Thursday 11 October 2012

Re: [wanabidii] Mwangosi - Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu

Iwapo siku zote tume ingefanya kazi kama hii dhidi ya watu, vyombo au mamlaka zinazovunja haki za binadam au kushtumiwa kufanya hivyo, tungekuwa tumeshapata uelekeo mpya na Sura halisi ya kisiwa cha amani (Tanzania).

Lakini katika matukio kadhaa walionekana kulala, huku kazi wakiachiwa wanaharakati.

Nataka niamini kuwa Tume haitarudi nyuma

Nova



From: Mobhare Matinyi <matinyi@hotmail.com>
To: Mabadiliko <mabadilikotanzania@googlegroups.com>; Wanabidii googlegroups <wanabidii@googlegroups.com>
Sent: Wednesday, October 10, 2012 9:32 PM
Subject: [wanabidii] Mwangosi - Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu

Ufuatao ni Muhtasari wa taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
 
Tume imetamka bila kuuma maneno kwa uvunjaji wa haki za binadamu ulitokea, na wamepiga marungu RPC wa Iringa na Msajili wa Vyama vya Siasa. Wamechambua sheria za nchi zilizovunjwa. Kwa ufupi, wamezikanyaga zile taarifa za jana bila kunuia.
 
Kwa sentensi chache tu, kuna mapendekezo yao kuna sehemy wamesema:
4.      Demokrasia ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
 
Kwenye hitimisho sentensi ya mwisho imesema:
 
Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala.
 
Jisomee au chota kwenye kishikizo.
 
***********************************
 
MUHTASARI WA TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
YA UCHUNGUZI WA TUKIO LILILOPELEKEA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI KILICHOTOKEA SEPTEMBA 2, 2012 KIJIJINI NYOLOLO, WILAYA YA MUFINDI, MKOANI IRINGA
 
1.       UTANGULIZI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 129(1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7  ya mwaka 2001. Jukumu kubwa la Tume ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini.  Katika kutekeleza jukumu hilo Tume imepewa mamlaka ya kupokea malalamiko (kwa njia mbalimbali) kutoka kwa mtu yeyote au kuanzisha uchunguzi wake yenyewe endapo itaona kuna uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
 
Kwa kuzingatia majukumu hayo, Tume ilianzisha uchunguzi wake yenyewe baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa ya tukio la kifo cha Daudi Mwangosi. Tume iliunda timu ya watu watatu iliyoongozwa na Mhe. Kamishna Bernadeta Gambishi akisaidiwa na maafisa wawili, Bwana Gabriel Lubyagila na Bwana Yohana Mcharo. Timu hiyo ilifanya uchunguzi wake kuanzia tarehe 13-19 Septemba, 2012.
 
Katika uchunguzi uliofanywa, Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo basi, Tume ilitilia maanani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria mbalimbali za nchi na mikataba ya kimataifa na ya kikanda inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.
 
Kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Tume Na. 7 ya mwaka 2001, baada ya uchunguzi huo kukamilika, Tume imeandaa taarifa yake na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
 
Taarifa ya uchunguzi wa Tume imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo ni:
a.      Maelezo ya viongozi, watendaji na wananchi waliohojiwa
b.      Uchambuzi wa taarifa/vielelezo vilivyopokelewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu
c.       Matokeo ya uchunguzi
d.      Maoni na mapendekezo.
 
Kwa kuwa tukio la kifo cha Daudi Mwangosi liligusa hisia za jamii, Tume imeona ni vyema kukutana na wawakilishi wa vyombo vya habari  ili kutoa taarifa yake.
 
2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
Katika uchunguzi wake Tume imebaini kuwa:
a.      Tarehe 02/09/2012 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi (OCD) kufanya mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya.  Lakini jioni ya tarehe 01/09/2012 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (RPC), alizuia CHADEMA kufanya mikutano iliyoruhusiwa na OCD ambaye ni "Officer In-charge" wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.
b.      Viongozi wa CHADEMA walikuwa na mazungumzo na Mkuu wa Polisi Mkoa Upelelezi (RCO) na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.
c.       Msajili wa vyama vya siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa.
d.      Wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, RPC alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe; na kuwa wafuasi wa CHADEMA walipinga kukamatwa kwa viongozi wao.
e.      RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
f.        Baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo; na kuwa marehemu Daudi Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu na kufa hapo hapo.
g.      Daudi Mwangosi aliuwawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.
h.     Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo Mwandishi wa Habari wa Nipashe, Bwana Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Bibi Winnie Sanga na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi, Asseli Mwampamba aliyekuwa akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.
 
Kutokana na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
 
2.1 Uvunjwaji wa Haki za Binadamu
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights of 1948), Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights of 1966) na Mkataba wa mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples Rights of 1981), Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki zifuatazo:
·         Haki ya kuishi,
·         Haki ya kutoteswa na kupigwa,
·         Haki ya usawa mbele ya sheria na
·         Haki ya kukusanyika na kutoa maoni.
 
CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu.  Chini ya sheria ya vyama  vya siasa (Cap. 258 RE. 2002), vyama vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa "Afisa wa Polisi" wa eneo husika.  Baada ya taarifa kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na "security agencies" (mawakala wa usalama).

2.2 Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora
Ili pawepo utawala bora mamlaka zote za serikali ni lazima zifuate utawala wa sheria.  Uchunguzi umebaini kuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa "Officer In-charge" wa polisi wa eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo.  Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
 
Aidha, hatua ya Msajili wa vyama vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) Kifungu cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa.
 
Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelezea kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na Haki ya Kijamii, aidha ibara 18(b) na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari) na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.  Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa waandishi wa habari na wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za kisiasa.  Huu ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha uhuru wa habari.

3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
Kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001 Kifungu cha 15(2)(c) na 28 Tume inapendekeza yafuatayo:
1.       Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utalawa bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.  Aidha, kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
2.      Viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti.  Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
3.      Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo Chama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampeni huko Zanzibar.  Aidha, rai ya Msajili wa vyama vya siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo.
4.      Demokrasia ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
5.      Elimu ya vyama vya siasa na sheria ya Polisi kuhusu vyama vya siasa itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.
 
4.0 HITIMISHO
Jukumu la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania, mkulima na mfanyakazi, viongozi wa serikali na watumishi wa umma wote wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.  Tume inatoa wito kwa watanzania wote kuheshimu haki za binadamu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya utalawa bora.  Kwa kufanya hivi Taifa letu litaendelea kuwa na amani na utulivu.  Tume inatoa rai kwa jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila kutumia jazba.
 
Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala.
 
....................................................
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri R. Manento
 
MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
 
OKTOBA 10, 2012
 
--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 


0 comments:

Post a Comment