Thursday 13 September 2012

[wanabidii] Neno La Leo: Ukimwona Mtu Tajiri, Tamani Kuwa Kama Yeye, Na Ukimwona Masikini...

Ndugu zangu,

JAMBO moja kubwa ni dhahiri, kuwa Watanzania bado tuna safari ndefu sana kufikia hatua ya kuitwa taifa la kisasa.



Tuyafanyayo mengi bado ni mambo ya hovyo hovyo, na wenye kuongoza kuyafanya hayo ya hovyo hovyo ni viongozi wetu. Lakini hatuna jinsi, hatua tunayopitia sasa ni lazima tuipitie. Hakuna njia nyingine ya kupita na kutufikisha kwa haraka tunakotaka kwenda. Tusisahau tu , kutunza kumbukumbu. Tufanye hivyo ili Watanzania wa vizazi vijavyo waje wajifunze kutokana na matendo yetu.



Tulikuliku ni aina ya ndege. Viongozi wetu wanaweza kujifunza kutoka kwa ndege huyu. Tulikuliku ana kanuni inayomwongoza. Mara ile tulikuliku anapotaga mayai, basi, hufanya maamuzi magumu ya kujinyonyoa manyoya yake.

Kwa pamoja, tulikuliku dume na jike watafanya tendo hilo.

Kwanini?

Wanajiwekea wenyewe mazingira ya kushindwa kuruka. Wanafanya hivyo ili waatamie mayai yao hata atakapotokea nyoka mpenda mayai wapambane nae hapo hapo. Kwamba wangebaki na manyoya, huenda wangemwogopa nyoka. Hivyo, wangeruka na kuacha mayai yakiliwa na nyoka.


Kwa kiongozi kujinyonyoa manyoya ina maana ya kukubali kushuka chini kwa watu. Kuyaelewa matatizo ya watu anaowaongoza. Kuwa tayari kupambana kuyatatua matatizo ya watu akiwa na watu.



Ilivyo kwa viongozi wetu wengi wa leo, ni kuwa, katikati ya dhiki kubwa ya wanaowaongoza, si tu wamefuga manyoya mengi, bali, hata pale wananchi wanapokabiliwa na adui maradhi, wao, viongozi, wana mbawa za kuwawezesha kuruka juu angani huku wakiwaimbia watu wao nyimbo za kejeli. Na bado watafanya hila ili kuwachonganisha na kuwagawa watu wao walio kwenye dhahma ya umasikini.


Na kuna mawili ambayo yaliwezekana kutumiwa na yakafanya kazi miaka ya sitini hadi themanini, na mawili hayo hata yanapotumika sasa, hayafanyi kazi tarajiwa. Maana, wakati umebadilika. Ni yepi hayo?


Naam, ni kwa kiongozi kutumia Uongo na kutishia nguvu za mamlaka. Kiongozi anayetaka kufanikiwa katika zama hizi ni yule aliye tayari na kuachama na mambo ya zama hizo; kuwaongopea watu wako na kutishia nguvu za mamlaka. Badala yake, kuwa tayari kufanya maongezi hata na wale ambao huko nyuma haikuwezekana kukaa nao meza moja.



Vinginevyo, Watanzania tungali na safari ndefu sana. Njia ina miba mingi, lakini ni lazima tuipite. Hakuna njia nyingine.


Nilipata kuandika, kuwa kwenye Uchina ya kale kulikuwa na mwanafalsafa kwa jina la Comfucius. Katika mafundisho yake mengi aliyopata kumpa mwanafunzi wake Tzu Kung, mojawapo linahusu dhana ya utajiri na mahusiano yake na umasikini.


Comfucius anasema; ukimwona mtu tajiri(aliyefanikiwa kimaisha),basi tamani kuwa kama yeye, lakini, ukimwona aliye masikini, basi, jitafakari wewe mwenyewe.


Kwa mwanafalsafa Comfucius, dhana ya utajiri haikuwa na maana kuwa na mali pekee, bali, pamoja nazo, ni uwezo wa mtu kuishi maisha adilifu na yenye fadhila (virtues). Na katika fadhila zote, ile ya unyenyekevu na ukweli ndio chanzo cha fadhila nyingine zote.


Umasikini vilevile, yumkini unaweza kuwa na maana ya kukosa mali na uadilifu. Ndio, mwanadamu waweza kuwa na mali lakini ukakosa uadilifu. Ni dhahiri, katika hali hiyo, hata mwenye mali naye ni masikini sana.


Kuna kitu kinatokea katika jamii yetu. Wengine wanakiona, wengine hawakioni. Wengine wanakiona lakini hawataki kukiona. Na kuna wanaoonyeshwa , lakini wanashindwa kukiona. Tunafanyaje?
Hakuna kitu kingine bali ni watu ndio wenye kuifanya nchi. Kuna kitu kimetutokea waTanzania. Kinaendelea kuota mizizi. Na kwa vile kitu ndicho hufanya vitu, basi, mimi naviona vitu vya hovyo hovyo vikitokea katika jamii yetu. Na pengine, kwa vile tumeanza kuwa na hulka za hovyo hovyo, basi, vinavyotokea hatuvioni kuwa ni vya hovyo hovyo.


Naam, vinatokea kila leo, na kuna wenye kusimama kuvitetea vitu hivyo vya hovyo hovyo. Ni kuanzia namna tunavyouza rasilimali zetu. Na wenye kuuza, ni viongozi wetu waliogeuka ' madalali' wa kutanguliza tenipasenti. Hawa wa kundi la pili ndio matajiri wetu wapya . Ni watu waliopungukiwa chembe nyingi za uadilifu, hivyo basi, nao ni masikini.


Na tumeimbiwa sana, kuwa nchi yetu ni masikini (japo wanamaanisha kipato pekee). Wenye kutuimbisha wanasahau, au labda hawajui, kuwa sisi ni masikini zaidi kwenye maadili.


Ndugu zangu,


Katika wakati huu tunaoenda nao, na tujifunze kutoka kwa mwanafalsafa Comfucius. Kwamba katika umasikini wetu huu kama taifa, basi, walau tujitahidi kujitafakari tulivyo huku tukiwaangalia wenzetu waliopiga na wanaondelea kupiga hatua za mafanikio ya kiuchumi.



Maana, nasi tutamani kuwa taifa la kisasa. Lakini hatuwezi kuwa taifa la kisasa kwa staili hii tunayoenda nayo. Oneni kule Marekani. Hawa ni matajiri wa kipato. Wanafanya kazi usiku na mchana kutimiza ndoto ya taifa lao. WaMarekani wanaijua ndoto yao na huungana dhidi ya yeyote anayetaka kuikwamisha. Na pengine ni katika kutimiza ndoto hiyo sisi tunalalamika kuwa Marekani ni taifa baya.


Tujiulize; ni taifa gani litaishi bila kuwa na ndoto na haja ya kuwa na maslahi ya kudumu? Hivi, ni nini ndoto na maslahi ya kudumu ya Tanzania? Je, ni WaTanzania wangapi wakiwemo viongozi wanaijua sera ya Tanzania inapohusu uhusiano wake na mataifa mengine?

Na hilo ni Neno La Leo:
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam
13, Septemba, 2011
http://mjengwablog.com

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment