Saturday 20 October 2012

[wanabidii] RE: [Mabadiliko] Neno La Leo: Udini Ndipo Ulipo Ubovu Kwenye Kamba Inayotuunganisha Watanzania

Maggid,
Haya wenye hekima wote waliyaona na hata siye wa kawaida tuliyaona pia lakini kilichoyalipua ama kinachoyalipua wote tunakijua; tunakijua na hata chenyewe nacho kinajijua.
Hapa ndipo thamani ya busara za Mwalimu Nyerere inapoonekana kwani alikuwa tayari kutumia 'mikwaju' ili watu tunyooke kwani aliubaini udhaifu wa mwafrika - kujibagua, kutaka kutengana na kuzua kasheshe lenye kifo. Mnaijeria mmoja aliniambia mwaka 2006 hivi: "Nyie Watanzania mna bahati sana Mungu aliwapa Nyerere, siye wengine tulipata viongozi wapumbavu kabisa." Lakini kama ujuavyo, leo watu wazima na akili zao wanayashika mafundisho ya ajabu ajabu na kumwita Nyerere eti "Mzee Nyerere" kama njia ya kukwepa na kuyatusi aliyoyafanya, kuyakataa yale yaliyotufikisha hapa hata kama yeye binafsi yake hatumpendi kwa udhaifu wetu ule ule.
Sijui kwa nini watu hawajifunzi yaliyowapata wengine hapa hapa Afrika?
Matinyi.
 

Date: Sun, 21 Oct 2012 06:26:41 +0100
Subject: [Mabadiliko] Neno La Leo: Udini Ndipo Ulipo Ubovu Kwenye Kamba Inayotuunganisha Watanzania
From: mjengwamaggid@gmail.com
To: wanabidii@googlegroups.com; mabadilikotanzania@googlegroups.com

Ndugu zangu, 

Wahenga walisema; Kamba hukatikia pabovu. Na siku zote, uzoefu ni mwalimu mzuri sana. Mathalan, uzoefu unatufundisha, kuwa kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, yaweza kuwa ni kazi ngumu sana. 

Ona, moto ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza kijiji kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa hatari ya kucheza na moto. 
Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe. 

Ndugu zangu,
Jumapili hii ya leo ningependa sana tuyakumbuke maneno ya busara na hekima nyingi kutoka kwa Bi. Joy Mukanyange. Huyu alikuwa Balozi wa zamani wa Rwanda nchini Tanzania. Mama huyu aliyatamka maneno haya miaka 13 iliyopita,  takribani miezi sita kabla ya kifo cha Baba wa Taifa. Bi. Joy Mukanyange ( Pichani juu) alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona. Ni kama vile alikuwa mtabiri, maana, alichokisema mama yule leo ndio tunaanza kukiona. Siku ile ya Aprili 6, 1999, katika iliyokuwa Kilimanjaro Hotel, Bi Joy Mukanyanga aliyatamka haya; 

" Naogopa, kwani nimeanza kuona dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa kidini nchini Tanzania na eneo lote la Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza kusababisha maauji ya halaiki kama yale yaliyotokea nchini mwetu mwaka 1994." Alisema Balozi yule wa Rwanda kabla ya kuendelea kutoa ufafanuzi wa historia ya Rwanda na matukio yaliyosababisha mauaji yale ya Wanyarwanda ya wao kwa wao. Ndio, Bi Joy Mukanyange alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona. 

Na tutafanya makosa makubwa, kama hata sasa, tutajifanya kuwa hatukioni kile ambacho Balozi Joy Mukanyange alikiona .  Watanzania tukubali  sasa kuwa tumepatwa na bahati mbaya sana ya baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Kuna wanaotaka tuanze kubaguana kwa misingi ya kidini. 

Hili ni jambo la hatari sana. Ni hulka ya mwanadamu, anapokuwa matatizoni kumtafuta kondoo wa kafara. Mtu mwingine wa kummyooshea kidole kwa matatizo yake. Hali duni ya uchumi wa nchi, hali duni za maisha na umasikini wa watu wetu isiwe chachu ya kuanzisha vurugu za kijamii. 

Maana, taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachagga na wao Wazaramo. Tunasahau, kuwa katika nchi yetu hii hakuna Sisi na Wao, kuna SISI tu.Tutakapokumbwa na maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI, hakutakuwapo na WAO. 

Hatari kubwa ninayoiona ni tatizo la wengi wetu kuwa na ufahamu mdogo juu ya dunia tunayoishi sasa, kibaya zaidi, ufahamu mdogo wa historia yetu. Hivyo basi, kupelekea hali ya kutojitambua kama taifa. Ndio, uelewa wa historia ya jamii husika ni jambo muhimu sana. Kiumbe huwezi kuelewa ya leo, kesho na kesho kutwa kama huelewi ya jana. Kuielewa historia yako ni kuelewa ulipo na unakokwenda. Historia ni kama maji ya mto, kamwe haijirudii. Historia ni wakati, ni muda. Kihistoria jana ni sawa na zamani. 

 Karne nyingi zilizopita wahenga wetu walitafsiri muda kama mkusanyiko wa matukio ya zamani na sasa. Waliamini kuwa yaliyotokea zamani na yanayotokea sasa ndiyo yenye kusaidia kubashiri yatakayotea kesho, yataamua mustakabali wetu. 

 Dalili tunazoziona sasa za kupandikiza mbegu za chuki kwa misingi ya udini na ukabila si dalili njema. Haya yatatupelekea kwenye maafa. Tuliopata bahati ya kutumia kalamu zetu hatuna budi kuliweka hili hadharani. 

Hii ni nchi yetu. Katika ulimwengu tunamoishi kuna mamilioni ya watu ambao hawana nchi. Wahenga wetu walishiriki katika kuijenga nchi hii, wametutarajia sisi tuendelee kuijenga na kuilinda hadhi ya nchi yetu. Mengine yanayofanyika sasa sio tu yanaitia doa nchi yetu, bali, yanaiaibisha nchi yetu. 

Ndugu zangu, 

 Hatuna haja ya kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini na rangi. Sisi wote ni Watanzania. Tuna historia ya kujivunia. Ni historia yetu wenyewe. Kinyume na baadhi yetu wanavyofikiri au wanavyotutaka tufikiri, historia yetu haikuanzia enzi za Mwarabu , Mjerumani au Mwingereza. Historia yetu haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz. 

Na dini hizi za kimapokeo zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta dini zetu za asili, na bado tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii matambiko. Afrika kila ukoo una tambiko lake, hivyo basi, dini yake. Kamwe hutasikia Waafrika wanagombania matambiko. Hutasikia Waafrika wakigombana kwa tofauti za matambiko yao. 

Na sisi ni Waafrika. Hii leo mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa kuwafanya wachinjane ni kwenye kwenye tofauti zao za imani hizi za kimapokeo; Uislamu na Ukristo. 

Naam; kamba hukatikia pabovu, wanasema wahenga.Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania. Tusifike mahali tukagombana kutokana na tofauti za imani ama dini ambazo wala si za asili yetu. Imani au dini ambazo, kama ilivyo dini zetu za asili, nazo zinatutaka wanadamu tuishi kwa amani, upendo na maelewano.

 Na hilo ndilo Neno la leo. 

Maggid Mjengwa, 

Iringa. 

0788 111 765, 0754 678 252
http://mjengwablog.com

--
Unapokea Email hizi kwa sababu umejiunga na Jukwaa la 'Mabadiliko'.
Kuchangia mada tuma kwenye Email hii: mabadilikotanzania@googlegroups.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda; mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com
Utapokea Email ya kudhibitisha kujiondoa kwako.
 
TEMBELEA Facebook yetu:
http://www.facebook.com/MabadilikoForums?ref=hl
 
For more options, visit this group at:
http://groups.google.com/group/mabadilikotanzania?hl=en?hl=en
 
---
You received this message because you are subscribed to the Google Groups "Mabadiliko Forums" group.
To post to this group, send email to mabadilikotanzania@googlegroups.com.
To unsubscribe from this group, send email to mabadilikotanzania+unsubscribe@googlegroups.com.
 
 

0 comments:

Post a Comment