Saturday 8 September 2012

[wanabidii] Binti yangu kasingiziwa kufaulu darasa la saba

Niliamka Jumamosi ya tarehe 8 mwezi wa tisa ya mwaka 2012 salama
salimini na ikanibidi nielekee kijijini kidogo kuangalia mipaka ya
baadhi ya mashamba ya urithi. Si unaju tena sie wa Pwani wazee wetu
wanatuachia Mikorosho, minazi, miembe na michungwa.

Wapo wanaosema aha aha hii nchi tajiri sijui kuna dhahabu, almasi,
Tanzanite aha mie nasema si kweli maana hadi leo hii siijui ata
rangi ya hiyo almasi na Tanzanite. Mie najua embe dodo likoje
madafu aha usiseme mananasi ata likiwa halijakomaa nakwambia. Hii
nchi ya utajiri wa embe, madafu na mananasi. Siwezi kujinasibu
aha Tanzania tajiri kwa kitu nisichokijua ata rangi yake. Najua
nikienda shambani angalau ninaweza kupata madafu mawili matatu, hiyo
ndiyo Tanzania.

Nilianza safari yangu mapema kidogo, kama ujuavyo mashamba yenyewe ya
urithi yako mbali kidogo na ukitegemea unatakiwa kutembela umbali
mrefu kwa miguuu kwani ata pikipiki hizo ambao ndiyo usafiri wa
kutegemea unaishia katika baadhi ya maeneo.

Nilifika kijiji chetu nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam saa saba
mchana huku nikiwaona waumini wakitoka kuswali sala ya alasiri.
Nilikaribishwa na taarifa kutoka kwa jirani yangu katika eneo hilo
juu ya mgogoro kati ya mtendaji wa kijiji na Mwananchi mmoja ambaye
amekusudia kuifunguliakesi idara ya elimu ya Wilaya ya Mkuranga
kwa kumdanganya kuwa binti yake alifaulu kidato cha kwanza wakati si
kweli.

Nilivutiwa na habari hiyo ikanibidi niombe maji ya kunywa. Mke wa
jirani aliniletea maji kutoka mtungini katika chombo maalumu
kiitwacho kata kilichotengenezwa kwa kifuuu cha nazi na kupachikwa
mti mrefu ndani yake. Nikanywa maji hayo.Namaliza kumeza fundo la
mwisho la maji tu akafika jirani yangu kwa salamu kubwa alaa alwatan
Shekhe Makwega habari za siku tele? Nikamjibu njema tupo tumekuja
kwetu!

Bila kuchelewa niliomba nipewe habari ya kufaulu kwa binti yetu. Si
unajua tena mtu anyimwi neon, pesa utanyimwa. Nilianza kusimuliwa.
Mara baada ya kufanywa mtihani wa darasa la saba mwishoni mwa mwaka
jana nilipata barua kutoka huko Mkuranga kuwa binti yangu alikuwa
miongoni mwa waliofaulu. Nikasema Shekhe Hongera sana.

Basi anasema alipokea fomu maalumu kutoka sekondari kuwa binti yake
kafaulu kwenda kidato cha kwanza.Basi jirani alimpa taarifa hiyo mkewe
wakaamua waangalie kibindoni kuna nini. Si unajua tena, hamadi
Kibindoni Yakhe!Kulikutwa laki tatu. Akaweka mfukoni akamwambia
binti yake avae nguo zake za shule ya msingi na mguu kwa mguu
hadi shule ya msingi aliyosoma.

Jirani akafika shuleni hapo na kuwakuta walimu wamejaa tele
wakijipongeza kwa kuweza kufaulisha watoto wengi kwa mwaka
2011."Nikasema ninamuomba mwalimu Mkuu nina shida kidogo,"anasema
jirani yangu.


Mguu kwa mguu hadi ofisini kwa mwalimu mkuu.Tulipofika nikamwambia
mwalimu huyu ni binti yangu alikuwa anasoma hapa na ni miongoni mwa
wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza.

"Naam na mwaka huu tu tumefaulisha wote." Alisema kwa kujigamba
Mwalimu Mkubwa. Basi jirani akamwaambia sasa ninaomba unikusanyie
alama zote za mwanangu wakati akiwa darasa la saba ili nijue alikuwa
na maendeleo gani maana ninachoelewa mimi siyo hicho mlichoandika
humu.

Basi mwalimu mkuu akawaomba walimu wafanye kazi hiyo baada ya muda
wakaja na ripoti kuwa kwa mwaka 2011 binti hiyo alikuwa na alama
zisizozidi 100 kwa darasa la saba lote.

Mzazi akawauliza sasa mbona nimeambiwa kuwa binti yangu amefaulu kwa
uwezo gani?Mwalimu yule akamwambia kama kuna swali zaidi basi aende
hadi katika shule husika ya sekondari atapata majibu zaidi au kwa
wakubwa wa elimu.Maana wao wana fomu inyaoitwa TSM 9 ambayo
inaonyesha alama zote za mtoto akiwa darasa la saba.

Mzazi akafunga safari hadi shule ya kata husika akawafuata walimu wa
shule hiyo na kuwambia kuwa mwanagu mmemsingizia kuwa amefaulu
lakini mimi mzazi nasema mwanangu hajafaulu sasa sitamleta shule
kama kuna mahakama mwende mimi nipo Mlamleni. Sasa ni mwezi wa tisa
hakuna afisa elimu wala karani wa mahakama aliyepiga hodi nyumbani
kwa jirani yangu, zaidi ya kuulizwa na mtendaji wa kijiji tu na tena
kwa utani. .

Jirani amenidokeza kuwa kwa tathmini yake binti yake hawezi
kufaulu mitihani wa darasa la saba bali wamemsingizia. Kwa kufanya
hivyo ni kosa na anasema yeye amesoma hadi darasa la nne la
mkoloni."Mimi ninajua huyo mtoto si wa kufaulu yeye ni wa kufeli,"
anasema jirani.

Nilimuuliza sasa binti yetu anafanya nini ?alinijibu, nimemnunulia
cherehani na amempeleka kwa fundi kujifunza ushonaji huko Mbagala
Kuu lakini akitokea kijana anayetaka kumposa atampa binti yake bure
bila posa na ile charahani aliyomnunulia atawapa waende nayo kuanzia
maisha.

Kwa kujinasibu anasema mpaka leo hakuna serikali wala mahakama
iliyosubutu kumuita kwa kumkataza binti yake kusoma."Shekhe
waliofaulu kihalali wanaenda shule zenye mantiki." Anasema.
Wakinigusa tu nitawafungulia mashitaka kwa kuwadanga watu kuwa watoto
wao wamefaulu katika shule za kata wakati si kweli.

Mwsho

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.

0 comments:

Post a Comment