Sunday 26 August 2012

[wanabidii] KWANINI WAISLAMU HAWANA IMANI NA VITENGO VINAVYOHUSIKA NA TAKWIMU?

Hili ni suala muhimu kulipatia jibu na kulifahamu kwa kina sisi kama Waislamu. Wengi wana maoni kuwa kitendo cha Waislamu kuomba kushirikishwa katika Sensa na kuomba kuingizwa kwa swali la Dini ni ukorofi tu wa Waislamu. Ukweli unafichwa na makala hii ina lengo la kuwajuza watu vipengele kadhaa juu ya hila katika sensa zilizopita.

Makala hii itadhihisha "uchakachuaji uliofanyika na ofisi za serikali katika kutangaza mgawanyiko wa watu kwa mujibu wa dini kabla ya serikali ya Mwalimu Nyerere kuamua kulifuta swali la dini katika sensa ya Tanzania iliyofanyika mwaka 1978.

Tanganyika au Tanzania imeshafanya sensa mara 6. Mara mbili za mwanzo sensa ilifanyika kama Tanganyika chini ya mkoloni wa Kiingereza yaani mwaka 1948 na mwaka 1957. Kisha sensa nne zilizobaki zilifanyika Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zikiwa zimeshaungana. Sensa ya mwanzo ya Tanzania huru iliyoungana iifanyika mwaka 1967 na hii ilikuwa ni sensa ya mwisho kuuliza swali la dini. Sensa zilizobaki zilifanyika mwaka 1978, 1988 na 2002. Sensa ya mwaka huu, 2012 itakuwa ni ya saba katika historia ya nchi yetu na ya tano ya Tanzania huru iliyoungana. 

Sensa ya mwisho ya Tanganyika chini ya mkoloni wa Kiingereza katika mwaka 1957 ilionyesha kuwa Tanganyika ina Waislamu 58%, Wakristo 32% na Wapagani 10%. Uwiano kati ya Waislamu na Wakristo ilikuwa ni karibu 2:1 yaani kila penye watu watatu, 2 ni Waislamu na 1 ni mkristo, vile vile unaweza kusema waislamu walikuwa ni karibu mara mbili ya wakristo kiidadi Tanzania. 

Mwaka 1967 ndio uliotoa matokeo ya ajabu ambayo mpaka leo sio tu Waislamu bali mtu yoyote aliye na akili timamu ana haki ya kuhoji matokeo hayo. Matokeo haya yalionyesha mgawanyiko wa kidini kama ifuatavyo:

WAKRISTO: 33.5% yaani wameongezeka kwa 1.5% kulinganisha na sensa ya 1957.

WAISLAMU: 31.4% yaani wamepungua kwa 26.6% katika kipindi cha miaka 10 tu. Hii haikuwahi kutokea sehemu yoyote Duniani iwapo sehemu hiyo haikukabiliwa na janga kama vile vita au jambo lolote lilisababisha idadi kubwa ya watu kufariki. Hata china ambayo imeweka sheria ya kuzaa mtoto mmoja tu basi haikuwahi kupungikiwa na watu au kundi fulani la watu katika nchi yao. 

WAPAGANI: 34.3% yaani wameongezeka kwa 24.3% kwa kipindi cha miaka 10. Haya nayo ni maajabu, yaani unaweza ukadhani labda Tanzania ina tatizo la Waislamu kuwacha dini yao na kuwa wapagani. Hili nalo halina ushahidi wowote kuwa lilitokea katika kipindi hicho. 

Athari kubwa ya kimabadiliko iliyotekea katika sensa hii ni kujumuishwa kwa Wazanzibari katika sensa kwa mara ya kwanza. Kwa vile Wazanzibari karibu 98% ni Waislamu tegemeo lilikuwa Waislamu Tanzania wapindukie angalau 65% (kutoka 58% ya mwaka 57 ambayo haikujumuisha Wazanzibari) ya watu wote lakini badala yake wakashuka hadi 31.4% 

Tukumbuke kuwa Waislamu ndio watu ambao mara nyingi hulaumiwa kutofuata uzazi wa majira, hulaumiwa kwa kuozesha mabinti zao mapema na ni dini inayoruhusu mume mmoja kuoa wake wanne, haya yote hupelekea ongezeko kubwa la idadi, lakini ajabu ni kuwa Waislamu walipungua, si kwa asilimia 2 - 3% bali kwa 26.6%!

Hivyo ni wazi Takwimu zilizotolewa na serikali ya Mwalimu Nyerere ama zilikuwa ni za uongo wa makusudi ya kupotosha au zina makosa. Lakini cha kushangaza ni kuwa baada ya sensa hiyo Serikali ya Mwalimu Nyerere iliamrisha kipengele cha dini kuenguliwa kwenye sensa bila ya kueleza Watanzania lengo la kukiondoa kipengele hicho. wakati huo tayari Tanzania ilishaanza kugubikwa na wingu la udini baada ya Mwalimu Nyerere kuamua kuivunja Jumuiya adhimu ya Waislamu East Africa Muslim Walfare Society (EAMWS) na serikali kuunda Jumuiya ambayo mpaka leo waislamu wana mashaka nayo ambayo ni BAKWATA. Naomba sana tuzingatie nukta hii kuwa BAKWATA haikuundwa na Waislamu bali iliundwa na Serikali iliyoongozwa na Mwalimu Nyerere. 

Kudhihirishwa kuwa mwaka 1967 udini ndio ulikuwa unaanza kushamiri Tanzania sio tu katika sensa na kuvunjwa kwa EAMWS na kuundwa kwa BAKWATA, mwaka 1967 ndio mwaka wa Azimio la Arusha na mwaka wa kesi ya uhaini iliyojumuisha Waislamu na wengi wakawekwa rumande kwa tuhuma hizo akiwemo wanasiasa maarufu ambao waliiunga mkono EAMWS akina marehemu Bibi Titi Muhammed na Tewa Said Tewa. 

Hivyo leo utaweza je kuwalaumu Waislamu kwa kukosa imani na serikali katika hoja ya sensa? Mara nyingi panapotokea badiliko kubwa kama lile ambalo linaaminika kuwa ni la kuchakachuliwa yaani Waislamu kupungua Tanzania kwa 26.6% na wapagani kuongezeka Tanzania kwa 24.3 katika kipindi cha miaka 10 (jambo ambalo mtaalamu yoyote wa sensa au takwimu hawezi kukubaliana nalo) palitegemwa pfanyike utafiti wa sababu za mabadiliko hayo, lakini hakuna aliyeamua kufanya hivyo na sababu kuu ni kuwa watu walijua wazi kuwa takwimu hizo ni za kupika. 
Source: Mapara
Na Ndugu Mohamed Said  anaandika  juu ya KITENDAWILI CHA SENSA TANZANIA na anaelezea kuwa:
Theluthi mbili ya Waislam wote wa Afrika ya Mashariki wanaishi Tanzania mbayo ndiyo nchi yenye watu wengi kuliko zote katika Afrika ya Mashariki, yaani Kenya, Uganda na Tanzania. Hii ni pamoja na nchi ya Kiislam yenye Waislam takriban 90% na kuna wakati ilikuwa ndiyo kitovu cha maarifa ya Kiislam katika Afrika ya Mashariki na Kati. Kutokana na sensa ya mwaka 1957, kwa kila Waislam watatu walikuwepo Wakristo wawili. Kwa wakati ule hii ilionyesha kuwa Tanganyika ilikuwa na Waislam wengi katika nchi zote Kusini ya Ikweta. Lakini katika sensa ya kwanza mwaka 1967 baada ya uhuru jumla ya Wakristo Tanzania Bara ilikuwa asilimia 32 % na Waislam 30% Wapagani asilimia 37%. Sensa hii inaonyesha kuwa Wapagani ndiyo walio wengi Tanzania. Sensa hii ya mwaka 1967 haikueleza kwa nini katika kipindi cha miaka kumi kwa ghafla Waislam wamepungua nchini au kwa nini ghafla Wapagani wameongozeka katika nchi ya waumini. Hii ndiyo ilikuwa sensa ya mwisho iliyokuwa ikionyesha mgawanyo wa dini. Inaaminika kuwa matokeo ya sensa hii yalifanyiwa mabadiliko kwa ajili ya sababu za kisiasa pale ilipobainika kuwa Waislam Tanzania walikuwa wengi kupita Wakristo. Upo ushahidi kuwa mwaka 1970, ilipobainika kuwa Waislam ni wengi Tanzania serikali iliiamrisha Idara ya Takwimu kuchoma moto matokeo yote ya sensa ya mwaka 1970. Si tabu kwa hivi leo kutambua ni nani walitoa amri hii na kwa sababu zipi. Bahati mbaya mgao wa madaraka katika siasa Tanzania umewatupa nje Waislam, ingawa inafahamika kuwa usalama na utulivu wa nchi yeyote unategemea mizani hii kuwa sawa. Vyanzo tofauti vya takwimu vinatoa takwimu tofauti zinazopingana kuhusu hesabu ya Waislam na Wakristo katika Tanzania. Hii inatokana na ukweli kuwa somo hili limefanywa nyeti na la kutisha sana. Lakini wanaotishwa na hesabu na takwimu za sensa si Waislam bali ni Wakristo na makanisa yao. Katika nchi za Kiafrika ambazo zina wafuasi wengi wa dini hizi mbili, kwa mfano Tanzania na Nigeria, uchunguzi wa kuwa ni dini gani ina wafuasi wengi kupita mwenzake ni chanzo cha mgongano na mzozo. Tatizo hili lipo Tanzania. D.B. Barret anasema kuwa Waislam Tanzania ni wachache wakilinganishwa na Wakristo. Takwimu zake zinaeleza kuwa Waislam ni 26%, Wakristo 45% na Wapagani ni 28%. Takwimu za Tanzania National Demographic Survey za mwaka wa 1973 zinaonyesha kuwa Waislam ni wengi kidogo kupita Wakristo wakiwa 40%, Wakristo 38.9% na Wapagani 21.1%. Lakini takwimu za Africa South of the Sahara, zinaonyesha Waislam ni wengi Tanzania kwa 60%. Takwimu hizi zimebaki hivyo bila ya mabadiliko toka mwaka 1982. Kwa kuwa utafiti wa Waislam wenyewe katika suala hili ni mdogo sana au haupo kabisa, suala la wingi wa Waislam katika Tanzania halijafanyiwa utafiti na Waislam wenyewe. Mgao wa madaraka na kugawana vyeo haikupashwa kuwa sababu ya migongano na mifarakano katika Afrika huru. Lakini kwa bahati mbaya sana hii imekuja kuwa sababu ya mifarakano katika serikali za wananchi wenyewe. Jambo hili limekuwa ni suala nyeti kwa sababu ukabila, udini na kujuana ni kitu muhimu katika serikali za Afrika. Mgawanyo wa madaraka na wingi wa wafuasi katika dini au kabila havikuwa vitu vilivyokuwa vikiwashughulisha wananchi wakati wa ukoloni kiasi cha kuleta mifarakano katika jamii. Kwa bahati nzuri ukabila hauna nguvu Tanzania lakini dini imekuwa chanzo cha ubaguzi toka zama za ukoloni, tofauti ni kuwa wakati wa ukoloni waliokuwa wakiwabagua Waislam hawakuwa Wakristo weusi bali Wazungu. Ukristo ni dini mpya Tanzania kwa kuwa uliingizwa katika karne ya kumi na nane na wamisionari. Kanisa na Mwafrika Mkristo ni matokeo ya ukoloni. Kwa ajili hii basi historia ya Kanisa katika Afrika ni ile ya kushirikiana na kuwa tiifu kwa serikali ya kikoloni. Chini ya ukoloni, taratibu Kanisa likaweza kujenga uhusiano maalum kati yake na serikali pamoja na Mkristo Mwafrika ambae imemuelimisha katika shule zake za misheni. Mwafrika Mkristo akawa ananufaika na mfumo wa kikoloni. Waislam wakawa wanataabika kwa kuwa dini yao ilikuwa inapingana na dini ya mtawala kuanzia Wajerumani hadi Waingereza. Mwafrika Mkristo akawa mnyeyekevu kwa serikali wakati wa ukoloni na baada ya kupatikana kwa uhuru akaja kushika madaraka ya serikali. Waislam wakatengwa na kuteswa katika ukoloni kwa kubaguliwa na kunyimwa elimu hivyo kuwaondolea fursa ya maendeleo. Kuwepo kwa Waislam kama raia na ili kuinusuru dini yao ilibidi Waislam wasimame kuutokomeza ukoloni. Baada ya uhuru Kanisa likabaki na msimamo wake wa enzi ya ukoloni wa kutii na kujipendekeza kwa serikali mpya iliyokuwa madarakani. Ushirika huu kati ya Kanisa na serikali, uliojengwa na tabia ya Kanisa ya kukubaliana na mfumo wowote wa serikali ulililelewa vyema na umeisaidia sana Kanisa. Kanisa likaweza kujijengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zake bila ya kipingamizi wala wasiwasi. Kutokana na uhusiano huu maalum Kanisa likajifanyia msingi imara wenye nguvu kutokana wa Wakristo waliowasomesha katika shule zao. Kanisa likatumia nafasi na uhusiano huu kwanza na serikali ya kikoloni kisha na serikali ya wananchi kujijengea himaya ambayo wafuasi wake wakaja kushika nafasi zote muhimu katika uongozi wa juu wa serikali, bunge na mahakama katika Tanzania. Katika miaka yake mia moja tu Kanisa likaweza kupata safu yake ya viongozi ambao wanadhibiti kila sekta katika jamii ya Watanzania. Waingereza walipokuja kuitawala Tanganyika (kama Tanzania inavyojulikana) baada ya kuondoka Wajerumni baada ya Vita Kuu ya Kwanza, Wajeruamani walikuwa wameshafanya kazi ya kutosha ya kuiweka Tanganyika ndani ya mamlaka mbalimbali za Kikristo. Tanganyika ilikuwa imegawanywa katika mamlaka za Kikristo kutoka nchi tofauti za Ulaya. Kanisa Katoliki ambalo ndilo lenye nguvu zaidi, lilikuwa tayari limeshajikita Tanganyika. White Fathers walikuwa wapo Tabora, Karema, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Bukoba; Holy Ghost Fathers walikuwa Morogoro na Kilimanjaro; Benedictine Fathers walikwepo Peramiho na Ndanda; Capuchin Fathers walikuwepo Dar es Salaam; Consolata Fathers walikuwepo Iringa na Meru; Passionist Fathers walikuwa Dodoma; Pallotine Fathers walikuwa Mbulu; Maryknoll Fathers walikuwapo Musoma; na Rosmillian Fathers walikuwa Iringa. Wamisionari hawa walipotia mguu pwani ya Afrika ya Mashariki, nia yao hasa ilikuwa kuufuta Uislam. Wakazi wa pwani hii iliyokuwa ikijulikana kama Zanj waliuona Ukrsto kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1498 Wareno walipofika sehemu hizo. Mwaka 1567 wamishionari wa Augustinian waliingia Afrika ya Mashariki ili kupambana na Uislam ili Ukristo uwe dini ya dunia nzima. Kadinali Lavigirie alianzisha The White Fathers, taasisi ya Kanisa Katoliki kwa kusudi maalum la kuupiga vita UislamWakati huo huo Church Missionary Society (CMS) ilikuwa imejitwisha kazi ya kuondoa ulimwengu kutokana na Uislam, ujinga na giza. Hadi hii leo White Fathers wapo Tanzania wakiendelea kufanya kazi iliyowaleta Tanganyika zaidi ya miaka mia iliyopita. Wajerumani walipofika Tanganyika waliwakuta Waislam wanafahamu kuandika, kusoma na walikuwa wameelimika katika hesabu. Mmishionari Ludwig Krapf alipofika kwa Chifu Kimweri wa Usambaa mwaka 1848 alimkuta yeye na wanae wote wanajua kusoma. Herufi walizokuwa wakitumia zilikuwa za Kiarabu. Wajerumani kwa ajili hii basi waliwaajiri Waislam kama walimu, wakalimani na makarani serikalini. Wamisionari na wakoloni waliona wivu na nyoyo zao zikaingia hasad kwa maendeleo haya waliyoyakuta kwa Waislam. Kubwa zaidi ni kuwa walikuwa wamekuja kustaarabisha watu "washenzi" badala yake wamewakuta watu waliostaaarabika na wanye utamaduni wa kupendeza. Elimu hii yote na utamaduni huu wa hali ya juu ulikuwa unatokana na Uislam na shule zake zilizojulikana kama madras. Hapo ndipo zilipoaanza mbinu ya kuvunja maendeleo haya yote. Vita vilivyodumu hadi hii leo. Herufi za Kiarabu zikapigwa marufuku kutumika na badala yake watu wakalazimishwa kujifunza herufi za Kirumi. Muislam ambae jana alipoingia kulala alikuwa anaitwa ameelimika akaamka asubuhi yake mjinga, hana elimu, hajui kusoma wala kuandika. Njama hizi zote dhidi ya Uislam ilikuwa sehemu ya makubaliano kama ilivyoandikwa katika kifungu IV cha Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884. Kifungu hicho kilikuwa kinasema kuwa Ukristo ni lazima ulindwe dhidi ya Uislam. Kati ya mwaka 1888-1892 katika kutekeleza kifungu hicho kama ilivyokubalika katia Mkutano wa Berlin, Imperial British East Africa Company ilitumia nguvu za kisiasa na kijeshi kuulinda Ukristo katika Afrika ya Mashariki. Ombwe lililoachwa na elimu ya Kiislam ikajazwa na elimu ya Kanisa chini ya usimamizi wa Waingereza. Kanisa hivi sasa linaeneza uongo na propaganda kuwa lenyewe ndilo lililoweka msingi wa kwanza wa elimu Tanganyika. Ukweli ni kuwa Wamisionari walifuata nyayo za madras na walimu wa kwanza katika shule za misheni walikuwa Waislam ambao hawakusoma katika shule za kanisa bali katika madras. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mia moja Kanisa likaelekeza nguvu zake katika katika kuwatayarisha raia ambao wengi wao walikuwa Wakristo, watakaokuwa watiifu kwa Kanisa na serikali. Ni katika mtandao huu ndiyo Wakristo wanaimiliki serikali na Chama Cha Mapinduzi na kuiamrisha ifanye linavyopenda Kanisa, wakati Waislam na Uislam ukifanywa kama vitu visivyokuwa na maana yoyote. Hadi kufikia mwaka wa 1960 Kanisa likawa taasisi kubwa inayomiliki mamilioni ya dola ya misaada inayopokelewa kutoka wahisani na wafadhili walioko katika ulimwengu wa Kikristo. Kanisa sasa hivi linahodhi mahospitali, misururu ya ndege binafsi, viwanja vya ndege, makampuni ya uchapaji na mitambo ya kupiga chapa, stesheni za radio, tv na magazeti. Kanisa limekuwa na nguvu na udhibiti wa mambo kiasi kwamba wakati mwingine watendaji, hasa Wakristo katika serikali na ndani ya chama tawala CCM hawajui utii wao upo kwa nani, serikalini au katika Kanisa? Ni katika kuchanganyikiwa huku kwa watendaji wa serikali kuhusu uhusiano wao na Kanisa na serikali ndiko kulikoamsha kutoaminiana kati ya Waislam na serikali mara tu baada ya uhuru kupatikana. Serikali ikaonekana kama moja ya taasisi za Kanisa na Waislam wakiwa ni watazamaji tu. Mara baada ya uhuru Kanisa likaangalia nafasi yake na serikali mpya iliyokuwa madarakani. Wakati wa kudai uhuru Kanisa lilijiweka mbali na siasa na ikaonekana kuwa Kanisa lilikuwa likiheshima ule mpaka kati ya dini na siasa. Wakati ule mgongano kati ya Kanisa na serikali haukupata kusikika hata kidogo. Baada ya uhuru kupatikana tu na serikali ikawa mikononi mwa wananchi, Kanisa likaanza kusikika likisema kuwa lina haki na wajibu kuwa na ushawishi ndani ya serikali, kuikosoa serikali na kuingooza pale inapoona serikali haifanyi mambo sawa kwa matarajio yake. Katika msimamo huu mpya, Kanisa likajipa fursa ya kuwa msemaji wa watu. Huu ulikuwa ni mwelekeo mpya katika mambo ya siasa na utawala. Katika Uislam siasa na dini ni kitu kimoja. Vitu hivi viwili havitenganishwi. Lakini mwaka wa 1955 wakati wa siku za mwanzo kabisa za TANU, Waislam katika TANU walivyoweza kukiongoza chama katika misingi ya kisekula na utaifa ili kulinda umoja wa wananchi. Kutochanganya dini na siasa ikawa moja ya maadili makuu ya TANU. Kuanzia hapa ndipo sasa tunaweza kuelewa mapambano kati ya Waislam kwa upande mmoja na serikali na Wakristo kwa upande wa pili yalivyokuja kigubika Tanzania mara baada ya uhuru. (Inatoka katika kita bu "Maisha na Nyakati za Abduliwahid Sykes…"na Mohamed Said, Phoenix Publishers, Nairobi 2002)

Source: Trendinface

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment