Sunday 14 October 2012

Re: [wanabidii] Kongamano la Mwl Nyerere Live kutoka ukumbi wa Nkrumah UDSM - Mwanzo

NaEsther Wasira

Mabibi na Mabwana,Mawazo na fikra za Mwalimu zilikuwa pana sana. Kwa kuwa siwezi kuzungumzia maeneo yote, naomba nijikite katika maeneo mawili ambayo naamini ni ya muhimu sana hasa vijana kuyazingatia ili kumuenzi Mwalimu: Maeneo hayo ni, Ukombozi wa mtanzania na Elimu.

1. UKOMBOZI WA MTANZANIA
Dhana ya ukombozi wa mtanzania ilianza tangia wakati wa ukoloni tukiwa bado tunatawaliwa na wazungu. Historia ya ukombozi wa Taifa letu inaanzia nyuma sana, enzi za mababu zetu, akina Mkwawa, Mirambo, Mangi Sina na wengine wengi. Mashujaa hawa walipigania uhuru wa Taifa hili na kuupinga ukoloni na ubeberu, hata kuwa tayari kuifia nchi yao.Mwalimu Nyerere aliendeleza historia ya ukombozi kwa kupinga kwa nguvu zake zote ukoloni na ubeberu mpaka tukafanikiwa kujitawala mwaka 1961. Baada ya uhuru, agenda kubwa ya Taifa ilikuwa ni kujitawala na kujiletea maendeleo yetu.Vijana tunajifunza nini kutoka kwa kizazi cha kina Mkwawa? Walipigana na ukoloni hadi kujitoa maisha yao kwa ajili tu ya Ukombozi; yaani walijitoa sadaka. Halikadhalika, kizazi cha mashujaa wasiotetereka, cha Mwalimu Nyerere, kilipambana kutafuta uhuru wa mtanzania na kufanikiwa kuweka misingi ya ujenzi wa Taifa letu. Hawa mashujaa wote walijitoa sadaka. "They sacrificed their lives for the people of Tanzania".

Mkwawa hakushindwa kupokea rushwa kutoka kwa Wajerumani ili watoto wake japo wakasomeshwe Ulaya, au ajengewe nyumba nzuri, hata ghorofa kama angetaka kupata tu mali nyingi na kuwa tajiri. Lakini, alipuuza utajiri wa kitumwa na vishawishi vya mali ya hatia, akaamua kupigania Taifa lake na uhuru wao wa kuishi, uhuru wa kujitawala, uhuru wa kuamua na kumiliki vitu vyao.Embu tumfikirie Mwalimu, hakushindwa kabisa kuendelea na kazi yake ya ualimu, ambayo wakati huo ilikuwa kazi ya maana na yenye masurufu manono mno, na kunyamaza kimya bila kudai Uhuru. Katika hotuba yake moja aliwahi kusema, baadhi ya watu walikuwa waoga kudai uhuru hasa vijana wasomi, waliogopa kupoteza ajira. Hivyo tunaona jinsi gani uhuru ulivyopatikana kwa mtu aliyeamua kulipa sadaka na kukubali kuyazika maslahi yake binafsi kwa ajili ya wengi. Historia inajua kuenzi na inajua kuhukumu.

Leo waoga wale au wasaliti wale wanakuwa mfano wa kuhukumiwa kwa kupenda maslahi yao binafsi na kushindwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wengi kwa ujumla. Hebu iangalie historia inavyomzungumzia Chief Mangungo wa Msovero ambaye miaka mingi sana iliyopita alikubali kununuliwa na Wajerumani kwa kupewa blanketi na vitu vidogo vidogo na kuuza ardhi na utu wake kwa Wajerumani. Historia inampuuza, inamwona alikuwa mjinga na msaliti. Kwa upande mwingine, Mkwawa na wengine walioamua kujitoa sadaka kwa ajili ya kupigania uhuru na kulinda utu wao leo tunawaheshimu kama mashujaa.Ukienda mbele zaidi, historia inamuenzi Mwalimu Julius Nyerere kwa kutoangalia maslahi yake binafsi bali alijali watu zaidi.

Former director of the Russian Academy of Sciences, Alexei Vassiliev called Nyerere, "Mister Clean Hands" because of his reputation of being a transparent, honest man who served his people with selfless devotion". Ni kiongozi gani Tanzania leo hii anaweza kuitwa na mzungu 'Mister au Mistress Clean na hata katika bara letu la Afrika? Ni vijana wangapi leo hapa Tanzania wanaotamani kuwa na mikono misafi watakapoanza kazi kama watumishi wa umma au viongozi kama sehemu ya kumuenzi Nyerere?Mwalimu hakuwahi kujipendelea au kupendelea kabila lake, dini yake na hata familia yake. Hata baada ya kupata uhuru, Nyerere angeamua asingeshindwa kuwapeleka watoto wake wa kuzaa ng'ambo wakasome huko ughaibuni, hakushindwa kujijengea mahekalu na hata ayaite kwa jina lake, kujilimbikizia mali, majumba na magari ya kifahari, wala watoto wake wasingeshindwa kutumia mgongo wa baba yao kutawala siasa za nchi hii. Leo hii tunaambiwa kazi pekee wanayoweza kufanya watoto wa viongozi ni kurithi kazi za wazazi wao; ndio kusema siku wananchi wakiamua kuwafukuza wazazi wao madarakani ndio mwisho wa watoto hao kisiasa.

Lakini huyo hakuwa Nyerere. Mwalimu na viongozi wenzake walikuwa ni wazalendo, waadilifu waliojitoa sadaka ili kuhakikisha wanaijenga Tanzania tunayoiona leo hata kukubali kufa wakiwa maskini.Nyerere died a poor man but was buried as a hero!! Hapa kipo cha kujifunza, nacho ni kwamba moja ya nguzo muhimu ya uongozi ni kukubali kujitoa kwa ajili ya jamii hata kama wewe hufaidiki na uongozi wako moja kwa moja. Kikubwa zaidi cha kujifunza ni kuwa heshima yako haitatokana na kumiliki majumba, magari ya fahari au mabilioni uliyoweka benki za Uswisi baada ya kuwaibia Watanzania masikini wanaokufa kwa kukosa hata shilingi elfu mbili ya kununua dawa. Heshima yako itatokana na mchango wako katika kutetea maslahi ya taifa hili na watu wake na kulitumikia kwa uadilifu na uaminifu. Heshima yako itatokana na kutetea maslahi wa wanyonge na kuwa tayari kuweka maslahi yako nyuma kwa ajili ya wengine. Ukiweza kufanya hayo vizazi vijavyo vitasema "hapa amelala mtu shujaa".

Hivyo ndivyo wanavyosema watu wanaoenda kuzuru kaburi la Mwalimu pale Butiama. Ukithamini mali tu na kuitumikia familia yako kwa gharama yeyote ile, historia yako itafikia tamati siku udongo wa mwisho utakapowekwa kwenye kaburi lako.Ndio kusema, vijana wa leo, hasa nyie mliopo mashuleni na katika vyuo, tunapaswa na tunalazimika kufungia macho kizazi cha viongozi wa leo kwa kuwa hakuna cha kujifunza katika kizazi hiki. Bali tunapaswa na tunalazimika kufungua macho na bongo zetu tujifunze kwa bidii na kwa haraka sana na hatimaye tuungane kuhuisha misingi imara ya uongozi iliyojengwa na Mwalimu Nyerere na ambayo imebolewa katika kizazi hiki cha leo cha uongozi. Hili ni jukumu la msingi la vijana katika kumuenzi Mwalimu Nyerere na kama kizazi chetu kinataka kuepuka laana ya Mwalimu Nyerere. Vijana, kizazi chetu kina changamoto nyingi sana. Nyerere katika kitabu chake, "Uhuru na Ujamaa, 1968, alisema katika ukurasa wa 33 kama ifuatavyo:

"Kila kizazi kina changamoto zake na kila kizazi kinapaswa kutumia fursa walizonazo kujiletea maendeleo na kufanya maisha bora"

Vijana, fursa ya kuleta maendeleo kwa maisha ya mtanzania ni mabadiliko kutoka katika mfumo wa utawala ulioshindwa na kuweka mfumo mpya. Kuendelea kuimba leo kuwa chama hiki kilituletea uhuru haitusaidii sana vijana maana kutafuta uhuru sio moja ya agenda tena; agenda hii ilizikwa mwaka 1961. Inapoonekana kitendea kazi chochote kimekuwa "hakifai tena" huwa kinatolewa na kifaa kipya huwekwa kulingana na uhitaji wa muda ule na nitakuwa mwongo nikisema mfumo wa utawala na aina ya uongozi uliopo sasa bado unaifaa Tanzania tunayotaka kuijenga.Baadhi ya changamoto tulizonazo vijana katika kumuenzi Mwalimu Nyerere ambazo ndizo tunapaswa kushughulika nazo ili kujikomboa na pia ili tuweze kumuenzi Mwalimu ni hizi zifuatazo:-

a) Kutojitambua tuna nafasi gani katika ujenzi wa Taifa letu.

Tatizo hili la kutokujitambua linaambatana na tatizo kuu la Uoga. Uoga ndio adui mkubwa wa maendeleo ya kijana na Taifa kwa ujumla na limezuia mabadiliko chanya ambayo yangeweza kutokea ili kulikomboa taifa letu. Vijana tumekuwa waoga kusema na waoga wa kutenda. Tumetoa mwanya kwa baadhi ya watu wasio na nia njema na nchi hii kuchukua fursa ya kugandamiza wananchi wa hali ya chini na wao kujineemesha wakiwa katika ncha ya juu ya ngazi. Mwalimu Nyerere alitabiri mwaka 1966, tukiwa wachanga kabisa katika kujitawala, kwenye Kitabu chake "Freedom and Socialism, 1968" ukurasa wa 141, akisema:"If we do not remove fear from our people, it will mean that the sacrifice we paid to help in the work of removing colonialism will be used to maintain other clever Africans capable of oppressing the people more than the colonialists"Inashangaza jinsi gani Mwalimu aliliona hili jambo kwa mbali sana likija.

Tumeshindwa kabisa kuwaenzi wazee wetu waliopigania uhuru wa Tanzania, tumekataa kuihesabu kuwa ya thamani damu yao waliokufa wakipigania uhuru wetu, tumepoteza dira, tunatemea mate jitihada za Mwalimu Nyerere aliyejihatarisha kupoteza kila alichonacho kwa ajili ya maisha ya watanzania. Kwanini tunakuwa waoga? Tukatae kutishwa. Mwalimu anaongezea katika ukurasa huo wa 141:"This is what is going to happen if you do not remove fear from your minds. You will even lose your property. It will be taken by those who are clever among you. You will discover President, Minister, RC or DC owns a very big farm and you will be surprised how he obtained it. We will ask, yesterday we were all poor, how did these leaders become rich overnight?" Iweje wote tulale maskini, leo wewe uamke tajiri, haya majumba na magari ya kifahari umeyapata wapi wakati mshahara wako halali tunaujua? Ni ukweli kabisa kuwa kila siku tunapiga kelele za rushwa na ubadhilifu.

Vijana tunaona madini yetu yanaondoka, rasilimali zetu zinawanufaisha wageni na watanzania wachache, cha ajabu zaidi viongozi wetu wanaelekea huko huko ambako mali zetu zinapelekwa kuomba misaada, na tukijaribu kuhoji mbona safari zimekuwa nyingi, tunaambiwa "bila safari hizo watanzania tutakufa njaa". This is Hilarious! Katika kuenzi fikra za Mwalimu, wakati umefika vijana wote tusimame imara, sisi ndio nguvu kazi ya taifa hili, kukataa rasilimali zetu kutoroshwa, kuhakikisha mikataba inayoingiwa na wageni inanufaisha wananchi wa Tanzania, tukatae kabisa Ukoloni mamboleo na ubeberu. Nyerere katika kitabu cha Uhuru na Ujamaa, (1968), uk 167 anasema;

"Any country must be looked after by the people. If you do not like to accept your responsibility for looking after this country, I shall get a few clever people and together we will declare this country to be our property"

Yaani inashangaza leo hii mpaka watu wamefikia hatua ya kutorosha wanyama hai tena nasikia kwa ndege za jeshi. Yaani kwa maana nyingine ni kwamba tumeamua kuiua sekta nzima ya Utalii Tanzania; maana ukishawapelekea wageni hao wanyama hai, hawana sababu ya msingi ya kuja Tanzania kama watalii. Tukatae kwa kishindo kupelekeshwa na sera mfu na zilizo hoi na kutuingiza kwenye kizaazaa cha maisha yasiyomnufaisha mtanzania. Nyerere aliacha wajibu huo, na hilo ndilo jukumu letu kama vijana.

Nyerere katika kitabu hicho cha Uhuru na Ujamaa, (1968), uk 34 anasema;

"Happily we shall enter into agreements and contracts for trade and economic assistance with friendly peoples and nations from all parts of the globe. But from no quarter shall we accept direction or neo-colonialism and at no time shall we lower our guard against the subversion of our government or our people. Neither our Government, our country nor our freedom to determine our own future are for sale."Ladies and Gentlemen, lets today in unisom declare that "neither our Government, our country, our heritage nor our freedom to determine our own destiny are for sale."
Tukitulia kimya ipo siku tutauzwa na sisi. Ninawaasa vijana tujitambue, tuache uoga, tuichukue nchi yetu, tuijenge Tanzania Mpya. Kila rasilimali unayoiona ndio urithi wetu tuliorithi kwa Baba yetu Mpendwa Mwl Nyerere, kuanzia kijana wa kijijini anayechunga ng'ombe mpaka yule wa mjini aliyeajiriwa kwenye taasisi isiyo ya kiserikali. Tuondoe mtazamo wa kukaa pembeni na kupewa imla ya namna ya kuishi huku wajanja wakiteketeza urithi wetu na kutuacha mafukara. Mabadiliko hayaji bila kulipa gharama, tutatoa gharama. Ila kwa kujaribu kuangalia sababu za uoga huu, nawaona watawala wakifanya watu wawe waoga wa mabadiliko. Kila siku tunaambiwa kuwa tukileta mabadiliko vitatokea vita, watanzania tutakosa maendeleo na mambo mengi yanayofanana na hayo. That is a completely wrong notion!! Labda niseme kwamba, amani ya nchi ya Tanzania ni urithi wetu na ni moja kati ya vitu vya kipekee sana ambavyo Tanzania inavyo. Lakini na ijulikane, hakuna chama chenye haki miliki ya amani ya Tanzania.

Amani hii imejengwa na wazee wetu na itaendelea kuwepo kama tutaendelea kujenga misingi ya haki na usawa kwa watu wetu na wala si kwa kuwa chama fulani kitakuwa madarakani.Katika enzi ya uhai wake, Mwalimu aliwahi kuhojiwa aseme ni jinsi gani Tanzania itaweza kuendelea kutunza amani yake. Mwalimu hakusema, amani ingetunzwa kwa kukichagua chama fulani milele, bali alisema: "Amani ni kama mti ambao ili ustawi lazima uongezewe mbolea, umwagiliwe maji na upaliliwe. Akasema mbolea na maji hayo katika mti wa amani ni haki na usawa katika nchi, kama haki ya kupata elimu, kazi, kuwa na uongozi bora, kumiliki ardhi, kutotofautiana sana kipato hasa kama wenye kipato kikubwa hawalipi kodi au wamepata kipato kwa njia za rushwa au kuiibia serikali nk. Sasa suala la kujiuliza ni, Je, watawala wa sasa wamefanikiwa kupalilia mti wa amani Tanzania, kumwagilia maji na kuuwekea mbolea? Je, ni yupi hasa ambaye ana hatari ya kuleta vita Tanzania? Rushwa ni kilio cha kila siku, elimu si ya usawa kabisa, hata elimu ya juu kupata mikopo watoto wa masikini imekuwa kazi; ukihoji jibu ni kwamba "alisoma masomo yasiyopewa kipaumbele", sasa kama hayapewi kipaumbele, si yafutwe kwenye mitaala ya elimu? Tuache kugandamizana, wanatuambia hatuwezi kujilisha, ni lazima viongozi wakatuombee chakula la sivyo tutakufa njaa, are we not playing with our sovereignty!! Mimi naamini vijana tunaweza, akina mama tunaweza, wazee tunaweza, tuondoe na tuupuuze uoga huu.

b) Ubinafsi.

Hii ni changamoto kubwa sana na ina mahusiano ya karibu na ile ya kwanza. Tunadhani kuwa ukipata wewe na familia yako imetosha. Watanzania tumekuwa na roho za kutojaliana, unajifikiria mwenyewe tu. Yafaa nini kupata mali, kuwa na vitu vya thamani sana na kula vyakula vya gharama, lakini mtanzania mwenzako hawezi hata kujikimu kwa siku. Hayo nayo utayaita ni mafanikio? Hapana, huo ni ubatili na kujilisha upepo! Jaribu kuchukua mfano wa Mtu kama Nelson Mandela, angeweza kupata maisha mazuri sana kama angeamua kutafuta ugali wa familia yake tu. Viongozi wa Tanzania kuanzia kizazi cha Mkwawa na Nyerere walilipia sadaka, hawakuogopa kupoteza, au familia zao kuteseka, hawakuwa wabinafsi. Bila Mandela kujikana, labda leo Afrika ya Kusini ingekuwa bado chini ya makaburu.Vijana lazima tuache ubinafsi, tuiangalie Tanzania, watu wote wa Tanzania, tusijikwamue wenyewe kimaisha tukawasahau wenzetu wasio hata na fursa ya kupata elimu, tuwe tayari kuteseka kwa muda mfupi kwa ajili ya Neema ya kudumu ndani ya nchi yetu.Hainifai kitu na wala haitamfaa kijana kitu kama utapigania maslahi ya familia yako yenye watu wanne au watano.

Harakati zetu za ukombozi, badala ya kuwaletea maisha bora watu wanne wa familia, zitaleta maisha bora kwa watu milioni hamsini wa Tanzania, zitaleta maisha bora kwa wanafunzi wasio na fursa ya kupata elimu au kupata elimu bora, zitawaleta manufaa akina mama wanaotembea makumi ya kilomita kutafuta maji, zitawapa madawati watoto wanaokaa chini, wengine wanasomea chini ya mibuyu, wengine hawana hata matundu ya vyoo ya kutosha, wakifundishwa na walimu waliovunjika moyo na pia zitawafaa akina mama wanaobebwa makumi ya kilomita kutafuta zahanati za kujifungulia na hata wakifika huko hawapati huduma za kufaa nkBila kuondoa ubinafsi, bila kuweka maslahi ya Taifa mbele na maslahi binafsi nyuma, hatutaweza kupata ukombozi wa pili wa Taifa letu yaani kulichukua Taifa hili kutoka katika mikono ya walanguzi na mafisadi wa nchi hii. Kama una tawala ambazo zinaingia kwa makusudi kabisa kwenye mikataba mibovu ambayo Mwalimu aliikataa, serikali inayouza wanyama hai nje, serikali inayoamini kuwa hatuwezi kuishi bila misaada, sidhani kama kuna jina zuri la kuziita tawala za aina hiyo zaidi ya hayo.

c) Ajira

Changamoto ya kukosa ajira yaweza pengine ikawa ndio kilio cha kwanza kikubwa kwa vijana walio wengi wa Tanzania, kuanzia kwa waliokosa fursa ya elimu mpaka kwa waliopata fursa ya elimu, lakini wasijue cha kufanya baada ya kupata elimu hiyo. Ajira zipo za aina mbili: I. Kujiajiri II. Kuajiriwa (ambayo ndiyo nitakayoijadili leo)Kuajiriwa.
Kimsingi, ingawa hata sekta binafsi pia inaajiri sana leo, lakini bado serikali ndio mwajiri mkuu. Swali la vijana ni je, ajira zinatolewa kwa wanaostahili au zinatolewa kwa watoto wanaotoka familia fulani? Ni ukweli kwamba katika Tanzania ya leo ajira muhimu zinatolewa si kwa watu wenye uwezo bali kwa wale waliotoka familia fulani. Ushahidi upo wazi na watanzania wanajua hilo. Hakuna uwazi kwenye ajira, na pasikuwa na uwazi hapana haki itakayotendeka. Kwamfano nilisoma magazeti ya tarehe 12/10/2012, kama Nipashe na Mtanzania, Mheshimiwa Magufuli amelalamikia kitengo cha Mizani kujaza watoto wa vigogo na hivyo kuzuia uwajibishwaji; tena nafasi hizo zilikuwa hazitangazwi, lakini amesema kuanzia sasa zitaanza kutangazwa. Lakini kila mtu ana haki ya kikatiba ya kufanya kazi kwa usawa (Ibara 22(1)(2)).

Ni wakati sasa vijana tudai uwazi katika ajira. Kama hakuna uwazi na haki katika ajira za sekta ya umma, itawavunja nguvu vijana, itaondoa morali ya vijana, na kuwafanya wasione thamani ya elimu waliyoipata tena katika mazingira magumu. Vijana wengi wamejaa mitaani na cha kusikitisha zaidi hata wale wa vyuo vikuu wamekosa ajira kabisa. Upendeleo na ubaguzi ndio unaleta vita na wala si upinzani kama ambavyo imekuwa inahubiriwa na baadhi ya watu.Embu jiulize, vijana wenye nguvu, wenye mitazamo mipya, mawazo mapya yenye kuweza kuleta manufaa kwa jamii yao, wanakosa kazi na badala yake mikataba ya kazi wanaongezewa wazee waliofikia umri wa kustaafu, wasiotaka mabadiliko, wenye mawazo yasiyo endelevu na yasiyoendana na mabadiliko na kasi ya utandawazi.

Ukifuatilia taasisi nyingi mno zimejaza wastaafu makazini, ambao wamechoka na utendaji kazi wao sio mzuri tena. Mfano mzuri upo katika mahakama zetu. Unamkuta jaji ameshatimiza umri wa kustaafu lakini anaongezewa muda au wengine wanateuliwa wakiwa na umri unaokaribia wa kustaafu mathalani miaka 57 na anafanya kazi miaka miwili au mitatu na mwishowe analipwa maslahi ya kustaafu sawa na jaji aliyeitumikia nchi hii kwa miaka zaidi ya thelathini, hii sio haki. Kwanini tusiwateue vijana wenye uwezo ambao si haba Tanzania, ili aweze kuitumikia nchi kwa miaka mingi? Hata katika uongozi wa serikali, hili liko wazi, wabunge vijana na wabunge wazee ni tofauti kabisa katika utendaji, hata kule kuwa "active" bungeni ni tofauti kabisa.

Sasa kwanini kijana ananyimwa nafasi ya kuitumikia nchi yake na uwezo anao? Je, inatosha kuwaambia vijana warudi vijijini kwenda kutekeleza sera ya kilimo kwanza, wakawe wakulima vijijini ambapo mazingira hayajaandaliwa kabisa? Kama miundo mbinu haitarekebishwa, kama huduma za kijamii hazitaboreshwa, sioni huu wito kwa vijana kama utazaa matunda yoyote. Nani atarudi mahali kwenye ukame kwenda kufanya kilimo kwanza kwa kutumia jembe la mkono? Hata basi kijana akibahatisha power tiller, bado si za msaada sana maana katika mazingira yetu haziwezi kulimia hata bustani. Nani alifanya maamuzi ya kuleta power tillers wakati wanajua kabisa kuwa hazitufai?Kwa kuwa leo ninazungumzia hapa Mlimani, kilele cha elimu nchini, nina ombi maalum kwa vijana wasomi:Mwalimu aliwahi kusema kwenye "Uhuru na Ujamaa" katika ukurasa wa 274:

"Our government and our party must always be responsible to the people….the education provided must encourage the development in each citizen, of three things: an enquiring mind…………………………………"

Vijana tunapaswa tuulize, tufuatilie mambo yanavyokwenda, lazima sauti zetu zisikike, sisi ndio tunasimama kwa niaba ya wenzetu waliokosa fursa ya kupata elimu, ambao hawana jukwaa la kuongelea, wenzetu ambao walipuuzwa kwa muda mrefu, ni sisi tuliofanikiwa kupata fursa ndio tutakaoulizwa tuliitumiaje elimu katika kumkomboa mtanzania. Elimu ya Mwalimu ilitusaidia wote, alikuwa ni mtu mwenye mawazo endelevu, aliyeangalia maslahi sio tu ya kizazi kile bali hadi kitakachokuja baada yetu.Mwalimu anaendelea kusema,

"Education system should not be designed to create robots who work hard but never question what the leaders in Government or TANU are saying"

Mimi sidhani kama vijana ni robots, ila tutakuwa endapo tutaendelea kukaa kimya wakati nchi inaporwa na kufilisiwa na watu wachache. Tusiwe watu ambao tumekosa udadisi, hatufuatilii wala kujua nchi yetu inaendaje, wala mchango weti ni upi kwenye jamii. 
2. KUHUSU ELIMU.

Kulingana na muda, nitazungumzia suala moja tu kuhusu Elimu, nayo ni haki ya kupata elimu. Mwalimu Nyerere katiba hotuba zake mbalimbali alizungumzia usawa katika elimu. Mara baada ya uhuru, serikali ya mwalimu ilitumia rasilimali ndogo zilizokuwepo kuhakikisha watanzania wanapata elimu bora na kwa usawa. Hadi Mwalimu anaondoka madarakani, Tanzania ilikuwa imefuta ujinga kwa asilimia 95. Mwalimu alikuwa na upeo wa kujua ili kuondoa ukabila, udini na matabaka ya mabwana na watwana,lazima elimu itolewe kwa usawa na kila mtanzamnia apate haki ya kusoma. Akitoa hotuba yake ya mwisho katika ukumbi huu wa Nkurumah, Mwalimu alisema: "tusomeshe watoto wetu wote, wote, wote kabisa!!Sera ya elimu ya serikali ya sasa bado haioneshi matumaini katika kuleta usawa katika elimu. Serikali ya sasa imetengeneza madaraja mawili ya elimu. Daraja la kwanza ni lile la watoto wa walionacho wanaosoma katika shule nzuri, zenye maabara, computers, maktaba, mabasi ya shule, walimu waliohamasishwa,nk. Bahati mbaya daraja hili ni dogo sana, lakini ndilo linalotoa watoto watakaokuja kujaza vyuo vikuu vyetu vya maana na watakaochukua sehemu muhimu za maamuzi.

Na kwa kweli tayari wameshaanza kushika nafasi muhimu. Daraja la pili ni lile la watoto wa walala hoi katika ngazi za elimu ya msingi na sekondari, hasa shule za kata, ambazo hazina walimu na hata hao wachache waliopo hawajahamasishwa, hazina vitabu, maabara na hata matundu ya vyoo hamna ya kutosha. Hawa wanaohudhuria maeneo na majengo yanayoitwa shule, lakini hakuna elimu ya maana inayoendelea huko. Hakuna ajabu basi kwamba matokeo ya shule hizi ndio kama ambavyo tumeyaona katika miaka miwili iliyopita, ambapo karibu asilimia 90% ya watoto waliomaliza katika shule hizi walipata madaraja ya sifuri (Division 0) na nne (Division 4)!Tukirudi kwenye elimu ya juu, vijana wengi wanarudi nyumbani kwa vile hawana mikopo, na kosa lao lilikuwa kuchagua masomo yasiyopewa kipaumbele, narudia kusema kama ni hivyo yafutwe moja kwa moja. Vijana lazima tudai haki ya elimu yenye usawa na tujue kuwa vijana wa kitanzania tuna haki ya kupata mikopo bila ubaguzi wowote. Cha kushangaza zaidi, wale wenye uwezo ndio wanapata mikopo na walalahoi wanahangaika. Enzi za Mwalimu, alikuwa ameboresha usawa kuanzia ngazi ya juu ya uongozi mpaka chini. Hakuweka matabaka ya waziwazi kama ilivyo leo, na ndio maana hata alivyowaambia vijana 'uchumi umeanguka' wote walimsikiliza na walimuelewa maana hawakumuona yeye akiwa ana maisha ya ufahari, bali wote walikuwa na usawa. Kwa kumalizia, narudia tena, vijana tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa Mwalimu Nyerere; lakini kikubwa ni kuthubutu na kupigania mabadiliko ya kweli bila woga wala kujali maslahi binafsi bali ya watanzania kwa ujumla wa kizazi hiki na kile kinachokuja. Kupigania kitu chenye uthamani unaozidi fedha na dhahabu na magari, kuacha historia ije iwaenzi vijana walioamua kufanya mabadiliko kwenye nchi yao kwa kukataa kuonewa, kuibiwa na kutumiwa kuwanufaisha wengine na kushiriki kuwaangamiza na kuwanyonya watanzania wenzetu wasio na fursa ya kujiongelea wenyewe. Naomba niwe muwazi na kusema mfumo wa utawala uliopo hauwezi na wala siamini kama unaweza kuleta mabadiliko chanya katika nchi yetu kwa sababu zifuatazo:

a. Hakuna kitu ambacho imeshindwa kufanya ndani ya ya miaka 50 ya kutawala kinaweza kufanywa leo. Hakuna kilichobadilika ndani ya uongozi wake, sera zake, mitazamo yake, malengo yake na katika hali kama hiyo vitu hudumaa. Mwalimu Nyerere aliitawala Tanzania kwa miaka 24 mpaka mwaka 1985 alipoachia madaraka hayo huku akisema, " siwezi kufanikisha chochote ndani ya miaka mitano au kumi ijayo au muda wangu uliobaki wa kuishi, kile ambacho nilishindwa kukifanikisha katika miaka yote hii niliyoiongoza Tanzania" Huu ndio unatakiwa kuwa mtazamo wa Chama tawala na ni dalili ya upevukaji wa kisiasa.

b. Majaribio ya kuleta mabadiliko binafsi tu yameshindikana. Mfano mzuri ni dhana ya kujivua gamba ambapo tulielezwa na viongozi wa CCM kuwa ni kuwaondoa viongozi watuhumiwa wa rushwa ndani ya chama. Wote mnajua jinsi jitihada hizi zilivyozikwa Dodoma na sasa wale watuhumiwa waliokuwa wanasemwa na CCM wenyewe na kutaka wajiuzulu ndio waliochaguliwa kwa kishindo CCM. Kamwe huwezi kutegemea mabadiliko katika hali ya aina hii.
c. CCM bado wameshindwa kudhibiti rushwa hata ndani ya chama. Tumesikia majuzi malalamiko kutoka kwa wana CCM wenyewe jinsi chaguzi zilivyogubikwa na rushwa. Kama viongozi wa CCM wanatafuta uongozi kwa rushwa, hizo hela wamezipataje? je, watazirudishaje?maana hakuna investment bila output!! Na Je, nia yao ya kutafuta uongozi ni nini? Nadhani majibu unaweza kujipa mwenyewe.
d. Watawala wa leo hawana imani kuwa mambo makubwa yanaweza kufanyika. Nchi haiwezi kusonga mbele bila malengo makubwa. Wamarekani walienda mwezini kwasababu kiongozi mmoja alithubutu. Kuna baadhi ya vingozi walituambia wakati wa kampeni kuwa kuwapa raia nyumba bora haiwezekani tuendelee kuishi kwenye tembe, kujilisha na kujitegemea haiwezekani lazima tukapige magoti kuomba chakula,kujenga reli na treni za kwenda kasi kuzunguka Tanzania haiwezekani, maana sisi ni masikini wakati tuna rasilimali nyingi kupita nchi nyingi tajiri; kusomesha vijana na kuwapa elimu bora bure na mikopo kwa wahitaji haiwezekani, wakati viongozi wetu wanatumia mamilioni kusafiri nchi za nje kila mara;wanatembelea magari ya thamani, kulipana posho za vikao bila sababu. 
Kwanini tunajipongeza kabla ya kufanya kazi, wachache mnalia kivulini bila hata kuchumia juani? Mtanzania atumikiwe kwanza, kisha mkajipongeze kwa kufanya wajibu wenu. Kuwa kiongozi si kuwa mfalme bali ni mtumishi wa watu. 
Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha mwisho, Uongozi wetu na hatma ya Tanzania, anasema;"Hakuna kitu cha thamani kinachopatikana bila gharama" Anasema kupata viongozi bora nchi hii lazima tuwe tayari kulipa gharama, na huu ni wajibu wa kila kijana, vijana tuamke, tutoke kwenye mistari ya pambizo, tuinue sauti zetu, turudishe thamani ya nchi yetu, vijana tujiandae, tuamke wote tuchague mabadiliko.Namalizia kwa kunukuu maneno ya Mwalimu; "IT CAN BE DONE, PLAY YOUR PART"

Asanteni sana kwa kunisikiliza.Ester anapatikana kwa namba: 0655048797

2012/10/14 Magiri paul <kiganyi@gmail.com>
. UKOMBOZI WA MTANZANIA
Dhana ya ukombozi wa mtanzania ilianza tangia wakati wa ukoloni tukiwa bado tunatawaliwa na wazungu. Historia ya ukombozi wa Taifa letu inaanzia nyuma sana, enzi za mababu zetu, akina Mkwawa, Mirambo, Mangi Sina na wengine wengi. Mashujaa hawa walipigania uhuru wa Taifa hili na kuupinga ukoloni na ubeberu, hata kuwa tayari kuifia nchi yao.Mwalimu Nyerere aliendeleza historia ya ukombozi kwa kupinga kwa nguvu zake zote ukoloni na ubeberu mpaka tukafanikiwa kujitawala mwaka 1961. Baada ya uhuru, agenda kubwa ya Taifa ilikuwa ni kujitawala na kujiletea maendeleo yetu.Vijana tunajifunza nini kutoka kwa kizazi cha kina Mkwawa? Walipigana na ukoloni hadi kujitoa maisha yao kwa ajili tu ya Ukombozi; yaani walijitoa sadaka. Halikadhalika, kizazi cha mashujaa wasiotetereka, cha Mwalimu Nyerere, kilipambana kutafuta uhuru wa mtanzania na kufanikiwa kuweka misingi ya ujenzi wa Taifa letu. Hawa mashujaa wote walijitoa sadaka. "They sacrificed their lives for the people of Tanzania".
http://wotepamoja.com/archives/8692#.UHqlcWXLZXg.gmail

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment