Wednesday 22 August 2012

Re: [wanabidii] Na mimi niliandika hivi kuhusu bastola ya Rage

Hatukumbuki. Unaonaje tukikumbushana?

On 22 Aug 2012 11:14, "frank John" <msike24@hotmail.com> wrote:
Unakumbuka comments za Tony PT? Kuhusu picha ya Rage na mguu wa kuku kiunoni?
Sent from my BlackBerry® smartphone from Vodacom

-----Original Message-----
From: Mashaka Mgeta <mgeta2000@yahoo.com>
Date: Wed, 22 Aug 2012 07:51:48
To: <wanabidii@googlegroups.com>
Subject: [wanabidii] Na mimi niliandika hivi kuhusu bastola ya Rage



Septemba 28, 2011, niliandika makala kwenye NIPASHE kupitia safu yangu ya MTAZAMO YAKINIFU inayotoka kila Jumatano, nikikemea kitendo cha Rage kuonekana na bastola kwenye mikutano ya kampeni za Igunga. Wakati nilikuwa kikazi nchini Kenya. Makala yenyewe ni hii hapa chini:-



Amani, utulivu na bastola ya Rage `nje nje`!
Na Mashaka Mgeta
 
28th September 2011
 
Ni tukio la aibu, linalofedhehesha na kustahili kuwekwa kwenye kumbukumbu za viashiria vya ulevi wa madaraka, ukosefu wa maadili na uchafuzi wa kijamii unaofanywa na watawala.
Mbunge wa Tabora Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ismail Aden Rage, ameonekana katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, akiwa na bastola.
Hakuna tasfiri rahisi inayoweza kupatikana kutoka katika picha na dhamira ya Rage kama si ujeuri, vitisho na kuudharau umma.
Ni kitendo kisichostahili kuvumiliwa na mamlaka yoyote ndani ya taifa linalojali na kutekeleza utawala wa sheria, haki na usawa kwa raia wote.
Katika kusanyiko la raia wasiokuwa na hatia, wenye umri wa kuanzia utoto, ujana hadi uzee, wakiwa kwa jinsia za kike na kiume, Rage anajitokeza, anapanda jukwaani huku bastola iliyo maarufu kama 'cha moto' ikionekana kiunoni!
Sijasikia karipio la aina yoyote kutoka kwa mtawala wa ngazi yoyote, zaidi ni 'kuipoza jamii', kwamba atahojiwa ili kupata ukweli wa nia hiyo.
Lakini ni tukio linalomgusa Mbunge kupitia chama tawala ambaye alifikia hatua hiyo mbele ya askari polisi, usalama wa taifa na viongozi kadhaa katika CCM na serikali.
Sikuwepo katika mkutano huo, lakini historia inayotokana na hulka ya 'ulevi wa madaraka', inawezekana Rage alishangiliwa.
Inawezekana washangiliaji walianzia jukwaa kuu, wakafuata `wapambe' waliovalia fulana, kofia ama skafu za njano na kijani, zikiwa na alama ya jembe na nyundo inayotumiwa na CCM.
Inawezekana ilikuwa hivyo kwa maana mkutano ambao Rage aliamua kuonyesha bastola hadharani, uliandaliwa na kuhutubiwa na viongozi wa chama hicho.
Je, Rage alitaka kuujulisha umma kwamba iwe iwavyo, silaha kama hiyo ni sehemu ya nyenzo zinaweza kutumika kufanikisha matokeo ya uchaguzi mdogo wa Igunga?
Je, Rage alitaka kuwasilisha ujumbe ya kwamba, kama alivyojidhihirisha machoni mwa waliohudhuria mkutano huo, 'vigogo' wenzake pia walikuwa wamekamilika hivyo kuwa mfano wa vitisho kwa wapiga kura wa Igunga?
Rage alikusudia nini kuonyesha bastola hadharani! Kwamba angeweza kuifanyia kazi wakati wowote na kwa yeyote aliyekuwepo na ambaye angeonyesha upinzani dhidi ya kauli zake jukwaani?
Hayo ni maswali machache miongoni mwa mengi ambayo yakiorodheshwa kwa ujumla wake, safu hii haitatosha.
Kwa namna iwayo yote, zipo sheria, taratibu na kanuni zinazowaongoza wamiliki wa silaha kama bastola aliyoinyesha Rage, ambapo ninaamini kwamba kuionyesha hadharani si sahihi.
Rage akiwa amevaa shati la rangi ya kijani, lisilokuwa na ufito wa njano (pengine kutokana na uachana wake katika klabu ya mpira wa miguu ya Simba inayotumia rangi nyekundu, ikiwa ni mpinzani wa Yanga inayotumia rangi ya njano), ameonyesha `jeuri' ya kumiliki bastola.
Hakuguswa, hakukamatwa, hakuwekwa chini ya ulinzi. Sina hakika ni kwa sababu gani, lakini yanaweza kuthibitisha kwamba ilikuwa kwa sababu ya kuwa "mwenzetu'.
Sababu hiyo inatumiwa sana na viongozi wasiokuwa na maono ama wito wa kuutumikia umma. Viongozi wanaoamini kwamba kwa vile wana dola, majeshi, silaha zikiwemo bastola, hakuna wa kuwagusa!
Wanafanya wanavyopenda, wanatishia umma pasipo kujali athari zake, wanajenga 'picha mbaya' kwa kizazi cha sasa na baadaye.hawaguswi!
Itakuwaje akitokea 'mwenzetu' mwingine ambaye kwa asili ni jambazi ama mhusika wa vitendo viovu, akavaa kwa jinsi ambavyo Rage alivaa kule Igunga, akiwa na bastola atakayoitumia kukidhi nia ovu dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, itakuwaje?
Kuna msemo unaotumika sana, 'kama baba-kama mwana'. Msemo huo una tafsiri nyingi ikiwemo ya kuanisha matendo, hulka na tabia zinazofanana, zikiwana matokeo ya kurithi.
Rage akiwa kiongozi mwenye hadhi ya kidiplomasia inayotokana na ubunge wake kupitia CCM-chama tawala, aliwasilisha ujumbe gani kwa jumuiya ya wanachama wenzake wakiwemo majambazi waliojificha humo ili kulinda uovu wao?
Rage anaweza kujitetea kwamba alikuwa analinda! Haiwezekani, haikubaliki ikawa hivyo. Atakuwa amepotosha kwa maana mkutanoni pale, hapakuwa na ishara zozote za uvunjivu wa amani ama kitisho kwa mfungwa huyo wa zamani.
Chama, watanzania na jumuiya za kimataifa zinaamini kwamba Tanzania ni mfano wa kisiwa cha amani na utulivu. Sifa ambazo zimechangia kushamirisha umoja wa kitaifa na ongezeko la watalii kutoka nje.
Inapofikia Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, tena kupitia chama tawala anajitokeza hadharani na bastola kiunoni, kuna uhalali wa kuamini uwepo wa amani na utulivu vingali hai hapa nchini?
Kituko alichokifanya Rage kinastahili kuchukuliwa kwa uzito usiohusisha misingi ya kulindana, bali kutekeleza kwa kadri ya sheria, kanuni na taratibu ili umma ubaki kuwa salama na amani.
Rage anaweza kulindwa kwa sababu zozote za kisiasa, lakini kama hali hiyo itatokea, ni dhahiri kwamba 'walinzi' wake watakuwa wamekubali kuuangamiza umma, kuliathiri taifa.
Kwa kadri ulivyo msemo wa 'kama baba-kama mwana', wapo watakaofuata nyendo hizo kwa kuamini kwamba, watalindwa kwa misingi ya 'uenzetu'.
Umma ubasubiri. Usiporidhishwa na hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Rage, umma utachukua hatua dhidi ya waliostahili kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kukomesha vituko vya aina hiyo.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE ambaye kwa sasa yupo nchini Kenya. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, +254 702 115 303 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com.
 
Source: Nipashe; link (http://www.ippmedia.com/frontend/index.php?l=33860)

--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com

Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com  Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma

Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.


--
Karibu Jukwaa la www.mwanabidii.com
Pata nafasi mpya za Kazi www.kazibongo.blogspot.com
Blogu ya Habari na Picha www.patahabari.blogspot.com
 
Kujiondoa Tuma Email kwenda
wanabidii+unsubscribe@googlegroups.com Utapata Email ya kudhibitisha ukishatuma
 
Disclaimer:
Everyone posting to this Forum bears the sole responsibility for any legal consequences of his or her postings, and hence statements and facts must be presented responsibly. Your continued membership signifies that you agree to this disclaimer and pledge to abide by our Rules and Guidelines.
 
 

0 comments:

Post a Comment