salaam, simjui Nyerere wala hanijui, ninahusika vipi na Nyerere wakati aliacha urais nikiwa sijafika miaka 18? Nyerere ametoka kwenye urais mwaka 1985 lakini miaka 27 baadaye bado Wakurya wamejaa jeshini ingawa wananyanyaswa kutokana na maneno ya kipuuzi kama haya, je, Nyerere anahusika vipi na kuwepo kwao? Mkurya wa miaka 20 leo, aliyeko jeshini, anahusika vipi na Nyerere? Kwa ufupi ni hivi ........... Wakurya tunalipenda jeshi, basi! Nenda hata Kenya utawakuta jeshini, mpaka hapa Marekani wamo jeshini. Je, Nyerere aliitawala Kenya na Marekani?
 
10. Pili, kutokana na maendeleo kuwa nyuma sana mkoani Mara, sehemu pekee ya ajira ilikuwa jeshini kwa miaka mingi hadi walipoanza kuchimba dhahabu kwa wingi kule Nyamongo, na kuuza ng'ombe kwa magendo nchini Kenya. Wilaya ya Tarime, wakati ule wa Nyerere, ilikuwa kama sehemu ya Kenya kwani magharibi ilizibwa na Ziwa Viktoria, kusini na mbuga ya Serengeti, na kuja Mwanza kulikuwa na mto usiokuwa na daraja (Mwinyi alilijenga baadaye), kule mashariki na kaskazini ilikuwa nchi ya Kenya. Nyerere hakutaka hata kufanya ziara tu, achilia mbali kujenga walau shule moja. Hivyo, jeshi likawa kama kimbilio la ajira lakini hii ikiwa ni baada ya kuangalia kwanza hulka na silka ya Wakurya kwenye masuala ya kupigana/jeshi/ushujaa, n.k.
 
Ndugu zanguni Kivuyo na LKK, siwalaumu kwa kudhani hivyo kwa kuwa haya maneno yako hivyo lakini kama nilivyosema, ndivyo Waafrika tulivyo. Ushahidi uliopo ni kwamba Nyerere hakuelewana na Wakurya hata mara moja na aliwabana wasiingie jeshini lakini akafika mahali akashindwa. Ushahidi ni wa kutosha na mkitaka nitawapa kwenye barua pepe zenu binafsi kwa kuwa hapa si vema kuyataja majina ya watu bila vibali vyao.
 
Wakurya tuna vitu vitano tunavyovipenda sana: Kupigana, familia, ng'ombe, ukweli na utaifa. Ni fahari kubwa kwa mkurya kuingia jeshini, fahari kubwa mno; wanangu madume wote wawili, mmoja miaka 9 na mwingine 6, wako hapa Marekani lakini wanapenda kuvaa nguo za jeshi na kucheza na matoi ya vifaru, ndege za jeshi, n.k.
 
Jeshi liko damuni kwa Wakurya!
 
Asante,
 
Mobhare.


From: lembu.kivuyo@gmail.com
Date: Wed, 12 Dec 2012 18:02:59 +0300
Subject: Re: [wanabidii] KATA 7 SERENGETI HAZITATOA MAONI KATIBA MPYA
To: wanabidii@googlegroups.com

Nitapenda kujua zaidi ukinitoa giza na wenzangu wengi tuliookota taarifa hizi mitaani. Lakini pia takwimu za wanajeshi wakurya waliokuwa jeshini wakati  wa Nyerere zinaashiria ukweli huu

Udadisi tu

Real Change for Real Development,  

Lemburis Kivuyo
+255654650100/078 7665050/0755646470
Website: www.kivuyo.com,  Skype: lekivuyo, Facebook: http://facebook.com/lemburis.kivuyo, Titter: http://twitter.com/lembu1, Linkedin: http://tz.linkedin.com/in/lembukivuyo, Google+: gplus.to/lembukivuyo



--
Jobs in Africa - www.wejobs.blogspot.com
nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
DELL LATITUDE D 620 & D30
 
80 GB HardDisk ,CORE 2 DUO , 2.0 GHZ CPU ,1 GB RAM
DVD/CD - RW ,WINDOWS 7 /WINDOWS XP ,WIRELESS , BLUE TOOTH .
 
TSHS : 360,000 , 1 YEAR WARRANTY
 
CALL : 0786 806028
Free Delivery in Dar es salaam
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment