Saturday 8 September 2012

[wanabidii] CHADEMA WAITISHA KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI KUU




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama, Mheshimiwa Freeman Mbowe, itakutana tarehe 9/9/2012 katika kikao cha dharura, kujadili hali ya siasa nchini, kufuatia mfululizo wa matukio ya mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwenye shughuli halali (kwa mujibu wa katiba ya nchi) za chama na njama za CCM na baadhi ya viongozi wa Serikali kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa mbinu haramu.


Itakumbukwa hivi karibuni baada ya mauaji ya Ndugu Ali Singano (Zona) mjini Morogoro, yaliyosababishwa na Jeshi la Polisi mkoani humo wakati walipoingilia kwa nia ya kuvuruga mapokezi na mkutano wa CHADEMA, chama kilitoa kauli kumtaka Rais Jakaya Kikwete aagize kutumika kwa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) ili kubaini chanzo na kuondoa utata wa kifo cha kijana huyo.


Hivi karibuni, baada ya mauaji ya mwandishi wa habari wa Channel Ten na Magic FM, Ndugu Daudi Mwangosi, CHADEMA kilitoa tamko kumtaka Rais Kikwete, aagize kufanyika uchunguzi huru kupitia tume ya kimahakama. Kwani katika tukio hilo hakukuwa na utata kuwa mwandishi huyo aliuwawa na polisi. Hivyo uchunguzi huru ulihitajika ili kubaini vitu vya ziada, kama vile kwa nini kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa katiba, haki za binadamu na sheria za nchi na nani alitoa amri za mauaji hayo.


Itakumbukwa pia kuwa CHADEMA kilipinga kuundwa kwa kamati ya kuchunguza tukio la kuuwawa kwa Mwangosi, iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, kwa sababu iliundwa kinyume cha sheria ya tume za uchunguzi, ikiwa na lengo la kufunika mambo na kurejesha uhusiano wa serikali na vyombo vya habari, badala ya kutafuta ukweli. Kwa mara nyingine tena kilimtaka Rais Kikwete aunde tume huru ya uchunguzi kwa mujibu wa sheria ili kweli tupu ijulikane.


Wakati chama kikitangaza kuahirisha kwa muda mikutano ya Operesheni Sangara-Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), mjini Iringa, kilisisitiza kauli yake ya kumtaka Rais Kikwete kuingilia kati kuhakikisha analinda katiba ya nchi inayotambua haki ya kuishi, kwa kagiza uchunguzi huru ufanyike ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuzuia hali hii ya vyombo vya dola kufanya mauaji ikiwa na lengo la kutisha wapinzani na wakosoaji wa serikali ya CCM.


Kutokana na ukimya wa Rais Kikwete katika matukio hayo na mengine ya namna hiyo ambapo raia wasiokuwa na hatia wametekwa, kuteswa na kuuwawa na vyombo vya dola au wakiwa mikononi mwa vyombo hivyo, CHADEMA kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kujadili hali hii, kisha kufanya maamuzi ya hatua zaidi za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi na Serikali inayoongozwa na CCM, kwa manufaa ya taifa letu na Watanzania wote kwa ujumla.


Imetolewa leo 8 Septemba, 2012 na;

Tumaini Makene,

Ofisa Habari wa CHADEMA;

Kurugenzi ya Habari na Uenezi;

Makao Makuu ya CHADEMA, Dar es Salaam

 



--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment