Sunday 26 August 2012

[wanabidii] Neno La Leo: Nilishaamua, Nitabaki Kuwa Mjamaa...

Ndugu zangu,

Kwa siku mbili mfululizo nilikuwa kijijini Mahango, Kata ya Madibira, Mbarali, Mbeya. Huko niliongozana na wageni kutoka Uingereza waliokwenda kushiriki kazi ya ujenzi wa Maktaba ya Kijamii kijijini Mahango.
Uzoefu nilioupata kijijini Mahango ni elimu yenye gharama kubwa. Hakika nimejifunza mambo mengi. Kijijini Mahango niliuona kwa karibu sana umasikini wa watu wetu. Kwa mfano, kwenye moja ya kitongoji nilimshuhudia mama anayelindia maji kwenye kisima chenye chemchemi yenye kutoa maji ya kujaa bakuli moja kila baada ya robo saa.

Mama yule kwa kauli yake alitamka huku akiwa ameshika tama; " Hali yetu ni mbaya sana, hapa ndoo moja kujaa inaweza kunichukua saa moja na nusu". Wakati akitamka hayo nilimwona binti wa mama huyo asiyezidi miaka kumi akiwa amesimama akimwangalia mama yake. Niliziona pia ndoo zilizopanga foleni bila wenye nazo. Bila shaka wamekwenda kujihifadhi na jua kali la mchana, na kufanya kazi nyingine pia.

Hali kama hiyo niliikuta pia kijijini Mapogolo. Kwenye ofisi ya Mtendaji Kata ya Miyombweni kilipo kijiji cha Mapogolo nilifanya mazungumzo na Diwani wa Kata Bw. Lokelo pamoja na  Mtendaji wa Kata Bw. Filipo. Nao  wakawa wamekunja mikono wasijue la kufanya, maana, bajeti ya Halmashauri ya kushughulikia na tatizo la maji haitoi matumaini ya kutatua tatizo la wananchi katika muda mfupi ujao. Fedha hazitoshi.

Kwenye Mkutano wa hadhara kijijini Mahango, Mwenyekiti wa Kijiji  alinipa nafasi adimu ya kuzungumza machache na wananchi. Nilisimama na kuwaangalia wananchi wale walioonyesha kwenye nyuso zao, kiu ya kutaka kunisikiliza; niliwaangalia akina mama na watoto migongoni, niliwaangalia watoto wale waliokaa mbele yangu. Niliwaangalia akina baba na vijana. Kwa jinsi watu walivyoitikia wito wa kukusanyika kushiriki kazi ya ujenzi wa Maktaba, kushiriki jambo la elimu, basi, nami niliyaona matumaini kwenye kusanyiko lile.

" Mahango Oyee!"
Nilitamka na nikaitikiwa kwa sauti kubwa. Haraka nikaamua niongelee umuhimu wa Ujamaa na Kujitegemea; kufanya kazi kwa ushirikiano. Nikaanza hotuba yangu fupi kwa kumnukuu Mwanafalsafa David Hume kwa maneno yake haya;

"MBEGU yako imekomaa leo, yangu itakomaa kesho. Ni jambo la manufaa kwetu sote kama  nitalima pamoja nawe leo, na wewe unisaidie kulima kesho. Siwezi kuwa na urafiki nawe kama naona kuwa hujengi urafiki nami. Msimu utapita, nasi tusipoaminiana na kushirikiana, basi, sote tutakula hasara."  (Mwanafalsafa David Hume)

Nikasisitiza pia umuhimu wa kuzingatia 'K' tatu ili kufanikiwa katika tuyafanyayo; Kujitambua, Kujiamini na Kuthubutu.  Pale Mahango nikasisitiza pia umuhimu wa kuitanguliza Tanzania kwanza katika yote tuyafanyayo. Tusiendekeze sana tofauti zetu za kisiasa. Tuwajue maadui tunaopambana nao, tuyajue malengo yetu kwenye vita iliyo mbele yetu. Tukubaliane kupambana kwa pamoja kwa maana ya kufanya kazi kwa pamoja ili kuyafikia malengo yetu.

Maana, hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hatima yetu kama watu binafsi, kama vikundi vya watu na kama taifa, inatutegemea sisi wenyewe. Umasikini wa watu wetu ni umasikini wetu.
Naam, sijawahi kuficha imani yangu ya kisiasa, kwa maana ya itikadi yangu.  Na imani yangu inaimarika zaidi kadri ninavyozidi kutembelea na kukutana na watu wa vijijini.

 Kiitikadi mimi ni Mjamaa ninayeamini katika uwepo wa demokrasia na kutanguliza maslahi ya walio wengi katika jamii-   I am a  Social Democrat.  Na bado naamini kuwa hata sasa, mfumo  wa enzi za Mwalimu wa Ujamaa na Kujitegemea bado una nafasi katika jamii yetu.  Misingi ya Ujamaa na Kujitegemea bado ni muhimili wa maendeleo ya nchi na watu wake. Ni udhaifu na kutokujiamini kwa kuionea haya misingi iliyoijenga jamii yetu na ambayo bado ina nafasi ya kuifanya nchi yetu kuwa ya kisasa zaidi kama itaimarishwa.

Maana, mfumo wa Ujamaa na Kujitegemea uliofanyiwa mabadiliko ya kimsingi unaweza kutuhakikishia ulinzi wa maslahi ya nchi yetu. Ni kwa sera zenye kuhakikisha usawa wa watu. Sera zitakazohakikisha kodi inakusanywa na kutumika katika yaliyo muhimu na yenye kumsaidia pia mwananchi wa chini katika nchi yetu. Mwananchi aweze kupata elimu bora na huduma bora za afya, maji, miundo mbinu  kati ya mengineyo ya msingi.

Tuazimie sasa kuwajibika kwa pamoja kwa maslahi ya nchi yetu. Na tukifanya ajizi, tutaigeuza nchi yetu kuwa ' nyumba ya njaa'.  
Naam, Nilishaamua nitabaki  kuwa Mjamaa.
Na hilo ndilo Neno La Leo.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765
http://mjengwablog.com

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment